Mke Wangu Na Mamake Wachawi Siwezi Kumwambia Dhahiri

 

Mke Wangu Na Mamake Wachawi Siwezi Kumwambia Dhahiri

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je kama nagundua mke wangu ni mchawi anashrikaina na mama yake mzazi nifanye nini pia siwezi kumwambia dhahiri kutokana na jambo lenyewe? 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Inatakiwa tufahamu kuwa uchawi ni miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu ambayo yanafanya amali ya mja iwe ni yenye kukataliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Hata hivyo, yaonyesha kuwa hukutazama hilo wakati unakwenda kuposa na mara nyingi wanaume na wanawake inapofika katika mas-ala ya posa na harusi husahau vipengele vyote tunavyotakiwa tuvitilie maanani na badala yake huangalia mambo ambayo si muhimu kama uzuri, nasaba na utajiri.

 

 

Hata hivyo, hilo lishatokea nawe unatakiwa ufuate mfumo uliowekwa na Uislamu katika kuondosha munkari hapo nyumbani ukianza na yule aliye chini yako katika amri. Aliye chini yako ni mkeo na inafaa umbadilishe yeye mwanzo arudi katika msimamo wa sawa. Katika kuondoa uchafu na maovu huwa kunatumika mkono, ulimi au kuchukia moyoni. Lakini kwa mkeo njia hii ya mwisho haingii, bali unatakiwa ima uondoe kwa mkono au kwa ulimi. Na unapozungumza naye unatakiwa uhimize mabadiliko hayo kutoka kwake wala usiwe ni mwenye kulegeza kabisa msimamo wako. Baada ya kuzungumza naye mpatie muda ajirekebishe na ikiwa hakurekebishika basi utakuwa huna budi kumpatie talaka na kutafuta mke mwengine ambaye hatakuwa ni mshirikina.

 

Atakapoitikia na kumtii Rabb Wake kujitoa katika shirki uendelee kuishi naye kwa wema na kuzidi kumpa mawaidha, na kumpatia mafunzo ya dini yake sawasawa khaswa kwa upande wa 'Aqiydah. AlhamduliLLaah, Alhidaaya ina mafunzo hayo kwa kiasi fulani cha kumfunza: Ingia katika kiungo kifuatacho unaweza kumchapishia makala au asome humu:

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!- إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

 

Kisha baada ya hapo ujaribu kumpatia nasaha mama yake, na ikiwa hutoweza wewe, basi jitahidi uwezavyo kumpatia Shekhe atakayeweza kumpa nasaha naye ajiepushe na shirki kubwa hiyo ambayo inamtoa mtu katika Uislamu. Kufanya hivyo utakuwa umeshajitoa katika jukumu la kukataza maovu uliyoyaona na kutimiza amri ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetuamrisha:

 

 

عن أبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيُّ (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم):  ((مَنْ رَأَى مِنْكُمْ مُنْكَرًا فَلْيُغَيِّرْهُ بِيَدِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِلِسَانِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِقَلْبِهِ وَذَلِكَ أَضْعَفُ الإيمَانِ)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anasema: ((Atakayeona munkari [uovu] basi aubadilishe kwa mkono wake, na asipoweza basi kwa ulimi wake, na asipoweza basi kwa moyo wake [achukizwe] na huo ni udhaifu wa Iymaan)) [Muslim]

 

Tunakutakia mafanikio katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share