Zingatio: Maisha: Siku Moja Au Sehemu Ya Siku

 

Zingatio: Maisha:Siku Moja Au Sehemu Ya Siku

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Raha na karaha ni vitu vinavyoenda sambamba ndani ya maisha ya mtu yeyote. Iwapo ni tajiri au masikini, au ni mfalme au mwananchi; wote wanakutana na mitihani mibaya iliyo khatari.

 

Ni sehemu moja tu ambayo mwanaadamu anahitaji kuishi bila ya karaha, usumbufu, bughudha au kero. Sehemu ambayo ataishi kwa raha milele, akistarehe kwa lahwa za aina kwa aina. Anahitaji sehemu isiyo na maneno ya kuchukiza, usengenyaji, uongo wala uzushi.

 

Hicho ni kipande cha sehemu ya mwanaadamu ambacho hakipatikani hapa duniani. Ni kipande ambacho kinapatikana sehemu moja tu! Nayo ni Jannah. Yeyote aweza kuipata kwa ‘amali zake pamoja na kuambatana na Rahma za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Filimbi ya mashindano inapopigwa inaashiria kwamba mashindano yameanza na mwisho wake ni kupatikana mshindi. Hakutakuwa na maana kuwepo mashindano bila ya mshindi. Halikadhalika kwa maisha yetu hapa duniani. Tuliingia humu tukiwa ni wenye kulia lakini furaha kwa wale wazee wetu wema. Basi elewa kwamba filimbi kimeshalizwa na kuna mstari unahitaji kuguswa ili kumaliza mashindano hayo. Mstari ambao utamtambulisha kwamba ni mshindi ama mshindwa.

 

Maisha ya dunia yana mwisho wake. Kaa ujiulize kwa umri uliopo wewe, ni wangapi hawajafika? Wamefariki na washatangulia pamoja na ‘amali zao. Fika miaka hata mia! Lakini utafumba tu jicho.

 

Hisabu itakapopitishwa siku ya Qiyaamah, watahuzunika mno wema na waovu kwa kupoteza muda kwenye ulimwengu huu. Waovu watalalama kwa kuambulia patupu, na wema watasikitika kwa chumo lao dogo. Lakini sikitiko kuu litawaangukia waovu, ambao wamekosa 'mtoto na maji ya moto'. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atawauliza:

 

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ ﴿١١٣﴾

(Allaah) Atasema: Muda gani mlikaa katika ardhi kwa idadi ya miaka? Watasema: Tumekaa siku au sehemu tu ya siku. Basi waulize wanaohesabu.

 

Ni wazi kabisa kwamba watakuwa na uchungu wa kushindwa kuchuma mema hapa ulimwenguni. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atawaambia:

 

قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١٤﴾

(Allaah) Atasema: Hamkukaa (huko duniani) isipokuwa kidogo tu, lau mngelikuwa mnajua. [Rudia Suwrah Al-Muuminuwn aayah ya 112 hadi 114]

 

Tenda leo mema, mingi jitahidi kuyachuma, usifanye masikhara daima. Dunia ina khatamu, yale yote matamu, tutayaacha milioni ‘awaamu. Huko ndugu uendako, hakuna mshirika wako, ila Rabb wako.

 

 

Share