Skip navigation.
Home kabah

Mjamzito Anatapika Swawm Yake Inafaa?

 

SWALI:



Assalaamu Alaykum, kwanza hongereni kwa michango yenu munayotowe kwa jamii, suala langu ni kuwa mimi nina mimba na huwa natapika baadhi ya muda, je nikitapika wakati nina funga ya ramadhaani, ramadhaani yangu bado imo au itakuwa haimo.  Nategemea nitapata jibu zuri.



 
JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Asli katika hukumu za swawm ni kuwa mwenye mimba au mwenye kunyonyesha na akajiogopea nafsi yake au kilichomo katika tumbo lake hutakiwa afunguwe ameruhusiwa kula na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallam alikuwa akipenda sana kuchukuwa ruhusa anayopewa na Allaah, hivyo ushauri ni kuwa chukuwa ruhusa na udhuru wake utapo ondoka itamlazimu kulipa siku alizo funguwa

Asli katika hukumu za kutapika kwa mwenye funga ni kama hivi:

1.     Kujitapisha kwa makusudi, hili linabatilisha funga kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Abi Hurayrah kuwa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam amesema:

“Atae ghilibiwa na matapishi na kushinda kuyadhibiti kwa kuwa yamemjia kwa nguvu na kumshinda mpaka akatapika pasina hiyari yake, haitoharibika swawm yake; na atae jitapisha kwa makusudi atalipa” lmepokelewa na Tirmithiy, Kitabi cha Swawm kutoka kwa Mtume  Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallam, mlango yaliyo kuja katika aliye jitapisha kwa makusudi.

2.    Kujiwa na matapishi kwa nguvu na kushindwa kuyazuia na ikiwa halikurudi ndani hata kidogo, hili halibatilishi funga.

Kama hali yako iko katika hizo mbili basi hukumu ndio kama hivyo, na lililo bora ni kuto jikalifisha kwani mwenye mimba ni katika walio ruhusiwa kula kwani anahisabika kuwa ni mgonjwa kama kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

(Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine))  [Al-Baqarah:185]

Na Allaah Anajua zaidi