Safari: Kustarehe Kwa Wanandoa Mwezi Wa Ramadhwaan Wakiwa Safarini

SWALI:

 

ASALAMU ALAYKUM

KAMA MTU ANASAFIRI KATIKA MWEZI WA RAMADHAN ANASAFIRI NA MKEWE NA SHARI’AH IMEWARUHUSU KUACHA SWAUMU JEE WANAWEZA KUFANYA TENDO LA NDOA KATIKA MCHANA ULE RAMAMADHANI ILIHAL WAO HAWAKUFUNGA. KAMA WANAWEZA NAOMBA NIPEWE DALILI NA KAMA HAWAWEZI PIA NIPEWE DALILI KWA MAANA YA AYA AU HADITHI.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu kustarehe kwa wanandoa mchana wa Ramadhaan wakiwa safirini.

 

Hakika suala la kustarehe kwa wanandoa mchana wa RamadhAan lipo wazi kwa ufahamu wa Aayah na Hadiyth za bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ufahamu huu unatokana na ile Aayah ambayo inawaruhusu usiku kuweza kustarehe kama Anavyosema Aliyetukuka:

Mmehalalishiwa usiku wa Swawm kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao” (al-Baqarah [2]: 187).

 

Na Akasema tena Aliyetukuka:

Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito” (al-Baqarah [2]: 185).

 

 

Kwa ajili hiyo, kwa aliye mgonjwa au safarini ameruhusiwa kula na kunywa mambo ambayo hayafai kufanywa mchana wa Ramadhaan kwa udhuru wa kishari’ah. Na kwa kuwa starehe hairuhusiwi mchana bila udhuru wa kishari’ah, mtu akiwa na udhuru wa kishari’ah hujuzu kwao wanandoa ikiwa katika hali hiyo kustarehe mchana kama vile walivyoruhusiwa kula na kunywa.

 

 

Na huo ndio usahali na wepesi wa Uislamu katika suala hili na mengineyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share