Mwenye Kufanya Maasi Ya Liwati Anaweza Kurudi Kwa Allah Kutubia?

SWALI:

 

Asalam Alaikum, mimi ninaishi ulaya na huku kuna wanaume wenye kulalana.

Swali langu ni je kama muislamu kafanya hivyo anaweza kurudi kwa mola wake na akaomba tawbah?

 


 

JIBU

 

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Shukurani kwa swali lako hili ambalo linaonyesha mwenye kufanya dhambi hizo anataka kurudi kwa Mola wake. Hakika ni jambo la kushukuriwa kwani wengi wamo katika maasi kama hayo na mengineyo lakini hawajashtuka wala kupata iymaan ya kutaka kurudi kuomba tawbah.

Maasi yoyote yale yakiwa ni madogo au makubwa vipi, hata ikiwa ni kumshirikisha  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hupokea tawbah ya mja Wake, wala mja asikate tamaa kabisa kwani Rahma Za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni nyingi na pana mno kama Anavyosema:.

((Sema: Enyi waja Wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na Rahma ya Allaah. Hakika Allah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Az-Zumar 39: 53].


Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anampenda mja Wake aliyefanya dhambi kisha Akarudi kuomba tawbah.  Hivyo basi linalokupasa ni haraka kukimbilia kufanya tawbah na baada ya hapo la muhimu ni kuwa ufuate masharti yake ambayo ni:

 

1-Kuacha  maovu aliyokuwa anayafanya na kutenda vitendo vyema

kwa wingi

 

2-Kujuta Ayajutie makosa aliyoyafanya na kuazimia kutokurudia maasi hayo

 

3-Aazimie kutourejea tena uovu huo katika maisha yake.

 

Na endapo kosa hilo litahusiana na haki ya mtu hapo litaongezeka sharti la nne nalo:

 

4-Ni kumuomba msamaha uliyemkosea kwa ulichomkosea ikiwa ni kuhusu haki za binaadamu

Hii ni fursa kwako kurudi kwa Mola wako haraka katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhaan ambao ni mwezi wa Rahma na Maghfirah. Hivyo basi kimbilia haraka kufanya tawbah na uazimie kuacha kabisa maasi haya na badala yake ufanye mema mengi.

Bonyeza kiungo kifuatacho upate makala muhimu kuhusu tawbah na uzifanye kazi ili utambue fadhila za tawbah na ubakie salama na maasi hayo:

 

Tawbah

 

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share