Kufanya Mapenzi Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Kwa Ambaye Hajaolewa?

 

 

SWALI:

 

Asalaam alykum, hukumu ya kufanya zinaa kwa asiekua katika ndoa ni kuchapwa fimbo 100 hadharani. Je nini hukumu ya afanyae 'romance' kwa asiekua katika ndoa. Ahsante

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufanya mapenzi tu bila ya kujamiiana. Awali ya yote sijui kwa nini Muislamu atakwenda kufanya mapenzi kabla ya ndoa baada ya Allaah Aliyetukuka kutuambia tusikaribie hata zinaa:

 

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).

 

Hii inaonyesha wazi kuwa jambo la kukaribia zina ni maasi makubwa na Muislamu anapaswa kujiepusha nayo kabisa.  Vile vile haya ni mambo ya uchafu wa  Makafiri, sisi Waislamu tuna sheria zetu zilizowekwa katika mas-ala mapenzi na ndoa, na kuzifuata ndio usalama wetu  kutokana adhabu ya Allaah na pia usalama wetu binafsi.

 

Pia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza pale aliposema:

 

Ni bora kwa mwanamme kupigwa sindano ya chuma katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake [At-Twabaraaniy na Silsilat Al-Ahaadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy].

 

Hata hivyo, kufanya kitendo hicho hakina adhabu maalumu katika sheria ya Kiislamu. Kwa kufanya lile ni funzo kwa wenye kufanya vitendo kama hivyo ambavyo vitawakaribisha na zinaa, sheria imemuachia mtawala wa Kiislamu au Qaadhi atoe adhabu. Hata hivyo, adhabu kama ambazo huitwa Ta’ziyr katika sheria itakuwa duni kuliko ile ya viboko mia moja. Inawezekana ikawa ni viboko kumi au adhabu nyengine yoyote anayohukumu Qaadhi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share