Ukitaka Kitu Sana Ina Maana Unakiabudu?

 

SWALI:

Assalam alaykum, wahusika wa site hii na yeyote anayesoma. Namshukuru Allah kwa kuniwezesha kupata nafasi hii ya kuuliza maswala. Na pia napenda kuwapongeza wahusika wote wa site hii kwani ina mafundisho mengi. Swala langu ni je matamanio yanaweza kumfanya mtu amshirikishe Mungu. Kwa mfano mtu unakitaka kitu fulani kupita kiasi, kila wakati unakiwaza. Siku haipiti kama hujakiwaza, hata usiku unakiwaza. Unamkumbuka Mungu lakini si kwa muda mrefu kama unavyokikumbuka hicho kitu. Au unasoma dhikri lakini akili yako iko katika kitu chengine. Je utakuwa unamshirikisha Mungu? Na je kama unajitahidi kuweka akili kwenye dhikr lakini japo mara moja unakuja kufikiri kitu chengine ufanye nini? Kwani tangu nilipoisoma ile ayah ambayo inasema kitu kama hivi “je umewaona wale ambao wanafanya matamanio yao kuwa Mungu wao?" sijui inamaanisha vile ambavyo nilielezea. 

 

 

 


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Shukrani kwa swali lako zuri na ili kupata ufumbuzi wake itabidi turudi katika Qur’ani ili tutizame aya hizo. Hapa itatosha kunukuu aya mbili ambazo zinazungumzia kuhusu mas-ala ya hawaa (matamanio). Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

“Je! Umemwona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?” (25: 43) na pia: 

 “Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu Akamwacha apotee pamoja na kuwa Ana ujuzi, na Akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na Akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?” (45: 23).

Wafasiri wanasema: “Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake ina maana kuwa mtu awe ni mtumwa wa matamanio yake: mtu ni kufanya analotaka ikiwa Mwenyezi Mungu Ameharamisha, na kutofanya asilopenda japokuwa Mwenyezi Mungu Amelifanya ni wajibu. Ikiwa mtu ataanza kutii kwa namna hii, inamaanisha kuwa mungu wake si Allah bali ni yule anayemtii bila maswali, bila kujali kama anamuita bwana  kwa ulimi) au la, na anachonga sanamu lake na kuliabudu au la. Kwani anapomuabudu moja kwa moja bila suala, inatosha kumfanya yeye mungu na baada hii shirki ya kimatendo mtu hawezi kutolewa kutokuwemo katika uhalifu wa shirki kwa sababu tu hakukiita kitu anacho kiabudu kuwa ni mungu kwa mdomo, wala hakukisujudia”.

Mufasirina wengi wametoa tafsiri hiyo hiyo kwa aya hii. Ibn Jariir amesema: “Amefanya matamanio yake kuwa mungu wake: alitekeleza yanayopenda nafsi yake, bila kujali vitu vilivyoharamishwa na Allah kuwa ni haramu, wala hakuchukulia vilivyohalalishwa na Yeye kuwa halali”. Abu Bakr al-Jaswswaasw anatoa maana ifuatayo: “Anatii matamanio yake kama mmoja anavyomtii Mwenyezi Mungu”. Naye az-Zamakhshari anaeleza kama ifuatavyo: “Anatii matamanio ya nafsi yake: anafuata nafsi yake pindi tu inapomuita, kama kwamba ananitumikia kama anavyotakiwa kutekeza maagizo ya Mwenyezi Mungu”. Ash-Shawkaaniy anasema: “Kafiri amechukua dini yake kwa anavyotamani yeye. Hatamani kitu isipokuwa hukifuata bila kutizama kinachompendeza Allah na kumridhisha au kinacho mchukiza na kumkasirisha. Au maana yake ni anaabudu anachotamani au anachokiona kizuri”. Huyu mtu ambaye ni Muislamu kisha akafanya hayo na kuyafuata huwa amejifananisha na kafiri na hilo halistahiki kwa Muumini.

 

Na Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Haamini mmoja wenu mpaka iwe matamanio yake ni yenye kulingana na mambo niliyokuja nayo” (Hadiith Hasan Swahiih iliyopkewa na Abul Qaasim Isma‘il ibn Muhammad al-Asfahani kutoka kwa ‘Abdullah ibn ‘Amr ibn al-‘Aasw [Radhiya Llaahu ‘anhuma]). Ikiwa mtu hatafuata muongozo huu basi hiko tayari ni cheti cha yeye kufanya anachotaka. Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Hakika katika maneno yaliyopatikana na watu kutokana na Mitume wa kwanza ni: ‘Ukitoona haya basi fanya utakalo’” (al-Bukhaariy kutoka kwa ‘Uqbah ibn ‘Amr al-Answaariy [Radhiya Llaahu ‘anhuma]).

Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuepushe na kufuata matamanio yetu badala yake tuwe tunafuata muongozo ambao Yeye Mwenyewe Ametupatia na pia Mtume Wake.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share