Hirizi Inakubalika Au Shirki?

 

 SWALI:

Asallam allaikum, swali langu ni je? Hazina (hirizi) inakubalika ktk uislam?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu mas-ala ya hirizi. Hirizi imekuwa ni kitu ambacho kinatumika sana kwa watu kuwa na nadharia kuwa huwakinga na mengi. Hii ni nadharia ya makosa kwani mwenye kutukinga na kutulinda ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) peke Yake. Mwanadamu, mnyama, jini au kiumbe chengine chochote hakiwezi kumdhuru mtu wala kumnufaisha.

 

Tufahamu kuwa kuvaa hirizi ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na hiyo ni dhulma iliyo kubwa, amali zote huharibika na ni dhambi ambalo haisamehewi na Allaah. Hayo ni kwa mujibu wa kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Hakika Allaah Hasamehi dhambi ya kushirikishwa na kitu lakini Yeye husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Allaah, basi bila shaka yeye amekwishapotea upotofu ulio mbali na haki” (4: 116).

 

Pia: “Na wakumbushe, Luqmaan alipomwambia mwanawe; na hali ya kuwa anampa nasaha. Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, maana shirki ni dhulma kubwa sana” (31: 13).

 

Miongoni mwa njia za shirki ni kupatiwa hirizi na Maalim, Shaykh na wengineo ambao huwadanganya watu kwa kuwasomea kisomo cha uwongo kisha kuwapa hirizi wavae. Waalimu wa kweli wanasoma kile kisomo kilichosuniwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuondosha kwa mtu ikiwa amekumbwa na jini au amefanyiwa uchawi. Mas-ala ya kutumia hazina au hirizi yamekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo kuwa haramu katika Dini yetu tukufu ya Uislamu.

 

 

Kuhusu hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza: “Mwenye kutungika hirizi hakika amefanya shirki” (Ahmad na al-Haakim, naye akaisahihisha).

 

Na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Aliyetundika hirizi na mwenye kutungika azima basi Allaah Hamtimizii shida yake, na mwenye kutungika azima Allaah Hamuondolei alicho nacho” (Ahmad na al-Haakim, naye akasema Isnadi yake ni sahihi).

 

Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona kipofu mmoja ana kitambaa kakifunga mkononi mwake cha njano: “Kwa nini umefanya hivi?” Akasema: “Hii ni kutokana na ‘wahina’ tatizo lililonikuta”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ivue kwani Allaah Hatakuzidisha ila matatizo tu na kama utakufa na hiyo iko juu yako basi hautafanikiwa milele” (Ahmad).

 

 

Ikiwa una matatizo au ni mgonjwa kinachofaa kwako kufanya ni kujitibu kwa Ruqya (kisomo cha kisheria) ambamo hamna shirki ndani yake. Inatakiwa mwenye kukusomea awe atasoma zile ayah na Surah ambazo ni tiba kwako au wewe mwenyewe mbali na kusoma surah na ayah tofauti za Qur-aan, na uwe ni mwenye kusoma zile ayah ambazo zitakusaidia. Ndio katika hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: “Hakuna ubaya na Ruqya kama hakuna shirki” (Muslim).

 

Ikiwa kutakuwa na kisomo na shirki ndani yake kama ulivyofanyiwa itakuwa haifai. Ukitizama katika hirizi ambayo utakuwa umepatiwa hakuna kitu ndani isipokuwa karatasi isiyo na maandishi au karatasi iliyochorwa tu vitu au pengine kipande cha gazeti kama alivyopata mmoja wetu kuona pindi alipomtoa msichana mmoja hirizi na kuifungua ndani yake.

 

Ayah ambazo zinaweza kukusaidia ni kusoma asubuhi na jioni Suratul Baqarah (2), ayah 1-5, 255-257 na 284-286, Suratul Kaafiruun (109), Suratul Ikhlaasw (112) mara tatu, Suratul Falaq (113) mara tatu na Suratun Naas (114) mara tatu na zote ni kinga pamoja na duaa nyingi ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha.

 

Tunamuomba Allaah Akuponyeshe wewe pamoja na Waislamu wengine wenye maradhi tofauti.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share