Nini Hikma Ya Kuoa Wake Zaidi Ya Mmoja?

 

Aya Zilizodhulumiwa

 

Kimeandikwa na: Dr. ‘Umar bin ‘Abdil-‘Aziyz Qurayshi

Kimetafsiriwa na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y

 

 

Nini Hekima Ya Kuoa Wake Zaidi Ya Mmoja?

 

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً

 

“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” An-Nisaa: 3

 

 

Mambo mawili yanawatatanisha watu katika aya hii, nayo ni:

 

1.     Uko wapo uhusiano baina ya kutowafanyia uadilifu mayatima na kuoa mke zaidi ya mmoja?

2.     Si dhulma hii katika Uislamu kwa mwanamume aruhusiwe kuoa mke zaidi ya mmoja na mwanamke asiruhusiwe kuolewa na mume zaidi ya mmoja?

3.     Kisha kuoa huku mke zaidi ya mmoja kumewekewa sharti la uadilifu. Mwenyezi Mungu Amesema: “Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.”

Na hili ni jambo lisilowezekana, kama ilivyoelezwa ndani ya Qur-aan katika sura hiyo hiyo.

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ وَإِن تُصْلِحُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ غَفُوراً رَّحِيماً

 

“Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia. Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojawapo) kama aliyetundikwa. Na mkisikizana na mkamcha Mungu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu” An-Nisaa: 129

 

4.     Na ikiwa kuoa huko zaidi ya mke mmoja kama ilivyoruhusiwa katika aya, kwa nini basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alioa zaidi ya hao? Alioa wake tisa wakati mmoja.

 

Mambo haya yaliyowababaisha watu yaliyomo ndani ya aya hii ni dalili ya kufahamika vibaya kwa aya, na kutokana na haya kukatendeka aina nyingi za ufisadi na kufru. Na jambo hili wamelifanya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na pia makundi mbali mbali ya mafisadi, na kila anayetaka kuitia ila dini hii akatoka katika njia ya Mwenyezi Mungu.

 

Tunaanza kusahihisha kufahamika vibaya kwa aya hii kwa kujibu hoja moja baada ya nyingine, kwa haraka na kwa muhtasari.

 

Tunasema: huku tukimuomba Mwenyezi Mungu Atusahilishie na atupe tawfiyq;

Kuhusu uhusiano baina ya kutowafanyia uadilifu mayatima na kuoa wake zaidi ya mmoja, kwa mwenye kuzizingatia vizuri aya kumi za mwanzo za Surat An-Nisaa, ataona kuwa karibu aya zote zinaelezea juu ya mayatima, na baada ya aya ya mwanzo ambayo ndani yake imejumuisha baina ya usia wa kumcha Mungu, aya ya pili ikaanza moja kwa moja kuzungumza juu ya mayatima, iliposema:

 

وَآتُواْ الْيَتَامَى أَمْوَالَهُمْ

“Na wapeni mayatima mali yao.” An-Nisaa: 2

 

Na hizi ni aya zenye kuamrisha kuhifadhiwa kwa mali ya mayatima na kuzichunga vizuri zisipotee, na zinakataza kuikaribia isipokuwa kwa njia bora kwa ajili ya kuhifadhi mali hiyo au kuifanyia biashara tena kwa uadilifu. Uadilifu huo unatakiwa ufikie kiwango cha hali ya juu kilichowekewa na Uislamu katika utukufu wa sheria zake na namna ya kulea mayatima na madhaifu.

 

Na katika Hadiyth, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

إِنِّي أُحَرِّجُ حَقَّ الضَّعِيفَيْنِ: الْيَتِيمِ وَالْمَرْأَةِ.

 

“Mimi ninaharamisha (kupotea kwa) haki ya madhaifu wawili; Yatima na Mwanamke.” Ibn Maajah na Ibn Hibbaan na Ahmad na Al-Haakim na imesahihishwa na Adh-Dhahaby

 

Na mwanamke anapokuwa yatima, hapo anakuwa amejumuisha udhaifu mara mbili. Kwa ajili hiyo Uislamu ukaupa umuhimu mkubwa sana ‘haki za mayatima’ na ukasisitiza juu ya uadilifu mkubwa unaotakiwa katika kuhifadhi mali zao katika mandhari bora kupita zote inayonasibiana na umuhimu wa sheria hii.

 

Ndipo Mwenyezi Mungu Aliposema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً

 

“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” An-Nisaa: 3

 

Na hii ni kwa sababu wakati wa ujahilia, mwanamume alikuwa akilea mwanamke yatima nyumbani kwake, kisha binti huyo akishakuwa akapendezwa na uzuri wake na mali yake, mlezi wake hutaka kumuoa kwa sababu ya kujiepusha na gharama za kumlisha na kumvisha, na kwa vile yeye ndiye mlezi na msimamizi wa mambo yake, alikuwa akiruhusiwa kufanya hivyo. Kwa hivyo anamuoa kwa ajili ya mali yake na uzuri wake bila ya kulipa mahari wala kulipa haki yoyote katika haki zake. Ndipo Mwenyezi Mungu Alipokataza kitendo hicho Akaamrisha kuwafanyia uadilifu na kuwalipa mahari kwa ukamilifu kama wanavyolipwa wanawake wengine. Na kama hawataki basi wakaoe wanawake wengine wasiokuwa wao.

 

فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ

 

“basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane” An-Nisaa: 3

 

Kama vile Uislamu ulivyokataza mwenendo huu usiokuwa na uadilifu ndani yake kwa mayatima wanawake, mkabala wake ulikataza pia njia nyingine ambayo mtu alikuwa akilea yatima ambaye hana uzuri wa hivyo wala hana mali, au anakuwa mzuri kidogo na ana mali kidogo, kisha mlezi huyo akataka kumuowa.  Mwenyezi Mungu Akateremsha aya isemayo:

 

وَيَسْتَفْتُونَكَ فِي النِّسَاء قُلِ اللّهُ يُفْتِيكُمْ فِيهِنَّ وَمَا يُتْلَى عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ فِي يَتَامَى النِّسَاء الَّلاتِي لاَ تُؤْتُونَهُنَّ مَا كُتِبَ لَهُنَّ وَتَرْغَبُونَ أَن تَنكِحُوهُنَّ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الْوِلْدَانِ وَأَن تَقُومُواْ لِلْيَتَامَى بِالْقِسْطِ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِهِ عَلِيماً

 

“Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu Anakutoleeni fatwa juu yao, na mnayosomewa humu Kitabuni kukhusu mayatima wanawake ambao hamwapi walichoandikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri yoyote mnayofanya Mwenyezi Mungu Anaijua” An-Nisaa: 127

 

Na katika tafsiri nyingne, wafasiri wa Qur-aan Tukufu wamesema pia kuwa pale Mwenyezi Mungu Alipokataza dhulma na kutowafanyia uadilifu mayatima, Alikataza pia dhulma na kutowafanyia uadilifu wanawake kwa wenye kuoa zaidi ya mke mmoja.

 

Kwa hivyo kama ilivyoamrishwa kuwafanyia uadilifu mayatima, ikaamrishwa pia kuwafanyia uadilifu wanawake kwa wenye kuoa zaidi ya mke mmoja. Uadilifu unalazimika katika yote mawili, na huu ndio uhusiano uliopo katika aya baina ya kutowafanyia uadilifu mayatima na kuoa mke zaidi ya mmoja.

 

“Imesimuliwa na Imam Al-Bukhaariy kutoka kwa Urwa bin Az-Zubayr kuwa alimuuliza Bibi ‘Aaishah juu ya kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:  وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى “Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu.”

Akasema (Bibi ‘Aaishah): “Ewe mwana wa dada yangu, yatima huyu anakuwa ndani ya nyumba ya mlezi wake akishirikiana naye katika mali yake, akapendezwa na mali yake na uzuri wake, na mlezi wake akataka kumuoa bila ya kufanya uadilifu katika kumpa mahari yake akampa kama anavyowapa wengine. Wakakatazwa kuwaoa isipokuwa kama watawafanyia uadilifu, na kuwapa kile wanachostahiki katika mahari, na wakaamrishwa kuwaoa wanaowapenda katika wanawake wasiokuwa wao.”  Amesema Urwa: kuwa Bibi ‘Aaishah alisema: “Hakika watu walimuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kutaka fatwa juu ya aya hii, ndipo Mwenyezi Mungu Alipoteremsha: يَسْتَفْتُونَكَ فِي النِّسَاء “Wanakuuliza nini sharia ya wanawake”. Akasema Bibi ‘Aaishah: “Kauli ya Mwenyezi Mungu katika aya hii pale Aliposema “na mnapenda kuwaoa,” kwa ajili ya uyatima wao ikiwa ni mpungufu wa mali au uzuri. (Lakini) Walikatazwa kuwaoa wale waliopendezwa na mali yao au uzuri wao katika wanawake isipokuwa kama watawafayia uadilifu kwa ajili ya kupenda kwao kuwaoa ikiwa wana upungufu wa mali au uzuri.” Al-Bukhaariy na Muslim

 

2- Wakasema: ‘Uislamu umemdhulumu mwanamke pale uliporuhusu kuoa mke zaidi ya mmoja na kuziumiza nyoyo zao, kisha hawakufanya uadilifu wa kuwaruhusu na wao kuolewa na mume zaidi ya mmoja!!!’

 

Tunasema kwanza: Nani aliyemdhulumu mwanamke? Wakasema: Uislamu.

Tunasema: Na huu Uislamu ni dini ya nani? Wakajibu: Dini ya Mwenyezi Mungu.

Tunasema: Kwa hivo aliyemdhulumu mwanamke ni Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

كَبُرَتْ كَلِمَةً تَخْرُجُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ إِن يَقُولُونَ إِلا كَذِبًا

 

“Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu.” Al-Kahf: 5

 

Tunasema pia: Je Mwenyezi Mungu Anaweza kudhulumu? Mwenyezi Mungu Anasema:

 

وَلا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na Mola wako Mlezi Hamdhulumu yeyote” Al-Kahf: 49

 

 

Na Akasema katika aya nyingine:

 

وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

 

“Wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja” Fusswilat: 46

 

Na katika Hadiyth Al-Qudsy Amesema:

 

يا عبادي إني حرمت الظلم على نفسي وجعلته بينكم محرما فلا تظالموا

 

“Enyi waja wangu, Hakika Mimi nimejiharamishia dhulma na Nikaijaalia baina yenu iwe haramu, kwa hivyo msidhulumiane.” Muslim

 

Kisha tunasema: Na kwa nini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amdhulumu mwanamke? Kisha kwa maslahi ya nani? Amdhulumu kwa maslahi ya mwanamume? Au kwa ajili ya uzuri wake mwanamume huyu kama wanavyosema, au kwa sababu gani?

 

Kwani mwanamke si kiumbe cha Mwenyezi Mungu, na mwanamume pia ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu? Kwa nini basi Mwenyezi Mungu Amdhulumu kiumbe kwa ajili ya kumpendelea kiumbe mwengine? Na kwa nini Uislamu umehalalisha kuoa mke zaidi ya mmoja kwa ajili ya maslahi ya mwanamume, au kwa ajli ya maslahi ya mwanamke katika daraja ya mwanzo?

Tuelimisheni enyi watu. Munayatizama vipi mambo haya, au ni wapungufu wa akili?!!

 

Ifuatayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Aliposema: “Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane.”

Hapa Mwenyezi Mungu Alifaridhisha au Aliwajibisha? Hii ni rukhsa. Kwa hivyo kuoa mke zaidi ya mmoja siyo wajibu wala siyo fardhi, bali ni rukhsa iliyotolewa na Mwenyezi Mungu.

 

Kisha tunauliza: Kwani ni dini ya Kiislamu peke yake iliyoamrisha kuoa mke zaidi ya mmoja au ndiyo iliyoanzisha mwenendo huu?

 

Waislamu na watu wote kwa ujumla, wale wenye kufuata dini mbali mbali na wasiokuwa na dini wanaoa wake zaidi ya mmoja, tena wao wanaoa bila ya kiwango wala hesabu, bila kutimiza wajibu na bila ya kufanya uadilifu. Wanaoa bila kufuata kanuni wala kulinda uhusiano wa mke na mume, na bila ya kuulinda ubinadamu.

Kwa nini basi ulipokuja Uislamu ukataka kuyaweka sawa mambo haya ya kuoa mke zaidi ya mmoja katika nyanja zake zote, kwa kuweka idadi maalum ya kutoruhusu kuoa zaidi ya wane na kupanga namna kwa kuweka sharti la uadilifu na sharti la uwezo wa kuongeza.

Sasa kwa kufanya hivyo ndiyo Uislamu unakosolewa badala ya kusifiwa? Na kwa nini unakosolewa Uislamu peke yake wakati amri hii imekuja ndani ya vitabu vyote vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, na kufuatwa na umma zote?

 

Wakati wa ujahilia kabla ya kuja Uislamu, watu walikuwa wakioa zaidi ya mke mmoja. Warumi walikuwa wakioa wake zaidi ya mmoja. Wayunani walikuwa wakioa wake zaidi ya mmoja, Waajemi walikuwa hiyvo hivyo, hata mfalme wao alikuwa akioa zaidi ya wake mia moja. Katika dini ya Mayahudi wanaruhusiwa kuoa wake zaidi ya mmoja. Ndani ya Taurati imeandikwa kuwa Mitume wanaotokana na Bani Israil walikuwa wakioa wake kwa makumi na mamia. Imeandikwa kwa mfano kuwa ‘Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alikuwa na wake mia tatu, na Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) alikuwa na wake mia saba na vijakazi mia tatu.’

 

Katika Injili ya Manasara hapana panapokatazwa kuoa wake zaidi ya mmoja, na wakuu wa makanisa wanaoharamisha kuoa zaidi ya mke mmoja hawana egemeo lolote la kisheria. Wameitoa wapi hukmu hiyo? Kwa nini kanisa linakifumbia macho kitendo cha kuoa zaidi ya mke mmoja kwa Wakristo wa bara la Afrika, wakati kitendo hicho kinachofanywa hata na makasisi wa baadhi ya makanisa ya Afrika, kisha kanisa hilo hilo linaharamisha kufanya hivyo kwa Wakristo wa Ulaya?

 

Na sisi tunauliza; Kwani Dini ya Kiislamu ndio iliyovumbua kuoa wake zaidi ya mmoja kinyume na mafundisho ya dini nyingine zilizotangulia? Sasa ikiwa dini zote – zenye kufuata maamrisho kutoka mbinguni na wasiokuwa na dini - wameruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja, kwa nini basi Uislamu peke yake ulaumiwe?

Kisha tunasema pia; Je, Wakristo hivi sasa na watu wa Ulaya na watu wa nchi za Magharibi wametoshelezwa na mmoja na hawajatafuta wengine?

 

Hawajatafuta urafiki wa muda mfupi au mrefu na wanawake wengine? Kwa nini basi wanaharamisha kuoa zaidi ya mke mmoja wakati wanahalalisha kuzini na mwanamke zaidi ya mmoja? Kwa nini wanaharimisha halali na wanahalalisha haramu? Kwa nini mtoto mchanga anatupwa au analelewa akiwa ni mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa? Na kwa nini hanasibishwi na baba yake wa kweli?

 

Zinaa imekithiri (imezidi) kwa upande wa Wakristo huko Ulaya na Marekani na katika jamii zote zilizoharamisha kuoa mke zaidi ya mmoja. Na watoto waliozaliwa nje ya ndoa wamekithiri huko Marekani. Idadi yao imeongezeka kwa asilimia sitini ‘60%’, na Ulaya idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia zaidi ya sabini na tano ‘75%’. Na katika baadhi ya nchi zilizoharamisha kuoa wake zaidi ya mmoja, idadi yake inatisha sana, kwani watoto waliozaliwa nje ya ndoa inakaribia kuwa watoto watatu katika kila wane.

Wakati huo huo idadi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa katika nchi zinazohalalisha kuoa mke zaidi ya mmoja ni moja tu katika kila mia 1%.

 

Wanasema wataalamu wenye kuudurusu Uislamu katika watu wa Magharibi, wale wenye insafu kuwa; ‘Hii inatokana na sheria ya kuruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja iliyothibitishwa katika dini ya Kiislamu pamoja na uadilifu wake na usafi wake na sitara iliyo ndani yake.’

 

Nilitangulia kusema kuwa; Uislamu sio ulioanzisha ada ya kuoa zaidi ya mke mmoja, bali Uislamu umekuja kuweka idadi ya wake wane pamoja na masharti na hukmu, kwa sababu wakati wa Ujahilia (kabla ya kuja Uislamu) watu walikuwa wakioa wake kwa makumi na mamia.

Imepokelewa kuwa aliposilimu Aslam Ghaylaan Ath-Thaqafiy alikuwa na wake kumi, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamuambia:

 

اختر منهن أربعا وفارق سائرهن

 

“Chagua wane kati yao na uwaache waliobaki.” Ibn Maajah na Ahmad na Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibni Maajah.

 

Na wapo pia waliosilimu wakiwa na wake wanane na wengine kumi, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwataka wabaki na wane tu.

 

Kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuoa wake tisa, hiki ni kitendo kinachomhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) peke yake, kama tutakavyoelezea kila tukiendelea mbele.InshaAllaah.

 

Hekima ya mtu wa kawaida kuwekewa idadi ya wake wane inajulikana kuwa huu ndio upeo wa uwezo wake katika kuwasimamia na kutimiza wajibu wake juu yao katika kila Nyanja ya maisha. Na hii ni pamoja na uwezo wa kufanya uadilifu baina yao.

 

Mtu akiuliza; kwa nini Uislamu umekuja kukikubali kitendo cha kuoa mke zaidi ya mmoja na usikataze na kuuondoa kama ulivyoondoa baadhi ya sheria za zamani?

Tunasema: Uislamu umefanya hivyo kwa sababu zinazohusiana na adabu na mwenendo mwema, na pia kwa sababu za kijamii na kwa sababu za kibinafsi.

 

Uislamu ni Neno la Mwenyezi Mungu la mwisho Alilohitimisha kwalo Risala Zake, kwa ajili hiyo Neno hilo likaja na ujumbe uliokusanya kila kitu. Ujumbe unaokubalika kila pembe ya dunia na kila zama na kila mtu. Uislamu haujaweka sheria kwa ajili ya watu wanaoishi mjini ukawasahau wanoishi majangwani na mashambani. Haujaweka sheria kwa ajili ya wanoishi katika sehemu za baridi ukawasahau wa sehemu ya joto. Uislamu unachunga haki ya kila mtu pamoja na mambo yote ya dharura kwa waja kila mmoja kutokana na maslahi yake.

Wapo miongoni mwa watu wenye hamu kubwa ya kupata watoto, lakini wamejaaliwa kupata mke asiyezaa kutokana na umbile lake au kutokana na maradhi. Si litakuwa jambo la ukarimu kutoka kwake mwanamke huyo akimruhusu mumewe aoe ili apate kile anachokitamani, na wakati huo huo yeye anabaki mahali pake na haki zake zinadhaminiwa?

 

Wapo wanaume wenye uwezo mkubwa na nguvu za kufanya kitendo cha jinsia, hamu yake daima inakuwa kubwa, lakini amejaaliwa kupata mke mwenye uwezo mdogo na nguvu ndogo, au mgonjwa, au siku zake za hedhi ni nyingi, au mfano wa aina hiyo, na mwanamume anakuwa hana uwezo wa kusubiri. Kwa nini basi asiruhusiwe kuoa mwengine wa halali badala ya kwenda kutafuta mwengine wa nje?

 

Wapo wanawake waliokuwa vizuka wangali bado vijana wadogo, na wapo waliotalikiwa wakiwa bado wadogo, huenda pia idadi ya wanawake ikawa ni kubwa kupita ya wanaume – hasa kutokana na vita vinavyowamaliza wanaume na vijana – kwa ajili hii ni kwa maslahi ya jamii na maslahi ya wanawake pia kuolewa badala ya kuishi umri wao wote wakiwa vizuka au wajane wakinyimwa maisha ya ndoa, na utulivu na mapenzi yaliyomo ndani yake na pia wakinyimwa neema tumaini la kuweza kwa mara nyingine kuwa mama.

Kwa kina mama wa aina hii wenye uwezo wa kuolewa ambao ni wengi kupita idadi ya wanaume itawabidi waangukie mojawapo ya matatu yafuatayo:

 

1.     Waishi maisha yao yote wakiungulika kwa kukosa kuolewa.

2.     Ama waharibike na kugeuka kuwa chambo rahisi kwa wanaume wanaopenda kuishi nao kwa haramu.

3.     Au waruhusiwe kuolewa na wanaume waliokwishaoa wenye uwezo wa kuishi nao kwa ihsani na wenye uwezo wa kuwasimamia kifedha.

 

Uwekezano wa mwanzo: ni dhulma kubwa kwa mwanamke ambaye hajafanya kosa lolote hata akastahiki kufanyiwa hivyo.

 

Ama uwezekano wa pili: Uhalifu mkubwa dhidi ya haki ya mwanamke na dhidi ya jamii na dhidi ya khulqa njema, na hili nasema kwa masikitiko kuwa ndiyo njia walioichagua watu wa Magharibi. Wao wameharamisha kuoa zaidi ya mke mmoja wakahalalisha kuwa na wanawake na wapenzi zaidi ya mmoja, eti kwa sababu imewabidi wawe na wanawake zaidi ya mmoja, lakini kinyume na mwenendo na tabia njema na kinyume na ubinadamu, kwa sababu mwanamume anamaliza hamu yake na matamanio yake bila ya kulichukua jukumu lolote juu ya natija ya kitendo chake hicho.

 

Ama uwezekano wa tatu: ndio pekee wenye uadilifu ndani yake na uliotahirika na wa kibinaadamu na unakubaliana na mwenendo na tabia njema, na ndio tiba ya maradhi haya, na haya ndiyo yaliyokuja nao Uislamu na ukatoa hukmu juu yake.

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللّهِ حُكْماً لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

 

“Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?” Al-Maaidah: 50

                                                       

Huku ndiko kuoa zaidi ya mke mmoja kunakopigwa vita na nchi za Magharibi na Wakristo. Wakachukizwa nako wakati wamependezwa kuwa na wapenzi na kufanya kitendo cha jinsia na wanawake wengi bila ya kuwa na uhusiano wa ndoa na bila ya mipaka wala idadi. Wamefanya hayo kinyume na sheria na kinyume na adabu na bila ya kumheshimu mwanamke wala kizazi kitakachopatikana kutokana na kitendo kile cha kinyama. Sasa ni kundi lipi lenye msimamo bora, na ni kundi lipi lipo katika njia iliyoongoka?

 

Katika Uislamu imeruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja kwa sharti la uwezo wa mali na hali, na ikiwa sharti hizi mbili haziwezi kupatikana basi hairuhusiwi kuongeza. Kwa hivyo Muislamu lazima awe na uhakika kuwa anao uwezo wa kufanya uadilifu baina ya wake zake katika chakula na vinywaji na makazi na mavazi Ikiwa hana uhakika kuwa ataweza kusimamia yote haya kwa usawa na uadilifu basi ni haramu kwake kuongeza mke zaidi ya mmoja.

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً

 

“na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu”

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

من كانت له امرأتان يميل لإحداهما على الأخرى جاء يوم القيامة يجر أحد شقيه ساقطاً أو مائلاً

 

“Mwenye kuwa na wake wawili akampendelea mmoja wao dhidi ya mwengine atakuja siku ya Qiyaama akiwa ubavu wake mmoja umeanguka au umepinda”

Abu Daawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhiy na Imaam Ahmad, na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy.

 

Na kupendelea kulikokusudiwa katika Hadiyth hii upendeleo katika haki zake mwanamke, jambo lisilohusiana na moyo, kwa sababu uadilifu uliotajwa katika aya ni uadilifu katika kuisimamia nyumba kwa hali na mali. Na hili ni jambo linalowezekana. Lakini haukusudiwi upendeleo katika moyo. Kwa sababu mwanamume anaweza kuwa na nishati usiku mmoja na usiku mwingine asiwe na nishati, kwa hivyo kinachokusudiwa ni uadilifu katika hali na mali na mwanamume anatakiwa amche Mungu katika jambo hili.

 

Kuhusu kauli yao kuwa; kwa nini Uislamu umemruhusu mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja lakini haukumruhusu mwanamke kuolewa na mume zaidi ya mmoja? Hakika hili ni jambo la kustaajabisha sana!!!

Itakuwaje mwanamke awe na mume zaidi ya mmoja, atawezaje kuwaridhisha wote, atawezaje kuwakusanya? Mtoto atanasibishwa na yupi kati ya waume hao, na mimba itakuwa ya nani?

Nani atakayekuwa msimamizi wa aila (familia)? Yeye ndiye atakayewasimamia waume zake au atamsimamia mmoja wao au atawasimamia wote? Sheria gani hii na dini gani hii na tabia gani hizi?

Wanataka kumgeuza mwanamume awe kitu gani? Na wanataka kumgeuza mwanamke awe kitu gani? Na wanataka kuigeuza jamii yetu iwe kitu gani?

 

 

3-      Wakasema pia: Uislamu umeruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja kwa sharti la uadilifu:

 

Mwenyezi Mungu Amesema:

 فإن خفتم ألا تعدلوا فواحدة Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu. Kisha Qur-aan ikabainisha kuwa uadilifu huu hautawezekana ولن تستطيعوا أن تعدلوا بين النساء ولو حرصتم Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata mkikakamia.

 

Kwa hivyo kuoa zaidi ya mke mmoja ni haramu.kwa nassi ya Qur-aan!! Na kama inaruhusu basi Qur-aan inagongana yenyewe kwa yenyewe.

 

Tunasema: Maneno haya ni katika vichekesho vinavyoliza na yanatukumbusha maneno ya walevi na wahuni.wenye kutumia dalili kama hizi zenye kuchekesha mfano wa yule aliyelewa, na alipowaona watu wakitoka msikitini akawaambia: “Mwenyezi Mungu hajasema; ‘Ole wao wenye kulewa’ bali Alisema: فويل للمصلين ‘Ole wao wanaoswali,’

Bila kuikamilisha aya inayosema:“Ambao wanapuuza Swalah zao.”

 

Katika mfumo huu, tunakuta watu wanazungumza juu ya Uislamu na kuifasiri Qur-aan kwa njia zao.

 

Hakika Qur-aan imesema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً

 

“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.”

 

Hili ni kweli, lakini uwezo uliokusudiwa hapa ni uwezo wa kufanya uadilifu katika makazi na malipo na maisha na mengine ya mfano huo kwa kiasi cha uwezo wako wote.

Na aya nyingine inasema:

ولن تستطيعوا أن تعدلوا

 

“Wala hamtaweza kufanya uadilifu”

 

Aya hii inatubainishia kuwa uadilifu usio na mipaka hauwezekani kupatikana, kwa hivyo kilichokusudiwa hapa ni uwezo wa kufanya uadilifu wa moyo, katika kupenda na kumili kunakohusiana na hisia za kibinadamu, ‘Mapenzi’.

Haya ni mambo yanayohusiana na moyo, na mwanadamu hana uwezo wa kuyamiliki baraabara, na nyoyo ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, Anazigeuza Apendavyo. Kwa hivyo ikiwa mume atampenda mmojawapo wa wake zake zaidi ya mwengine, kwa sababu yoyote ile, hii haina maana kuwa amdhulumu mwengine, au asifanyie uadilifu baina yao. Bali anatakiwa kama Alivyosema Mwenyezi Mungu: “Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliyetundikwa.” Akageuka kuwa si mke wala si mjane. Na uadilifu unaotakiwa ni kutoyadhihirisha mapenzi hayo kwa wengine.

 

Huyu hapa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekuwa akimpenda Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) kupita wake zake wengine, lakini hakuwa akiyadhihirisha kwa wenzake, na alikuwa akifanya uadilifu baina yao kwa kila anachomiliki, kisha akisema:

 

(اللهم إن هذه قسمتي فيما أملك فلا تلمني فيما تملك ولا أملك)

 

“Mola wangu, hakika hii ni sehemu yangu katika ninachomiliki, kwa hivyo usinilaumu katika Unachomiliki na wala similiki.” Abu Daawuud na At-Tirmidhiy na Ibni Maajah

 

Na hapa anakusudia kuumiliki moyo ambao unaweza ukamili zaidi kwa mke mwengine kupita wenzake.

 

“Na alikuwa anapokwenda safari akipiga kura kwa ajili ya kumchagua mmoja wao, na yeyote itakayomuangukia ndiye atakayemchukua katika safari hiyo.” Al-Bukhaariy

 

Alifanya hivyo kwa ajili ya kuwaridhisha, na kwa njia hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alihiji na wake zake wote.

 

Mwenyezi Mungu Amesema:

 

وَإِن تُصْلِحُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ غَفُوراً رَّحِيماً

 

“Na mkisikizana na mkamcha Mungu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu.” An-Nisaa: 129

 

Na maana yake ni kuwa; Kama mtasikilizana katika mambo yenu, mkayafanya yawe mema, kisha mkafanya uadilifu baina yenu katika yale mnayomiliki, na mkamcha Mungu, katika mambo yenu yote, hapo Mwenyezi Mungu Atakusameheni katika yale mliyomili kidogo bila ya uwezo wenu wa kuumiliki moyo. Tafsiri ya Ibn Kathiyr

 

 

4-      Kwa kumaliza tunasema: Wakasema kuwa ikiwa sheria hairuhusu kuoa zaidi ya wake wane, kwa nini basi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaoa zaidi ya hao, ikafika idadi yao wake tisa?

Wakasema pia kuwa eti hii ni dalili ya kupenda kwake wanawake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Tunasema: Inajulikana kuwa mke wa mwanzo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Bibi Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Llaahu ‘anha). Alimuoa akiwa yeye ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na tano, na wakati huo Bibi Khadiyjah (Radhiya Llaahu ‘anha) alikuwa na umri wa miaka arubaini na tano aliyewahi kuolewa kabla ya hapo na wanaume wawili, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuongeza mke mwingine wakati wote alipokuwa naye Bibi Khadiyjah, mpaka alipofariki Bibi Khadiyjah, na wakati huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka hamsini au hamsini na moja.

 

Tunauliza; Je, mtu wa aina hii ni mwenye kupenda wanawake? Na Bibi Khadiyjah ni mke wa pekee aliyemuoa kwa kutaka mwenyewe, na hii ni kwa sababu alimuoa kabla ya kuanza kuremshiwa wahyi kutoka mbinguni. Lakini wake zake wote waliobaki, aliwaoa kwa amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa sababu baada ya kuanza kuteremshiwa wahyi alikuwa hafanyi lolote bila ya kuletewa wahyi.

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَى إِنْ هُوَ إِلا وَحْيٌ يُوحَى

 

“Wala hatamki kwa matamanio Hayakuwa haya ila ni ufunuo uliofunuliwa” An-Najm: 3-4

 

Baada ya kupewa utume akawa na kanuni inayokhitalifiana na watu wengine. Kwa hivyo kuoa kwake idadi hii ya wanawake lilikuwa ni jambo lenye kuhusiana na utume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Na inajulikana kuwa Mitume wote (‘Alayhimus Salaam) walikuwa na mambo yanayowahusu wao tu, tofauti na watu wengine katika umma wao. Na kuhusika huku si katika mambo ya kuoa tu, bali ni katika mambo mengi mengine, ambayo hapa si mahali pake kuyataja, kwa sababu wasaa hautoshi kuyaelezea yote.

 

Bila shaka tukiweka upande kuhusishwa huku, tutaona kuwa ndani yake pana hekima kubwa, bali hekima nyingi tulizozifahamu na tusizozifahamu.

 

Pana hekima za kisheria na za kijamii na za kielimu nk. Kwa Hekima Yake Mwenyezi Mungu Alitaka wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) wabaki kuwa chini yake asiwataliki, kwa sababu akiwataliki haitokuwa halali kwa mwengine yeyote kuwaoa.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّهِ وَلَا أَن تَنكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِن بَعْدِهِ أَبَدًا إِنَّ ذَلِكُمْ كَانَ عِندَ اللَّهِ عَظِيمًا

 

“Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.” Al-Ahzaab: 53

 

Na Mwenyezi Mungu alipowahiarisha wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) iwapo wanamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na nyumba ya Akhera, na wote walipochagua kumtaka Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na nyumba ya akhera, Mwenyezi Mungu Akawatunukia zawadi ya kumpa amri Mtume Wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) asioe tena baada ya hao.

 

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Akasema:

 

لا يَحِلُّ لَكَ النِّسَاء مِن بَعْدُ وَلا أَن تَبَدَّلَ بِهِنَّ مِنْ أَزْوَاجٍ وَلَوْ أَعْجَبَكَ حُسْنُهُنَّ إِلَّا مَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ وَكَانَ اللَّهُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ رَّقِيباً

 

“Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipokuwa yule uliyemmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu Anachungua kila kitu.” Al-Ahzaab: 52

 

Kwa hivyo Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyempa amri ya kuoa, na Yeye Ndiye Aliyemkataza kuoa wengine baada ya hao na hakumruhusu kuwataliki.

Sasa kutokana na haya ndiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) analaumiwa? SubhanaAllaah!!

 

Kisha kuko wapi huko kupenda wanawake wanakomtuhumu, wakati alifanya hivyo kwa amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa Bibi Khadiyjah (Radhiya Llaahu ‘anha) peke yake ndiye aliyeolewa kabla ya kuanza kuteremshiwa wahyi, na kitendo hicho hakiwezi kuitwa kuwa ni cha kupenda wanawake.

 

Isitoshe, wake zake wote waliobaki hawakuwa bikira isipokuwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) peke yake, na wakati alipomuoa alikuwa binti mdogo mwenye umri wa miaka tisa, na kutokana na umri wake na mwili wake, uliokuwa mwembamba sana hakuwa na umbo lenye kuvutia, lakini Mwenyezi Mungu alitaka amuoe, Akamteremsha Jibriyl akiwa na sura ya Bibi ‘Aaishah, na Mwenyezi Mungu Akamuonyesha sura hiyo mara nyingi usingizini mpaka alipomuoa. Na kutokana na ndoa hii, usuhuba wake na Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) ulizidi kupata nguvu, kama vile ulivyozidisha nguvu usuhuba wake na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kumuoa Hafswah binti ‘Umar. Na katika wakati huo huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuozesha ‘Uthmaan binti zake wawili Ruqayah na Ummu Kulthuum, mmoja baada ya mwengine. Na pia alimuozesha binti yake Fwaatimah kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhum ajma’iyn).

 

Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamuoa Zaynab binti Jahsh kwa hekima ya kisheria inayojulikana, kisha akamuoa Juwayriyah bint al-Haarith, na huyu alikuwa binti wa kiongozi wa kabila lao. Alifanya hivyo kwa ajili ya kuzikaribisha na kuizunganisha nyoyo za watu wa kabila lake, na matunda yake ni kuwa watu wa kabila lake wote walisilimu mara baada ya kuolewa Bibi Juwayriyah. Wakati huo huo katika Waislamu kila aliyekuwa na mateka anayetokana na kabila la Banu Mustaliq alimuacha huru huku akisema: ‘Shemeji zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hawa.”

 

Na Bibi Swafiyah bint Huyay Al-Akhtwab alikuwa binti wa kiongozi wa kabila Mayahudi, na pia Abu Sufyaan alifurahi aliposikia habari za kuolewa binti yake Ramlah ‘Ummu Habiybah’ na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), akasema: “Atapata wapi mfano wa Muhammad, huyu ni kijana asiyekuwa na kiburi hata chembe.”

 

Alikuwa siku zote akiona fahari kuwa binti yake aliolewa na Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) mpaka Mwenyezi Mungu Alipomjaalia kusilimu.

 

Ummu Salamah, baada ya kuuliwa mumewe katika vita vya Uhud, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuomba amuoe kwa ajili ya kumsaidia kuwalea wanawe mayatima, na kwa njia hiyo hiyo alimuoa Sawdah binti Zam’ah na Zaynab bint al-Haarith.

 

Na hivi ndivyo ilivyo, kila mke aliyeolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kulikuwa na kisa chake na sababu zake na hekima yake.

 

Na kubaki kwao chini ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kwa ajili ya hekima kubwa, kwa sababu wao ndio waliokuwa mfano wa waalimu kwa Waislamu baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuondoka duniani, na hii ni kwa sababu wao walikuwa na elimu juu ya yote aliyokuwa akifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ndani ya nyumba yake. Wakawafunza Waislamu wanawake kwa wanaume.

 

Juu ya yote haya, sisi binadamu tunaweza kuzijua baadhi ya hekima, wakati hekima nyengine inaweza kujificha tusiweze kuzijua, lakini sisi tunaijuwa dini yetu, na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Ametakasika na udhaifu huo, na kwamba hekima Yake haina nuksani wala makosa, na tunajua kuwa ikiwa mwanadamu haielewi hekima yoyote ile kwa ukamilifu, hii ni kwa sababu yeye ni mja dhaifu anayeweza kufanya makosa, lakini inambidi atambue kuwa hekima ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na haina makosa wala udhaifu.

 

Lakini hawa wenye kuitoa makosa hekima ya Mwenyezi Mungu au dini ya Mwenyezi Mungu au kumtoa makosa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kama kwamba hawaelewi kuwa kwa kufanya hivyo wanamtoa makosa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Anayatoa makosa Mafundisho na Hekima ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), wakati yeye ni kipofu asiyeweza kuona uhakika wote, mjinga asiyejua maana.

Mwenye kuutafuta ukweli akauliza, ataujua, na utambainikia, lakini mwenye maradhi moyoni mwake, huwezi kumsaidia kwa chochote.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

إِنَّكَ لا تَهْدِي مَنْ أَحْبَبْتَ وَلَكِنَّ  للَّهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ

 

“Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu Humwongoa Amtakaye. Na Yeye Ndiye Anawajua zaidi waongokao.” Al-Qaswas: 56

.

 

Share