Skip navigation.
Home kabah

Jiepushe Na Moto Wa Jahannam Pamoja Na Familia Yako

 

24 Swafar 1427 - 24-03-2006

 

  

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ))

((Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa)) [At-Tahriym  6]

 

'Aliy bin Abi Talhah amepokea kutoka Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba amesema kuhusu aya hii: "Mtiini Allaah سبحانه وتعالى   na jiepusheni na kumuasi Allaah سبحانه وتعالى na amrisheni familia zenu kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى ili Allaah سبحانه وتعالى Awaokoe na moto wa Jahannam". [At-Twabariy 23: 491]

 

Kutokana na ayah hiyo, ni wajib wa Muislamu kuwafundisha watu katika familia yake ikiwa ni mke au mume, watoto, ndugu, wazazi na kadhalika, mambo yaliyo fardhi kufanya na kuwakataza yaliyoharamishwa.

Hadiyth hii inathibitisha maana ya aya hiyo:

عبد الملك بن الربيع بن سَبْرَة، عن أبيه، عن جده قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((مروا الصبي بالصلاة إذا بلغ سبع سنين، فإذا بلغ عشر سنين فاضربوه عليها((   رواه الإمام أحمد، وأبو داود،  وقال الترمذي: هذا حديث حسن.

Imetoka kwa 'Abdul-Malik bin Ar-Rabiy' bin Sabrah kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwamba amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Amrisheni watoto kuswali watakapotimia miaka saba, na wapigeni (ikiwa hawatoswali) watakapotimia miaka kumi)) [Imaam Ahmad, Abu Daawuud, na kasema At-Tirmidhy  Hadiyth Hasan]

Na kuwaamrisha watu wako, mfano watoto wako kuswali ni kudhihirisha mapenzi yako kwao kwani hutopenda watoto wako waingie motoni, hivyo unapowaonea huruma asubuhi wasiamke kuswali Swalah ya Alfajiri, sio maana kuwa unawependa bali ni kinyume chake, kwa vile unawasababisha wawe miongoni mwa watu wa motoni.  Watu wa Peponi watakapowaona watu wa motoni watawauliza sababu ya kuwaingiza huko motoni na sababu mojawapo watasema kuwa ni kwa ajili ya kutokuswali:

((كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ))   ((إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ))   ((فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءلُونَ))  (( عَنِ الْمُجْرِمِينَ))   ((مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَر))َ   ((قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ))

 ((Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma)) 

((Isipokuwa watu wa kuliani) 

((Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana)) 

((Khabari za wakosefu)) 

((Ni nini kilichokupelekeni Motoni?)) 

((Waseme: Hatukuwa miongoni waliokuwa wakiswali))

[Al-Mudathhir: 38-43]

 

Bila ya shaka kuamrisha familia yako kuswali ni jambo gumu sana na ndio maana Allaah سبحانه وتعالى Alipoamrisha jambo hili Alitutaka tuendelee nalo kwani linahitaji kuwa na subira nalo, kama Anavyosema Allaah katika ayah ifuatayo, ambayo 'Umar ibnul-Khatwaabرضي الله عنه  alikuwa akiisoma huku akiamsha familia yake kuswali:

((وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا))

((Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo)) [Twaaha: 132]

 

Ayah hiyo ya mwanzo inaelezea hali ya huo moto kuwa:

 

((وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ))

((kuni zake ni watu na mawe))

Watu hao ni sisi wana wa Adam na mawe ni masanamu yaliyochongwa yaliyokuwa yakiabudiwa kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:

((إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ))

((Hakika nyinyi na hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu)) [Al-Anbiyaa: 98]

Kisha Malaika wanaowaingiza hao watu motoni hawana huruma kabisa kwa watu waliomkufuru Allaah سبحانه وتعالى, hukimbilia haraka kumtii Allaah سبحانه وتعالى kuwaingiza watu motoni bila ya kuchelewa hata upepesi wa macho. Malaika hao wanaitwa Az-Zabaaniya (walinzi wa moto wa Jahannam) kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:

((سَنَدْعُ الزَّبَانِيَة))

((Nasi tutawaita Mazabania!)) [Al-'Alaq: 18]

Basi tujitahidi kutimiza Swalah zetu kama zinavyopasa na kuwaamrisha familia zetu pia watimize Swalah ili tujiepushe sote na moto huo mkali wa Jahannam.

 

 

***********