Anataka Kuoa Lakini Hajui Taratibu Za Kutafuta Mchumba Kisheria?

SWALI: 

Assalaamu alaikum.

Kwanza natoa shukurani zangu kwa msaada wenu wa kutuelimisha kunako dini yetu. Allah awalipe pepo yake, ameen. Swali langu ni vipi muislamu mwanaume kama amkwishafikia uamuzi wa kwamba yuko tayari kuoa, uwezo akawa anao, lakini hana mchumba kama ilivyozoeleka leo ndani ya jamii zisizokuwa za kiislamu; ni upi utaratibu wa kuanzisha uchumba unaokubaliana na sheria zetu za kiislamu?

 


 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunakushukuru kwa du’aa zako na tunamuomba Allaah Atutakabalie hizi ‘amali zetu na pia Awazidishie nyinyi elimu ya Dini yenu na muweze kupata mwelekeo mwema wa kuweza kuifikia pepo inshaAllaah.

Na shukrani zetu kwa swali lako kuhusu taratibu za uchumba na kuoa. Hakika Uislamu umeweka utaratibu mzuri wa mvulana au msichana kutafuta wa pili wake katika maisha ya kindoa bila ya kupitia mifumo ambayo ni ya kumtweza mwenziwe.

Msichana pia anaweza kutafuta mchumba katika mipaka ya Uislamu bila ya kuwa na tatizo lolote lile. Hata hivyo, mara nyingi ni mvulana ndiye mwenye kutafuta mchumba kulingana na mipaka iliyowekwa na Uislamu. Ama kuhusu njia za Kiislamu za kutafuta mchumba zipo kadhaa na hapa tutaangazia kama mbili ambazo zinatumika sana. Nazo ni kama zifuatazo:

1.     Kumjua msichana kwa njia moja au nyingine. Inawezekana umemjua kwa kuwa mlisoma Madrasah moja, au shule au chuo kimoja na ukamuona kulingana na nadharia yako ni msichana anayejistahi na kuchunga mipaka ya Dini. Hata hivyo, kwa sababu hamjaingiliana sana inabidi uulizie kwa wanaomjua kuhusu undani zaidi wa Dini na maadili yake. Wale ambao wanaweza kukusaidia ni madada zako au jamaa wako wa kike ambao wanaweza kumfuatilia katika mipaka ya Kiislamu na hivyo kufuata taratibu nyingine baada ya hapo.

 

2.     Njia hii ni ile ambayo pindi mvulana anapokuwa tayari kuoa, anakaa chini na kuzungumza na mamake, dada zake, shangazi au halati zake na kuwaelezea lengo lake la kutaka kuoa. Hapo inabidi uwape sifa za mke unayemtaka na baada ya hapo watakutafutia mwenye sifa hizo kwani wao ndio wanaingiliana sana na wenziwao kuliko wewe au jamaa zako wa kiume. Mbali na kuwa jamaa zako wa kiume huenda wakawajua wale wasichana wengine walio na ujamaa na wao wa karibu hivyo kuweza kukusaidia katika hilo.

Baada ya kuridhika na yale uliyoambiwa na katika uchaguzi huo, utaratibu unaofuata ni kuswali Swalah ya Istikhaarah na kisha kinachofuatia ni kupeleka posa kwa wazazi wa msichana na kuonana ana kwa ana na unayemposa. Kuonana huko si faragha bali uonane naye mbele ya maharimu yake. Ikiwa umeridhika na Dini na maadili yake na ukaridhishwa na umbile lakemtaendelea na posa hiyo na kupanga siku ya harusi. Ikiwa hukuridhika basi utatafuta mwengine.

Huku kuonana na huyo unayetaka kumuoa ni kwa mujibu wa nasiha aliyopatiwa Mughiyrah bin Shu'bah (Radhiya Allaah 'anhu) na Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam), kwani kufanya hivyo kunajenga mapenzi. Wapo wanawake wengine ambao katika macho yao wana kitu kama walivyokuwa wanawake wa Kianswaar wa Madiynah. Na kimaumbile unaweza ukawa hupendezewi na hilo, hivyo utajitoa mapema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share