Sikumpa Mahari Mke Wa Kwanza, Kisha Nikaoa Wa Pili Na Kumpa Mahari Je, Ni Haki Kufanya Hivyo?

Sikumpa Mahari Mke Wa Kwanza, Kisha Nikaoa Wa Pili Na Kumpa Mahari

Je, Ni Haki Kufanya Hivyo?

 

 www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalam aleykum warahamatullahi wabarakatu. suali langu linahusu kutolipa mahari kwa mke wa kwanza. nimeowa mke bado sijamlipa mahari yake nimeowa mke wapili nimemlipa mahari yake kabla sijamlipa yule wa kwanza je ni haki?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Hakika ni makosa na kutofanya uadilifu ikiwa hilo limetokea kweli. Uadilifu na haki inatakiwa iwe ni yenye kufanywa na Muislamu katika hali zote kwa ajili hiyo, Allaah ('Azza wa Jalla)    Anatueleza:

 

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا  

Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe.  [An-Nisaa: 58]

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 135]

 

Hata hivyo, hukutueleza kuhusu makubaliano yenu na mke wa kwanza. Je, mke mwenyewe alitaka alipwe baadaye? Ikiwa alikuwa anataka hivyo, je muda wa kulipwa umefika? Ikiwa umefika je, umempatia haki yake au bado? Ikiwa muda umefika na hujampatia basi utakuwa umedhulumu na katika hali hiyo unatakiwa umuombe msamaha mkeo huyo wa kwanza na umlipe haki yake kwa haraka iwezekanavyo. Hakika ni kuwa ikiwa hukumlipa kwa wakati uliofaa utakuwa hukutenda haki.

 

 

Na pia haikukufalia wewe kwenda kukimbilia kuoa mke mwengine na hali hujatimiza na hukuweza kutimiza majukumu kwa mke wa mwanzo, na moja ya majukumu ni kwanza kabisa kumlipa mahari yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   katupa ruhusa ya kuoa mke zaidi ya mmoja lakini si kujiolea tu na hali hatuwezi kuwa waadilifu na kusimamia majukumu yetu kwao ipasavyo.

 

Kwa hiyo, fanya uadilifu baina ya wake zako kwani kutofanya uadilifu kutakufanya uwe ni mwenye kuhasirika Siku ya Qiyaamah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share