Hadiyth Ya Kumkosoa Kiongozi

SWALI

 

Je, ipo hadithi inayosema ukitaka kumkosoa kiongozi muone faragha usimkosoe mbele ya ummah?


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumkosoa Kiongozi.

 

 

Kwanza tutazame Hadiyth inayuhusu nasaha kwa ujumla.

Kutoka kwa Tamiym bin Aws Ad-Daariy (Radhiya Allaahu ‘anhu):  Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dini ni nasiha/nasaha.  Tukauliza: Kwa nani? Akasema kwa Allaah, Kitabu Chake, na Mtume Wake, na kwa Viongozi wa Waislamu, na watu wa kawaida. [Muslim]
Na Hadiyth nyingine kuhusu nasaha kwa viongozi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
“Hakika Allaah Anaridhia kwenu mambo matatu na Anachukizwa nanyi kwa mambo matatu. Anaridhia kwenu kumuabudu Yeye na Kutomshirikisha Yeye na chochote, na kushikamana kwenu na kamba (Dini) ya Allaah bila kufarakana, na kuwanasihi kwenu viongozi wenu wale ambao Allaah Amewapa madaraka juu yenu (viongozi wenu)…” [Ahmad, Maalik na Ibn Hibbaan].

 

Hakika ni kuwa suala hili linaingia katika mas-ala ya muamala baina ya kiongozi na raia. Wanazuoni wamegawanya mas-ala ya kumkosoa yeyote sio kiongozi tu katika vipengele viwili:

 

1.     Nasaha, na

2.     Fedheha.

 

Katika mas-ala ya nasaha inatakiwa ifanywe katika njia nzuri sana na faragha ili kutompatia nguvu Shetani. Pia ni katika maumbile ya mwanadamu kutotaka kukosolewa mbele ya watu. Na kutokufanya hivyo ndio njia nzuri kabisa ya nasaha kwani nasaha itapokelewa na pia italeta athari. Katika suala hilo tunaona jinsi gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akitoa nasaha zake. Al-Bukhaariy na Muslim wanatuelezea jinsi alivyowakosoa wale Maswahaba wa tatu waliotaka kufanya bid'ah mmoja akasema hataoa, mwingine ataswali usiku mzima na mwingine atafunga kila siku. Walikosolewa na kupatiwa njia bora ya kufuata Sunnah. Tunapata mara nyingi pia jinsi gani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akikosoa makosa bila ya kutaja majina ila inapokuwa makosa yamefanywa na wasiokuwa Waislamu.

 

Viongozi walikuwa wakikosolewa tu mbele ya watu inapokuwa yeye mwenyewe ameomba watu watoe maoni yao. Kisa maarufu ni kile cha 'Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) alipowauliza raia wake kwa kuwaambia, mkikosa mimi huwahukumu je, mimi nikikosa nani atanihukumu. Akatoka mtu mmoja ambaye alimwambia tutakunyoosha kwa panga zetu.

 

Hivyo, katika kutoa nasaha inaweza kutegemea na mazingira yenyewe lakini mara nyingi inatakiwa itolewe kwa njia ya faragha.

 

Na nasaha kwa viongozi wa Kiislam kunaingia: kuwasaidia wao wanapofuata yale ya haki, kuwatii wao katika yale ya sawa, kuwakumbusha wanapokosea au wanaposahau, kuwa na subira juu yao pale wanapofanya mambo ambayo hayapendezi au hayakubaliki, kushirikiana nao katika Jihaad na kutowaasi au kuwafanyia njama katika uongozi wao. Halikadhalika mtu anapaswa awaombee du’aa wawe katika uongofu na ucha Mungu, kwani uongofu wao na ucha Mungu utawanufaisha Waislam wote kwa ujumla.

 

Ama ushahidi uliotaka wa kumpa Kiongozi nasaha kwa siri ni huu:

 

Amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Anayetaka kumpa nasaha Kiongozi kuhusu jambo lolote, basi asimpe nasaha hiyo hadharani, bali amvute mkono pembeni faragha (azungumze naye), na akipokea nasaha hiyo kutoka kwake atakuwa amepata (ni kheri), na akikataa ushauri (nasaha), basi mtu huyo (mwenye kutoa nasaha) atakuwa ashatekeleza wajibu wake.” [Ahmad na Al-Haakim, na Imaam Al-Albaaniy kasema isnaad yake ni Swahiyh].

 

Na kuna mifano kadhaa ya wema waliopita kuhusiana na utoaji wa nasaha kwa siri, mmojawapo ni ule ulioelezwa na Ibn Rajab kuwa Sa’iyd bin Jubayr alimuuliza Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma), “Je, ninaweza kumuamrisha Kiongozi wangu kufanya ya sawa.” Akamjibu, “Ukiwa una khofu ukimwambia hayo atakuua, basi nyamaza na usiseme chochote kibaya kuhusu Kiongozi huyo. Na ikiwa unashikilia lazima umnasihi, basi ifanye nasaha hiyo baina yako na yeye pekee.” [Ibn Rajab, Kitabu ‘Jaami’I, mj. 1, uk. 225]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share