Hadiyth Dhaifu: Tafuta Elimu Hata Kama Ni China

SWALI:

 

HADITHI YA BW. MTUME (S.A.W) INAYOSEMA, "TAFUTA ELIMU HATA KAMA NI CHINA", SI SAHIHI? AU NI DHAIFU. WABILLAHI TAWFIQ. 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Kuhusu ibara, "Tafuta elimu hata kama ni China", imezoeleka kuwa ni Hadiyth tena iliyo mashuhuri, lakini hakika ni kuwa hiyo si Hadithi bali ni maneno ya wanazuoni wa Kiislamu. Ibara hiyo ilikuwa ni kuwashajiisha Waislamu waende China wakajifunze sanaa na utengezaji wa vyombo ili waje wasaidie dola ya Kiislamu wakati huo. Kuna Hadiyth nyingi zilizo sahihi za kuhusu umuhimu wa kutafuta elimu zinazotakiwa kutumiwa kuliko kutumia maneno ambayo yanahusishwa na Hadiyth na hali ni maneno ya kutungwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share