Zingatio: Mie Simo

 

Naaswir Haamid

 

 

Shukurani zote ni za kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyetujaalia kuwa miongoni mwa wanaoitamka kalimah. Hatuna budi kuelekeza nia, kauli na vitendo vyetu vyote kwa ajili Yake Muumba Pekee. Yote mazuri tuyatendayo yanatokana na Allaah na mabaya yote yanatokana na kasoro zetu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ndiye Ajuaye yaliyomo ndani ya nafsi zetu na wala sisi hatujui yaliyomo ndani ya nafsi Yake. Tunakuomba Mola wetu Utujaalie kheri kwa wanayotudhania, usituchukulie makosa kwa yanayosemwa juu yetu na utusamehe kwa madhambi ambayo hawayafahamu.

 

Amma ba'ad:

 

Kuna mchezo maarufu miongoni mwa watoto ambao huchezwa sana sehemu za mwambao wa Afrika Mashariki. Ni ule mchezo wa kuonesha vidole vitano vya mkono. Kidole cha mwanzo kikatoa rai ya kusema 'twende', cha pili kikauliza 'wapi?', cha tatu kikasema 'tukaibe', cha nne kikawa na wasiwasi na kikauliza 'tukija kukamatwa jee?', kidole cha tano kikakubaliana kubeba mawazo ya wote lakini kikamalizia 'mie simo!'. Huyu wa tano ndiye Ibilisi ambaye atakuwa nasi ndani ya maisha yetu yote ya kumuasi Mola lakini ataruka kwa hatua zote Siku ya Hesabu:

 

{{Na Shaytwaan atasema itakapokatwa hukumu (Qiyamaah): "Allaah Alikuahidini ahadi ya kweli (na leo Ameitimiza), nami nilikuahidini; lakini sikukutimizieni. Wala sikuwa na mamlaka juu yenu (ya kukulazimisheni kunifuata); isipokuwa nilikuiteni tu, nanyi mkaniitika. Basi msinilaumu, bali jilaumuni wenyewe siwezi kukusaidieni wala nyinyi hamuwezi kunisaidia. Hakika mimi nilikataa kunishirikisha kwenu toka zamani." Kwa yakini madhalimu watakuwa na adhabu iumizayo.}} [Ibraahiym: 22]

 

Ibilisi amechukua ahadi mbele ya Muumba kwa kusema kwamba atawapotosha wanaadamu ili wasiione nuru ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), waache kutekeleza maamrisho ya Mtume Wake pamoja na kutofuata njia sahihi ya diyn ya Kiislamu.

 

Atawakalia mbele yao waione dunia tamu wasahau mauti, atakuwa nyuma yao kuwapulizia upepo wa kila anasa wasitake kusikia shida za masikini. Bado Ibilisi huyu hatatosheka, bali atawakalia wanaadamu kuliani mwao na kuwafanya vibaraka vya ujinga hadi kufikia kumshirikisha Mola, atamalizia kwa kuifunga milango ya kushotoni mwao wasiamini ghayb na hivyo kuwakosesha iymaan ya Uislamu.

 

Rafiki mwema ni yule ambaye atakufaa duniani na akhera. Huyu si mwengine bali ni ndugu yako wa Kiislamu asiyependa ukhasirike:

 

{{Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira (kustahamiliana).}} [Al-'Asr: 3]

 

Munakutana kwenye madarasa mukishindana kuisaka elimu ya Kiislamu pamoja na kusaidiana kutekeleza yaliyoamrishwa na Muumba. Tofauti kabisa na Ibilisi pamoja na jeshi lake, ambao wana usuhuba wa kunyunyizia marashi juu ya kichwa tu kama kwenye harusi. Hata ukifika kwako harufu haipo nawe.

 

Tujitahidi kufuata Qur-aan na Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani hizo ndio kinga kuu za kumzuia Ibilisi kutuhadaa.

 

Share