Ufafanuzi Wa Ahlul Bayt (Masharifu) Na Kizazi Chake

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum warahmatullahi wabarakatu, naomba ufafanuzi kuhusu nyumba ya mtume wetu na kizazi chake cha ahlul bait kama vile kikwetu wanvyo itwa masharifu. Kulingana na ninavyo elewa masharifu wametokana na kizazi cha mtume pale mwenyezi mungu alipo sema katika kisa cha ahlul kisaa kuwa amewatahirisha mtume swaw, fatma bint muhamad, ali ibn abitalib, hassan and hussein. Shukran

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Ahlul Bayt.

Suala hili la Ahlul Bayt (Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na tafsiri yake ni mojawapo ya hitilafu kubwa baina ya Ahlus Sunnah na Shia.

 

Wakati Shia wanasema kuwa Ahlul Bayt ni ‘Aliy bin Abi Twaalib na Faatwimah bint Muhammad na wanawe (Radhiya Allaahu ‘anhum) peke yao, Ahlus Sunnah wanaitakidi kuwa Ahlul Bayt ni wote hao waliotangulia kutajwa pamoja na wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na binti zake waliobakia wasiotambuliwa na Shia, na pia wajukuu zake na baadhi ya waliohusiana naye katika ukoo wake.

 

Imeandikwa katika kamusi maarufu "Lisaanul ‘Arab" kuwa; mke na jamaa za mtu ni Ahli Bayti yake. Na katika Qur-aan tukufu, Mwenyezi Mungu Anawataja wake wa mtu kuwa ni Ahli yake.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Allaah? Rehema ya Allaah na baraka Zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba (Ahlal Bayti) hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa” (Huud 11:73). Maulamaa wote wanasema kuwa neno (Watu wa nyumba), katika Aayah hii anakusudiwa Sarah mke wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).

 

Na Akasema:

Alipouona moto, akawaambia watu wake (Li Ahlihi): Ngojeni! Mimi nimeuona moto” (Twahaa 20:10). Inajulikana hapa pia kuwa neno (Ahli yake) anakusudiwa mke wa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) aliyekuwa amefuatana naye katika safari hiyo.

 

Na Allaah Aliyetukuka Akasema pia:

Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo (Ahlika) isipokuwa kufungwa au kupewa adhabu kali” (Yuusuf 12:25). Neno (Ahlika katika Aayah hii) na maana yake ni 'mkeo' aliyekusudiwa ni mke wa al-‘Aziyz.

 

Kwa hivyo dalili zote zinaonyesha kuwa neno Ahlul Bayt au Ahl linatumika

zaidi kwa maana ya mke. Na katika Surat Al-Ahzaab kuanzia Aayah ya 28 hadi ya 33 Allaah Aliyetukuka Anasema:

Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri. Na ikiwa mnamtaka Allaah na Mtume Wake na nyumba ya Akhera, basi Allaah Amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa’. Enyi wake wa Nabii! Atakayefanya uchafu dhahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Allaah ni mepesi. Na miongoni mwenu atakeyemtii Allaah na Mtume Wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na Tutamwandalia riziki ya ukarimu. Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Allaah na Mtume Wake. Hakika Allaah Anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara”. (Al-Ahzaab 33: 28-33).

 

Ahlus Sunnah wanasema kuwa; kama vile katika Aayah zote zilizotangulia, kila anapotajwa Ahli ya mtu hukusudiwa mke, na katika Aayah hizi pia Allaah Anapotaja Ahli Anawakusudia wake zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ukizisoma kwa utulivu Aayah hizi utaona kuwa kuanzia Aayah ya 28 Allaah Anazungumza na wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Allaah Aliyetukuka Anasema:

Ewe Nabii! Waambie wake zako….”.

Akaendelea: “Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine.”

Akaendelea kuwahutubia: “Kaeni majumbani mwenu” “Toeni Zakaah”. “Mtiini Allaah”.

Mpaka Aliposema: “Hakika Allaah Anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara”.

Yote haya wanaambiwa wake zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuanzia Aayah ya 28 hadi 33. Hivi ndivyo ulivyo mfumo wote wa Aayah hizi zilizokamatana na haziwezi kutenganishwa isipokuwa kama mtu anataka kuvuka mipaka na kwenda kinyume na nassw (maandiko).

 

Mtu anaweza kuuliza: “Kwa nini basi Allaah Ametumia ‘swiyghah’ (mfumo wa maneno) ya wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Aliposema: ‘Ankum’. Ikiwa Amewakusudia wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nini asitumie swiyghah ya wanawake peke yao Akasema: ‘Ankunna’.

 

Kwa nini Asitumie swiyghah ya wanawake kama Alivyotumia katika Aayah nyingine zilizomo ndani ya mfumo huu?

 

Majibu ni kuwa; Aayah za mwanzo Allaah Alipozungumza juu ya hukmu za kishari’ah na makatazo na maamrisho yanayowahusu wake za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitumia Nuun ya wanawake lakini Alipozungumza juu ya wema anaotaka kuuingiza ndani ya nyumba ile pamoja na kuwasafisha watu wa nyumba ile barabara, Alimuingiza pia na mwenye nyumba ambaye ni mwanamume naye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kheri hiyo iwaenee wote. Na kawaida katika Lugha ya Kiarabu wanapotajwa wanawake na wanaume kwa pamoja hutumiwa wingi wa wanaume ‘Ankum’.

 

Nani wanaostahiki zaidi kusafishwa na kutakaswa kuliko wake zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu wa nyumba yake, mama za Waislamu, na wanaostahiki pia ni jamaa zake, watu wa aila yake. Kwa sababu Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anastahiki kuwa pamoja na kila kheri na kila jema na kila kilicho bora, na anastahiki zaidi kuwa pamoja na watu wema, naye haridhiki isipokuwa awe pamoja na watu wema, kwani wema lazima siku zote uwe katika mtiririko mmoja.

 

Ikiwa tumemkubali mke wa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) katika Aayah tuliyotangulia kuitaja kuwa ni Ahli yake na tukamkubali mke wa Al-‘Aziyz kama ilivyokuja katika Aayah kuwa ni Ahli yake na tukamuingiza Sarah mke wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kuwa ni Ahli yake, juu ya kuwa katika Aayah ile Allaah Alitumia mfumo ule ule wa wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Alitumia neno (‘Alaykum). Kama Alivyotumia (‘Ankum) katika Suratul Ahzaab. Ikiwa tumewakubali wake wa Mitume wote hao kuwa ni watu wa nyumba, tunalazimika pia kuwakubali wake wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni watu wa nyumba yake.

 

Kutokana na haya inafahamika zaidi tafsiri ya ile Hadiyth maarufu inayoitwa Hadiyth al-Kisaa na maana yake ni Hadiyth ya nguo au Hadiyth ya shuka, wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaingiza ndani ya shuka ile ‘Aliy na Bibi Faatwimah na Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum), kwa ajili ya kuwaingiza na wao katika zile baraka zilizoteremshwa ndani ya Aayah ile ya Suratul Ahzaab. Hadiyth inasimulia kuwa baada ya kuwaingiza wote hao ndani ya shuka, akasema:

Mola wangu hawa ni watu wa nyumba yangu, waondolee uchafu na uwasafishe baarabara”. Na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingiza kichwa chake ndani ya shuka hiyo akasema: “Ewe Mtume wa Allaah na mimi ni katika watu wa nyumba yako”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri”.

 

Na maana yake ni kuwa Ummu Salamah na wake wenzake wote wamekwishatajwa na Allaah katika Aayah hiyo na kwamba wao wamo katika kheri hiyo ya kusafishwa na kutakaswa. Ndiyo maana akaambiwa: Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri”.

 

Dalili nyingine inayothibitisha kuwa wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake imo katika Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy na wengine kama ilivyopokelewa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa na Maswahaba:

Vipi tukuswalie?” Akasema: “Semeni: Mola wangu mswalie Muhammad na wake zake na vizazi vyake, kama ulivyomswalia Ibraahiym, na umbariki Muhammad na wake zake na vizazi vyake kama ulivyowabariki watu wa nyumba ya Ibraahiym hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa uliye Mtukufu”.

Ikajulisha kuwa mke wa mtu na vizazi vyake ni watu wa nyumba yake.

 

Ikiwa mtu hajatoshelezwa na dalili zote tulizozinukuu kutoka katika Kitabu cha Allaah na mafundisho ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi ipo dalili nyingine katika Swahiyh Al-Bukhaariy itakayoondoa shaka yoyote iliyobaki kwa mwenye kuutafuta ukweli bila ya chuki moyoni mwake.

Inajulikana kuwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisingiziwa uongo katika kisa mashuhuri kinachojulikana kwa jina la Haadithatul Ifk, uongo ambao Allaah Aliyetukuka Aliteremsha Aayah katika Qur-aan tukufu kuukanusha, na wakati huo huo Aayah hizo ziliwaonya Waislamu kutorudia tena kueneza uvumi huo, na zikawatahadharisha juu ya adhabu kali itakayomfikia mwenye kurudia tena.

 

Wakati ule Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya mimbari yake kuhutubia, akasema:

Enyi Waislamu! Nani atakayenipumzisha na mtu aliyeniudhi katika Ahli yangu (watu wa nyumba yangu), kwani WaLlaahi sijaona kwa Ahli yangu isipokuwa kheri tupu, na hakuwa akiingia kwa Ahli yangu isipokuwa akiwa pamoja nami” Al-Bukhaariy.

 

Atakayechunguza, ataona kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelitaja neno Ahliy (watu wa nyumba yangu) katika Khutbah hiyo fupi mara tatu, zote zikimaanisha mkewe mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), ikituthibitishia kuwa neno Ahliy lina maana ya mke.

 

Ahlus Sunnah wanawapenda na wanawapa heshima kubwa na wanawatambua watu wote wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wale wanaokubaliwa na Shia na pia wasiokubaliwa na Shia kuwa ni katika Ahlul Bayt kama vile ‘ami zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watoto wa ami zake pamoja na watoto wao (Radhiya Allaahu ‘anhum), hawa ambao Shia hawawatambui kuwa ni watu wa nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama walivyotajwa katika Hadiyth iliyotangulia, nao ni kama ifuatavyo:

 

1. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

2. Wake zake

3. Binti zake wote

4. Watu wa nyumba ya Al-‘Abbaas bin Abdilmuttalib

5. Watu wa nyumba ya ‘Aqiyl bin Abi Twaalib

6. Watu wa nyumba ya ‘Aliy bin Abi Twaalib

7. Watu wa nyumba ya Ja‘afar bin Abi Twaalib

 

Hawa wote wametajwa katika Hadiyth iliyotolewa na Muslim wakati Zayd bin Al-Arqam (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa:

Wake zake si katika watu wa nyumba yake? Akasema: “Wake zake ni watu wa nyumba yake. Lakini watu wa nyumba yake (waliokusudiwa hapa) ni wale walioharimishwa kupokea sadaka. Akaulizwa: “Nani hao”. Akasema: “Hao ni watu wa nyumba ya ‘Aliy na watu wa nyumba ya ‘Aqiyl na watu wa nyumba ya Ja‘afar na watu wa nyumba ya ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhum).”

 

Kwa hiyvo watu wa nyumba hizo, juu ya kuwa wengine hawakuwemo ndani ya ile shuka (kisaa) lakini wametajwa kuwa ni watu wa nyumba yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Wake zake bila shaka wanaingia katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kutajwa katika Suratul Ahzaab kama ilivyotangulia, na ndiyo maana katika kuikamilisha Aayah hiyo Allaah Akasema:

Na watajieni (watu) yasomwayo majumbani mwenu katika Aayah za Allaah na hikima (ya Mtume), kwa hakika Allaah ni Mjuzi wa mambo ya siri na Mjuzi wa mambo ya dhahiri..” Al-Ahzaab 33: 34).

 

Na watoto na wajukuu wa Al-Hasan bin ‘Aliy na Al-Husayn bin ‘Aliy na ‘Abdullaah bin ‘Abbaas na Muhammad bin Al-Hanafiyah (mtoto wa ‘Aliy kwa mke mwengine), na Al-‘Abbaas bin ‘Aliy na wajukuu zao na wajukuu wa wajukuu zao, wote hao pia ni katika watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hii ni kwa wale waliokuwa Waislamu.

 

Abu Lahab juu ya kuwa ni ‘ami yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini yeye hayumo katika Ahli yake kwa sababu hakuwa Muislamu. Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) allipomuona mwanawe amekimbilia jabalini na maji yanaanza kumfikia alimuomba Allaah Aliyetukuka Amuokoe. Allaah Alimkatalia na kumuambia kuwa huyo si mwanawe, wala si katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kuukanusha ujumbe aliokuja nao Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam).

 

Shia hawakubali kuwaingiza wengine kuwa ni watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa wale tu wanne waliotajwa katika Hadiyth ya shuka, pamoja na maimamu kumi na mbili wa Shia Ithna ‘Ashariyah kwa sababu wanaamini kuwa hao ndio viongozi wa Waislamu waliotakaswa wasiotenda makosa watakaowaongoza Waislamu baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifutavyo upate maelezo zaidi:

 

Usharifu Nini Maana Yake? Je Ukoo Wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Uko Kweli?

 

Kizazi Cha Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Bado Kinaendelea?

 

Masharifu Wasioswali Wana Maovu Na Maasi Watukuzwe? Je, Wao Bora Kuliko Mja Anayefuata Sheria?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share