Hirizi Inafaa Kuvaliwa Kutibu Maradhi Ya Nafsi Na Jini?

SWALI:

Asallam allaikum natumai hamjambo, Swa langu ni mimi nilipwa na matatizo ya kuumwa na maradhi yasiyojulikana hospitali vipimo nilivimaliza,visomo nilisomewa sana na mimi mwenyewe kusoma lakini nilikuwa ni mtu wa kutulia tu na kulia lakini kwa baadae vilitulia na kurudi school kurudia darasa basi rehma zake ALLAAH [S.A.W] Mpaka nikamaliza kwa sasa nimeolewa huwa vinanitokea ninavyojisikia ni kukosa raha ya maisha[nafsi] na kupata kilio kikubwa sijui kinapotokea basi nikapelekwa kwa Maalim mmoja akanisomea na KUNIPA HAZINA NIWE NAKAA NAYO JE?INAFAA AU NI MAKOSA?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako hilo kuhusu matatizo yako na ugonjwa wako huo ambao kama unavyosema haukujulikana kabisa hata hospitali. Ifahamike kuwa si magonjwa yote yanafahamika hospitali na magonjwa kama baridi kumpeleka mtu hospitali ni kumharibu kabisa.

Baadhi ya maradhi yanatibika kwa urahisi zaidi kwa kutumia matibabu ya kienyeji japokuwa kwetu Waislamu ni fani ambayo imekuwa kuanzia enzi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka wakati wetu huu hasa katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki na hata katika Bara Arabu.

Kukosa raha ya maisha huja kwa sababu nyingi mojawapo ikiwa pengine kutosikilizana na mume wako na kadhalika. Pia kutumia dawa au vitu ambavyo ni kinyume na sharia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na mojawapo ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hutupatia mitihani ambayo kama Waislamu tunatakiwa tupambane nayo kwa Imani na yakini sio kwenda kinyume na Aliyoamrisha. Kuhusu mitihani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza:

Na Tutakutieni katika misukosuko (mitihani) kwa baadhi ya mambo; hofu na njaa na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wapashe habari njema wanaosubiri” (2: 155).

Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akatupatia dawa njema kwa haya yanayotukumba pale Alipotuambia: “Enyi Mlioamini! Jisaidieni katika mambo yenu kwa subira na Swalah; bila shaka Allaah yu pamoja na wanaosubiri” (2: 153).

Subira inaleta tija iliyo kubwa nasi inafaa tuwe na sifa hiyo na tuwashinde wasiokuwa Waislamu katika hilo.

Tufahamu kuwa kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ni dhulma iliyo kubwa, amali zote huharibika na ni dhambi ambalo halisamehewi na Allaah. Hayo ni kwa mujibu wa kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Hakika Allaah Hasamehi dhambi ya kushirikishwa na kitu lakini Yeye husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Allaah, basi bila shaka yeye amekwisha potea upotofu ulio mbali na haki” (4: 116).

Pia: “Na wakumbushe, Luqmaan alipomwambia mwanawe; na hali ya kuwa anampa nasaha. Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah, maana shirki ni dhulma kubwa sana” (31: 13).

Miongoni mwa njia za shirki ni kupatiwa hazina na Maalim, Shekhe na wengineo ambao huwadanganya watu kwa kuwasomea kisomo cha uwongo kisha kuwapa hirizi wavae. Waalimu wa kweli wanasoma kile kisomo kilichosuniwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kuondosha kwa mtu ikiwa amekumbwa na jini au amefanyiwa uchawi. Mas-ala ya kutumia hazina au hirizi yamekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo kuwa haramu katika Dini yetu tukufu ya Uislamu.

Kuhusu hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza: “Mwenye kutungika hirizi hakika amefanya shirki” (Ahmad na al-Haakim, naye akaisahihisha).

Na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Aliyetundika hirizi na mwenye kutungika azima basi Allaah Hamtimizii shida yake, na mwenye kutungika azima Allaah Hamuondolei alicho nacho” (Ahmad na al-Haakim, naye akasema Isnadi yake ni sahihi).

Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona kipofu mmoja ana kitambaa kakifunga mkononi mwake cha njano: “Kwa nini umefanya hivi?” Akasema: “Hii ni kutokana na ‘waahina’ tatizo lililonikuta”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ivue kwani Allaah Hatakuzidisha ila matatizo tu na kama utakufa na hiyo iko juu yako basi hautafanikiwa milele” (Ahmad).

Kile ambacho kinajuzu kwako kufanya ni kujitibu kwa Ruqya (kisomo cha kisheria) ambamo hamna shirki ndani yake. Inatakiwa mwenye kukusomea awe atasoma zile Aayah na Surah ambazo ni tiba kwako au wewe mwenyewe mbali na kusoma surah na Aayah tofauti za Qur-aan lakini uwe ni mwenye kusoma zile Aayah ambazo zitakusaidia. Ndio katika hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: “Hakuna ubaya na Ruqya kama hakuna shirki” (Muslim).

Ikiwa kutakuwa na kisomo na shirki ndani yake kama ulivyofanyiwa itakuwa haifai. Ukitazama katika hirizi ambayo utakuwa umepatiwa hakuna kitu ndani isipokuwa karatasi isiyo na maandishi au karatasi iliyochorwa tu vitu au pengine kipande cha gazeti kama tulivyopata pindi tulipomtoa mtoto mmoja hirizi na kuifungua ndani yake.

Aayah ambazo zinaweza kukusaidia ni kusoma asubuhi na jioni Suratul Baqarah (2), Aayah 1-5, 255-257 na 284-286, Suratul Kaafiruun (109), Suratul Ikhlaasw (112) mara tatu, Suratul Falaq (113) mara tatu a Suratun Naas (114) mara tatu na zote ni kinga pamoja na du’aa nyingi ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha na zinapatikana kwenye kitabu cha Hiswnul Muslim ambacho kiko katika ALHIDAAYA.

Tunamuomba Allaah Akuponyeshe wewe pamoja na Waislamu wengine wenye maradhi tofauti.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share