Kuvaa Shanga Kwa Ajili Ya Itikadi Ya Kuzuia Mimba Ni Shirki?

 

Kuvaa Shanga Kwa Ajili Ya Itikadi Ya Kuzuia Mimba Ni Shirki?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum. Ama baady, Mimi niko ndani ya ndoa na Allah ametujaalia na mume wangu tumepata binti mmoja, lakini katika kuzuia mimba ninatumia dawa ambayo nilienda kupewa ni dawa ya kienyeji ni kama kijiti kidogo kinachanganywa na kijiwe halafu natengenezewa kwenye ushanga naivaa!!! Je nauliza kufanya hivyo ni dhambi au ni shirki? Tafadhali naomba mnijibu swali langu na Allah awajaze kheri nyingi Amin

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hujatoa nyudhuru za ki-Shariy’ah za wewe kuzuia mimba. Bila udhuru au sababu za kisiha hairuhusiwi mtu kuzuia mimba kabisa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katupendezeshea sisi kuwa na kizazi kingi na amesema yeye atajifakharisha kwa wingi wa Ummah wake siku ya Qiyaamah. Sasa ikiwa ndugu yetu wewe mtoto mmoja tu unaanza kuzuia mamba, itakuwaje kwa wale wanaopata watoto sita au saba? Na, je, ungekuwa hukujaaliwa mtoto labda leo ungekuwa unalalamika na kwenda kwa waganga wa uongo wenye kukupa vitu vya ajabu ajabu kama hivyo vya kuvaa ili upate mtoto! Huoni ndugu yetu kila jambo utakuwa unafanya mambo ya kishirikina?

 

 

Hakuna dawa kutokana na vitu vya kuvaa kama shanga. Ushanga huo ni kama hirizi ambayo inavaliwa kwa sababu nyingi ambao watu wanapatiwa na wachawi kwa majina ya dawa za kienyeji. Uvaaji wa hirizi ni shirki, kwa mujibu wa Hadiyth za  Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mwenye kutundika hirizi, hakika amefanya shirki” [Ahmad].

 

Na pia:

 

“Aliyetundika hirizi basi Allaah hamtimizii (hamuondolei shida yake)” [Al-Haakim].

 

 

Na pia,

 

Imepokewa kutoka kwa Abu Bashiyr Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba alikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari mojawapo. Akamtuma mjumbe kuamrisha kwamba: ((Kusiachwe kidani cha uzi au kidani chochote katika shingo za ngamia isipokuwa kikatwe)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa hivyo, kutungika na kuvaa ushanga huo ni shirki na ni madhambi. Itabidi uuvue haraka sana na umuombe Allaah maghfirah na msamaha kwa makosa hayo uliyoyafanya. Naye ni Mwingi wa Kusamehe kwa wale waliofanya mambo wasiyoyajua.

 

Na daima tunakushauri, uwe unauliza jambo kwa wenye elimu kabla hujaamua kulifanya, na sio kulifanya kasha unakuja kuuliza hukumu yake baada ya kuwa tayari ushafanya! Na hilo ni tatizo sugu katika jamii yetu, watu huenda kwenye matatizo na madhambi kasha huja kuuliza hukumu baada ya kuwa tayari washavuruga na kufanya maovu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share