Bismillaahi Inahesabika Kuwa Ni Aayah Katika Suratul Faatihah?

SWALI: 

 

Assalamu aleykum warahmatullahi wabarakatu, swali langu ni hili katika sura nyingine zote tunapata kuwa bismillahi rahmani rahim ndio utangulizi au ndio ufunguzi wa sura lakini katika suratul fatiha 'BISMILLAHI RAHMANI RAHIM' imekuwa kama aya ya kwanza ya suratul 'FATIHA' naomba ufafanuzi kutoka kwenu, jee BISMILLAHI RAHMANI RAHIM ile katika suratul 'FATIHA' na zile BISMILLAHI RAHMANI RAHIM nyingine katika zile sura nyingine tafauti yake ni nini? SHUKRAN WA JAZAKALLAH KHER.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Bismillaahi ar-Rahmanir Rahiym katika Suratul Faatihah na Surah nyinginezo. Kuhusu suala hilo kuna tofauti baina ya wanachuoni na kila mmoja ana dalili zake kuhusu hilo:

 

Mwanzo ni kuwa wanazuoni wamekubaliana kuwa al-basmalah (BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym) iliyopo katika Suratun Naml (27) kuwa ni sehemu ya Aayah katika kauli Yake Aliyetukuka: "Imetoka kwa Sulaymaan, nayo ni Bismillaahi ar-Rahmanir Rahiym" (27: 30) na haihesabiwi kuwa ni mwanzo wa Aayah ya Surah hiyo, na kuisoma mwanzo wa Surah hiyo ni Makruuh.

 

Hata hivyo, wanachuoni wametofautiana kama al-basmalah ni Aayah katika Suratul Faatihah na katika mwanzo wa kila Surah au la? Kauli za wanachuoni katika hilo ni kama zifuatazo:

 

1.      Hiyo ni Aayah katika Suratul Faatihah na kila Surah katika kila Surah isipokuwa Bara’ah (Surat Tawbah). Na hiyo Madh-hab ya Imaam Ash-Shaafi'iy, Ath-Thawriy, Ibnul Mubaarak na kundi la wanachuoni.

2.      Si Aayah katika Suratul Faatihah wala Surah nyingine yoyote katika Qur-aan. Na hiyo ni kauli ya Imaam Maalik, Al-Awzaa’iy na moja ya riwaya kutoka kwa Imaam Ahmad (Ingawa kuna mashaka kuhusu usahihi wa hiyo riwaya kutoka kwa Imaam Ahmad kama ilivyotajwa katika Al-Muhadhab).

3.      Hiyo ni Aayah kamili katika Suuratul Faatihah na si katika Surah zingine. Hii ni kauli ya Is-haaq, Abu ‘Ubayd na riwaya moja kutoka kwa Imaam Ahmad.

4.      Si Aayah katika Suratul Faatihah wala mwanzo wa Surah nyinginezo, bali ni Aayah kitenganishi baina ya Surah. Na hiyo ni kauli ya Madh-hab ya Imaam Abu Haniyfah na ndio kauli sahihi katika madh-hab ya Imaam Ahmad.

Rai hii ya nne, ameielezea Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah kuwa ni rai au maelezo yaliyo ya kati kwa kati katika maelezo yote yaliyotangulia.

 

Na inayoonekana ni kuwa kauli ya Abu Haniyfah ina nguvu zaidi.

 

Ama kusoma al-basmalah katika Swalah, wanachuoni pia wametofautiana kwa kauli zifuatazo:

 

1.     Imaam Maalik amekataza kusoma al-basmallah katika Swalah za Faradhi, kwa sauti au kawa siri. Hilo halifai kufanywa katika ufunguzi wa Suratul Faatihah wala Surah nyingine. Na amejuzisha kusomwa katika Swalah za Sunnah.

2.     Imaam Abu Haniyfah naye amejuzisha kuisoma kwa siri pamoja na al-Faatihah katika kila Rak'ah ya Swalah, na ikiwa ataisoma pamoja na kila Surah itakuwa vyema.

3.     Ama Imaam ash-Shaafi'iy, ni wajibu kwa mwenye kuswali kuisoma, ikiwa kwa sauti aisome kwa sauti na ikiwa ni Swalah ya siri basi kwa siri.

4.     Na Imaam Ahmad bin Hanbal naye amesema, anafaa mwenye kuisoma aisome kwa siri na haifai kuijihirisha kabisa.

 

Hakika ni kuwa Surah al-Faatihah ina Aayah saba peke yake na katika hilo wametofautiana wanachuoni kuhusu ni ipi Aayah ya mwanzo. Wengine wamesema bismiLLaah ni Aayah na wengine wameona sio.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share