Kuombewa Du'aa Na Mkristo Ili Apone

SWALI:

assalama alaikum warahmatullah wabarakatu.

bismmillahi rahmani rahiim

suali langu ni kwamba mimi watoto wangu wanaumwa (wanakohoa sana) namuomba Allaah siku zote awape tahfifu, vile vile nishakwenda hospitali sana lakini matabibu wameshindwa kugundua ni tatizo gani na wamenishauri niwaangalie tu mpaka wakikuwa watapona lakini watoto hao wanateseka sana. Hivi karibuni nilikuwa nazungumza na mwenzangu asijekuwa muislam kuhusu tatizo hilo nae amenishauri kuwa aje kuniombea kwa jina la yesu kwani toka miaka yote watu wanaponywa na jina la yesu na si vyenginevyo, na akaniahidi kama akimaliza maombi anaamini kabisa kwamba watoto wangu tatizo hili litaondokaa kabisa na wala halitawarudia tena.

utatanishi unaonikuta je nikubali aje awaombee? na je watoto wakipona si itakuwa Allaah anaijaribu imani yangu na huyo mwenzangu ndio atapata njia nyepesi ya kujifaharisha mbele yetu waislam kuwa jina la yesu limetuponya na kufanya hivo si shirki?

wabillahi taufik. shukran.

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo muhimu kuhusu mas-ala hayo ya kuombewa. Mwanzo inatakiwa tuelewe kuwa maombi yanapitia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kuomba kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni shirki katika Uislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameliita jambo hilo kuwa ni dhulma kubwa sana, “Kwa hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa” (31: 13).

 

Hili pia ni dhambi ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hamsamehe kabisa mwenye kumshirikisha “Hakika Allaah hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Allaah basi hakika amezua dhambi kubwa” (4: 48).

 

Tujue kuwa uzima, siha na ugonjwa yote ni mitihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kututazama tutabaki vipi katika Imani yetu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Ambaye Ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi” (67: 2).

 

Na hata ukiwa na ugonjwa ambao umewashinda madaktari walio mabingwa katika fani hiyo hairuhusiwi kwani inakuingiza katika shirki ambayo ni dhambi kubwa.

 

Kuwa umemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa muda haitoshi, kwani hufai kufa moyo katika hilo wala kuona kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) hajakujibu. Huo ni utovu wa Imani kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani yeye mwenyewe Ametuahidi kuwa: “Na Mola wenu Anasema: Niombeni Nitakuitikieni” (40: 60). Bila shaka! Allaah Atakujibu kwa njia itakayowaondolea watoto wako matatizo na maradhi hayo.

 

Kitu ambacho tunaweza kukunasihi ni kuwa uende kwa Shaykh ambaye anajulikana kwa uchaji Allaah wake, Imani na maadili mema, pamoja na mtoto wako ili apate kumsomea kisomo cha Qur-aan na Du’aa ambazo zimethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Matumaini yetu ni makubwa kuwa maradhi hayo yataondoka lakini usijitie katika maangamivu kwa kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa). Hakika inajulikana kuwa hao makasisi hawaponyeshi chochote bali wanatumia udanganyifu katika hilo.

 

Tunakuombea kila la kheri na pia tuko nawe katika Du’aa ili watoto wetu wawe ni wenye kupata shifaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share