Mkojo Ni Najisi Ikiwa Nguoni Au Ardhini – Kuondoa Kwa Maji Au Mchanga?

 

Mkojo Ni Najisi Ikiwa Nguoni Au Ardhini  Kuondoa Kwa Maji Au Mchanga?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI

 

Natanguliza Shukrani zangu na pia naomba radhi kama nitakuwa nimetumia utaratibu ambao si sahihi. Nimeuliza maswali haya katika njia ya kawaida; ila itakuwa si vibaya nikiulizia kupitia njia hii huenda nikapata majibu mapema zaidi kwani hali hii inanitatiza sana na kila mara, na imekuwa ikinikumba sana katika makazi yangu mapya ambapo kuna mtoto mdogo wa kiume ambaye nampenda sana ila linapokuja suala na kutoharisha sehemu aliyo inajisisha napata utata sana!!

Kama nguo imeingia najisi, labda najisi ya mkojo, kisha nikailoweka na sabuni ili kuifua, kisha nikaitoharisha, yaani maana kwamba kuwa nikaiosha kwa maji yenye kuchuruzika, ila mwishowe kabisa wakati naikamua ikawa bado na mapovu ya sabuni, nikarudia tena takribani mara tatu, ila bado povu lile halikuisha. Sasa swali ni kuwa jee kuwepo kwa povu ni dalili kuwa bado najisi ipo?

 

Kama najisi ya mkojo imedondoka chini/sakafuni kiasi kwamba kuiondoa kwa maji ya kupita haiwezekani, na mimi nikajitahidi kuifuta kwa kitambaa, ila kila baada ya kufuta mara moja nikakiosha kwa maji ya kuchuruzika, takribani mara nane au tisa na nia yangu ni kuwa mara tatu miongoni mwa hizo zitakuwa ni kuitoharisha sehemu hiyo, ila baadae nikagundua kuwa kile kitambaa bado kina harufu ya mkojo. Sasa swali ni kuwa jee hiyo ni dalili kuwa bado najisi ipo? Na je hiyo ni njia sahihi ya kuodoa najisi sehemu ambayo maji ya kuchuruzika inakuwa shida kutumia?

Je naweza kuondoa najisi ya mkojo au kitu kingine chochote cha maji maji, kwenye sehemu kama kwenye swali la pili hapo juu kwa kutumia mchanga safi na mkavu?

 

Wabillah Tawfiq.

 

 

 JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika swali hilo halina utata kabisa kwani tumebainishiwa na Uislamu kuhusu hilo na mengineyo.

 

 

Ikiwa najisi ni mkojo wa mtoto ulioingia katika nguo utaiosha hiyo nguo yako kwa maji na ukiiosha kwa sabuni ni bora zaidi. Pindi harufu inapokuwa haipo tena tayari nguo hii itakuwa imetwaharika. Ikiwa hata mapovu ya sabuni hayajaisha lakini harufu imetoka, basi hakutakuwa na tatizo lolote unaweza kuitumia bila tatizo lolote.

 

Na kama najisi hiyo iko sakafuni cha kufanya ni kuifuta kwa kitambaa baada ya kumwagia maji kwenye mkojo huo ulioko sakafuni au kwa kitambaa ulichokitia maji. Ukishafuta utakiosha kitambaa hicho na pindi harufu yake itakapoondoka kitambaa na sakafu vitakuwa twahara wala usiwe na wasiwasi. Kutwaharisha kitambaa si lazima kuwe na maji ya kuchuruzika.

 

Na najisi ya mkojo haisafishwi kwa kutumia mchanga. Mchanga unatumiwa tu kuondoa najisi kwa kitu ambacho kimerambwa na mbwa, ila tu katika hali ya dharura ya kukosekana maji kabisa.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi

 

 

002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Aina Za Twahara

 

003-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je Manii Ni Twahara Au Najsi?

 

004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Pombe Ni Najsi?

 

005-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je Damu Ni Najsi?

 

006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Matapishi Ya Mwanadamu Ni Najsi?

 

007-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nini Hukmu Ya Majimaji Yanayotoka Kwenye Utupu Wa Mwanamke Au Unyevunyevu Wa Utupu Wake?

 

008-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Najsi Zinazosamehewa

 

009-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Za Najsi Zilizobainishwa na Hadiyth

 

 010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Ni Lazima (Kutumia) Maji Katika Kuondoshea Najsi? Au Inajuzu Kuondoshea Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share