Skip navigation.
Home kabah

Fisadi Gani Mbili Za Mayahudi Zilizotajwa Katika Surat Bani Israaiyl?

SWALI:

Assalam alaykum
Natumai mnaendelea vizuri na afya njema na shughuli zenu za Dawa. Ningependa kuuliza: Katika kitabu kitukufu Qur'an, Allah SWT ameelezea katika Suratul Israa au Bani Israel katika aya ya 4 - 5.
Napenda kujua hizo fisadi mbili zilizoandikwa kuwa Wana wa Israel watazifanya, haswa hiyo ya kwanza ilitokea wakati gani na wakati wa Mtume gani. Na ni watu gani katika waja wake Allah ambao aliwapeleka kuwatia adabu. Kisha napenda kujua hiyo fisadi ya pili ni ipi au lini itatokea. Na kama kuna mengine ya ziada tuchambulini kwa hawa watu ambao Allah SWT amewalaani kwa jeuri yao.
Shukran

 

 

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaama.

Hakika hili ni swali nyeti ambalo inatakiwa kila Muislamu awe na ufahamu nalo. Swala la Mayahudi ambao Qur-aan, Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Biblia na hata historia imetubainishia uovu wao usio kifani. Lakini hapa si mahali pake kuelezea hayo kwani swali mbele yetu ni jengine japokuwa linahusiana. Yapo makala marefu kuhusu hilo ambayo tumeyaandika na InshaAllah munaweza kuyasoma katika tovuti ya al-Hidaaya kwenye kiungo kifuatacho:

ARDHI ILIYOSAHAULIKA

Hakika ufisadi wa Bani Israili umetokea mara nyingi katika historia yao, idadi zake haziwezi kuhesabika. Na makusudio ya ayah ni kuwa mara mbili hizi ufisadi ni dahiri kabisa. Na kuwa ayah inayofuata ni dalili kuwa kusalitishwa juu yao waja wa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) utaendelea mpaka Siku ya Qiyaama kwa sababu ya ukafiri na uasi wao. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema: “Na kama mtarudia mwenendo wenu wa kuharibu, Sisi pia Tutarudia kukuangamizeni” (17: 8).

Kabla hatujazifafanua ayah hizo ni vyema tuandike tafsiri zake ili tuwe katika ufahamu kwa tunayoyaeleza. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na Tukawafunulia Bani Israili katika hicho Kitabu: ‘Bila shaka nyinyi mtafanya uharibifu (ufisadi) katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtatakabari kutakabari kukubwa’. Basi itakapofika ahadi ya kulipwa kwa uharibifu) wa kwanza wa hiyo miharibifu miwili, Tutakuleteeni watu wetu wenye mapigano makali; nao wataingia mijini mwenu kila upande. Na hii itakuwa ni ahadi itakayotimizwa” (17: 4 – 5)

Wametofautiana Mufasirina kuhusu maana ya kufanya ufisadi mara mbili katika ardhi. Nasi InshaAllah tutaangalia baadhi ya tafsiri na kutaja mwishowe rai ambayo ina nguvu zaidi.

Ash-Shawkaaniy katika Fathul Qadiir anasema: “Mara mbili inasemwa kuwa mara ya kwanza ni baada ya kuuliwa Ash‘iyaa’ au kufungwa kwa Nehemia au kuhalifu amri za Taurati. Na mara ya pili ni kuuliwa kwa Yahyaa ibn Zakariyya (‘Alayhimas Salaam) na azma ya kumuua ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam). Na panasemwa kuwa ufisadi wa kwanza umetokea lakini wa pili bado. Nao walitumilizwa watu wetu wenye mapigano makali yaani wenye nguvu katika vita na ukali wanapopambana na adui. Panasemwa kuwa huyu alikuwa ni Nebukadneza na jeshi lake kutoka Babeli”. Hapa upo mgongano wa maelezo kwani mfalme Nebukadneza alikuja takriban miaka 580 kabla ya kuja kwa Yahyaa na ‘Iysaa (‘Alayhimas Salaam).

Anasema Muhammad ‘Aliy asw-Swaabuuniy katika tafsiri yake Swafwatut-Tafaasiyr, mjalada wa 2, uk. 152 yafuatayo: “Amesema ‘Abbaas: Ufisadi wa mara ya kwanza ni kumuua Zakariyya (‘Alayhis Salaam) na mara ya pili ni kumuua Yahyaa (‘Alayhimas Salaam). … Hakika Bani Israili walipohalalisha haramu na kumwaga damu, Allah Aliwasaliti juu yao Nebukadneza, mfalme wa Babeli ambaye aliwaua elfu sabiini, na huo ndio ufisadi wao wa kwanza”. Hapa pia mfasiri amechanganya baina ya matukio kwani Nebukadneza alikuja kwa kitambo kikubwa kabla ya kuja kwa Zakariyya na Yahyaa (‘Alayhimas Salaam).

Na amesema Abul Fidaa’ Ismaa‘iyl ibn Kathiyr katika tafsiri yake Tafsiyrul Qur-aanil ‘Adhwiym, mjalada wa 3, uk. 28 – 29: “Hakika Mufasirina wa zamani na sasa wametofautiana ni kina nani hawa waliosalitishwa juu yao? Ibn ‘Abbaas na Qataadah wanasema kuwa ni Jaaluut na jeshi lake ambao waliwasumbua lakini baadae wakawa ni wenye kupata nguvu na Daawuud (‘Alayhis Salaam) kumuua Jaaluut. Na kwa hiyo Akasema Aliyetukuka: ‘Kisha Tukawarudishieni nguvu zenu juu yao’ (17: 6). Amesema Sa‘iyd ibn Jubayr kuwa huyo alikuwa na mfalme wa Muswul, Senharib na jeshi lake. Na kutoka kwake na wengineo kuwa huyo alikuwa ni mfalme wa Babeli, Nebukadneza”.

Wamesema baadhi ya Mufasirina kuwa maadui waliowatoa katika majumba yao walikuwa ni qaumu ya Jaaluut ambao walikuwa wamewashinda Bani Israili na kuwaua idadi kubwa. Hii ilikuwa ni kabla ya kurudishiwa nguvu zao chini ya uongozi wa Twaalut.

Na kauli ya Allah Aliyetukuka: ‘Kisha Tukawarudishieni nguvu zenu juu yao (hao waliokushindeni)’ (17: 6). Hii ni wazi kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliwanusuru baada ya kujuta na kutubia, nao wakawa ni wenye kulishinda jeshi la Jaaluut na Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) akamuua Jaaluut.

Na kauli Yake: ‘Na Tukakuongezeeni mali na watoto na Tutakufanyeni wenye kundi kubwa kuliko wao’ (17: 6). Hii ilipatikana katika kipindi cha dhahabu chini ya utawala wa Manabii Daawuud na Sulaymaan (‘Alayhimas Salaam) cha miaka 80. Ama baada ya kipindi hiki cha dhahabu dola hiyo iligawanywa sehemu mbili: Dola ya Yahudha na Dola ya Israili. Ufisadi uliingia kati yao, mzozano na mapambano mpaka Dola ya Israili ilipopigwa na kutawaliwa na Assyria mwaka wa 721 Kabla ya kuzaliwa kwa ‘Iysaa (BI) na ufalme wa Yahudha kusambaratishwa katika mwaka 588 BI na mfalme wa Babeli, Nebukadneza. Historia ya bani Israili baada ya hapo haikuwa ila ni silsila ya maasi, adhabu, balaa na maafa ambayo iliwapitia wakiwa na watu tofauti” (Banu Israili Fiyl Qur-aan was Sunnah, Mj. 2, uk. 366).

Na wengine wamesema: “Ufisadi wao wa mara ya pili ulikuwa wakati wa utawala wa Warumi ambapo jemedari jeshi wake, Titus aliwaua wengi na wengine kushikwa mateka na wengine kukimbia. Tukio hili lilitokea baada ya kuuliwa Nabii Yahyaa (‘Alayhis Salaam) kwa miaka kadhaa” (Dkt. Sa‘d al-Murswfiy, al-Khatwarul Yahuud, uk. 23 – 25).

Lakini ipo rai mpya ambayo haijaelezwa ne mwengine katika kufasiri ayah hizi nayo ni ya Shaykh ‘Abdul-Mu‘iz ‘Abdul-Sattaar, ambaye ametofautiana na Ijma‘a ya Mufasirina. Yeye amesema ya kwamba mara zote hizi mbili za ufisadi zilikuwa baada ya kutumilizwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mara ya kwanza wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mara ya pili ni wakati huu wetu wa sasa. Hii ni kuwa Hadiyth ya Isra’a inabashiri mambo yatakayotokea, kwani Suratul Isra’a ni surah iliyoteremka Makkah isipokuwa baadhi ya ayah. Nayo ilikuwa inaeleza kuhusu ufisadi wa Mayahudi waliofanya wakati wa Musa (‘Alayhis Salaam) na baada yake kwa kuwaua Mitume na watu wema na uharibifu mwengineo. Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walifanya uharibifu lakini wakatiwa adhabu na adabu kwa kung’olewa katika mji wa Madinah na hata Bara Arabu (Majallatul Azhar, Mj. 28, uk. 689 yenye anwani Suuratul Isra’a Naqsw Nihaayah Israa’iil). Na sasa pia wamerudia tena ufisadi wao kuanzia mwaka wa 1948 pale walipotunukiwa dola kama zawadi na Uingereza mbali ya kuwa hawakuwa na haki nayo kabisa.

Kwa ufupi tunaweza kusema kuwa ufisadi wa Wana wa Israili ulikuwa mwingi kuanzia wakati wa Muusa (‘Alayhis Salaam) na kila mara walisalitishwa watuengine. Kwa mfano Firauni, Jaalut, Waasuri, Wababeli, Wayunani, Wamakdoni, Warumi, na mwisho kabisa watakuwa ni Waislamu. Waislamu ambao watasimama imara kwa kufuata maagizo ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wakati huo mpaka mawe na miti itazungumza kumuashiria Muislamu pale alipojificha Myahudi. Hapo watauliwa na kushindwa na ardhi tukufu hiyo kurudi mikononi mwa Waislamu.

Na Allah Anajua zaidi