Watoto Wanaofariki Umri Mdogo Nini Hatima Yao?

SWALI:

 

Assalaam Alaykum.

Tumefundishwa na walimu wetu na wazee wetu kuwa watoto wadogo hawana makosa, na wataingia peponi moja kwa moja. Kama ni kweli jee kuna hikma gani ndani yake, ikiwa wakati tunasalia maiti ya watoto, tunaomba dua ya kuwaepusha na moto?? Au kuna umri ambao ikiwa hawakuufikia basi wanaepushwa na moto??


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu watoto wanaofariki wakiwa wadogo na hatima yao.

 

Hapa yapo mas-ala ambayo wanachuoni waliotangulia na wa sasa wametofautiana, Allaah Awarehemu wote. Mas-ala yenyewe ni kuhusu watoto waliokufa wakiwa wachanga, ilhali wazazi wao ni makafiri: Je, hukumu yao ni gani? Na hivyo hivyo, wendawazimu, viziwi, vikongwe na wanaokufa katika Fitwrah, wakiwa hawajafikiwa na ujumbe, hukumu yao itakuwa ipi? Hadiyth nyingi zimepokewa katika mas-ala haya, ambazo tutazitaja hapa kwa usaidizi na tawfiki ya Allaah Aliyetukuka.

 

Hadiyth ya Kwanza kutoka kwa al-Aswad bin Sari'

 

Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa al-Aswad bin Sari' (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Wapo watu aina nne watakaoleta kesi zao Siku ya Qiyaamah: Mtu kiziwi asiyesikia chochote, mwendawazimu, mzee dhaifu na aliyekufa katika Fitwrah. Ama yule kiziwi, atasema: 'Mola wangu Mlezi! Uislamu ulikuja na sikusikia chochote'. Ama yule mwendawazimu, atasema: 'Mola wangu Mlezi! Uislamu ulikuja wakati watoto wananirushia kinyesi cha ngamia'. Ama mzee dhaifu, atasema: 'Mola wangu Mlezi! Uislamu ulikuja nami sikufahamu chochote'. Na ama yule aliyekufa katika Fitwrah, atasema: 'Mola wangu Mlezi! Hakuja Mtume Wako kwangu'. Allaah Atakubali ahadi za kumtii, Atawatumia ujumbe waingie motoni. Naapa kwa Aliyemiliki nafsi ya Muhammad, lau watauingia, utakuwa kwao baridi na salama". Ipo Hadiyth kama hii yenye Isnadi kutoka kwa Qataadah aliyepokea kutoka kwa al-Hasan, naye kutoka kwa Abu Rafi' kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu), lakini mwisho wake amesema: "Yeyote atakayeingia ataukuta ukiwa baridi na salama, na yeyote asiyeuingia ataburuzwa kwayo".

 

Hii pia ilinukuliwa na Ishaaq bin Raahawayh kutoka kwa Mu'aadh bin Hishaam (atw-Twabariy), na al-Bayhaqiy katika kitabu al-I'tiqaad, akasema: "Isnadi yake ni sahihi".

 

Imenukuliwa na Ibn Jariyr kutoka kwa Hadiyth ya Ma'mar kutoka kwa Hammaam kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu), aliyeinasibisha na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha Abu Hurayrah akasema: "Soma ukitaka: 'Wala Sisi hatuadhibu mpaka Tumpeleke Mtume'" [atw-Twabariy].

 

Hii pia ilipokewa na Ma'mar kutoka kwa 'Abdullaah bin Twaawuus kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Abu Hurayrah, lakini ni Mawquuf (haikunasibishwa moja kwa moja kwa Mtume [Swalla Alaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam]) [al-Qurtwubiy].

 

 

Hadiyth ya Pili kutoka kwa Abu Hurayrah

 

Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah (maumbile ya asli [Tawhiyd]), ni wazazi wake ndio wanaomfanya awe Myahudi, Mkristo au Mmajusi kama hayawani wanavyozaa hayawani – je waona yeyote anayezaliwa akiwa ameatilika (akiwa hana kiungo kimoja au kingine)?" Katika riwaya moja, walisema: "Ewe Mtume wa Allaah! Waonaje kuhusu wale wanaozaliwa wakiwa wachanga?" Akasema: "Allaah Anajua zaidi kwa kile ambacho wangekifanya" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ninavyojua – mpokezi hana hakika ikiwa ilinasibishwa kwa Muusa – amesema: "Watoto wa Waislamu wapo Peponi, wakiwa wanatazamwa na kulelewa na Ibraahiym ('Alayhis Salaam)"(Ahmad 2: 326 na al-Majma' 7: 219).

 

Katika Swahiyh Muslim imenukuliwa kutoka kwa 'Iyaaadhw bin Hammaad (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kuwa Amesema: "Hakika Nimewaumba waja Wangu wakiwa Hunafaa (Kuegemea katika maumbile ya kumpwekesha Allaah Aliyetukuka)'" (Muslim). Kulingana na riwaya nyingine, neno lililotumika ni: "Muslimiyna – Waislamu".

 

 

Hadiyth ya Tatu kutoka kwa Samurah

 

Katika kitabu chake al-Mustakhraj 'alal Bukhaariy, al-Haafidh Abu Bakr al-Barqaaniy amenukuu Hadiyth ya 'Awf al-A'rabiy kutoka kwa Abu Rajaa' al-Utwaardi kutoka wa Samurah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah". Watu walimuita: "Ewe Mtume wa Allaah! Watoto wa mushirikina (watakuaje)?" akasema: "Na watoto wa mushirikina pia" (al-Bukhaariy).

 

Amepokea atw-Twabaraniy kutoka kwa Samurah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu watoto wa mushirikina, naye akasema: 'Wao watakuwa watumishi wa watu wa Peponi".

 

 

Hadiyth ya Nne kutoka kwa ‘Ami yake Hasnaa'

 

Amepokea Ahmad kutoka kwa Hasnaa' bint Mu'aawiyah, wa Bani Swuraym aliyesema: Amenihadithia ‘ami yangu kuwa alisema: "Ewe Mtume wa Allaah! Kina nani wapo Peponi?" Akasema: "Manabii tayari wapo Peponi, mashahidi wapo Peponi, watoto wachanga wapo Peponi na wasichana wadogo waliozikwa hai wapo Peponi".

 

 

Ukaraha wa Kuzungumzia Mas-ala haya

 

Yalipokuwa mazungumzo kuhusu mas-ala haya yanahitaji dalili zilizo sahihi, nzuri na huenda wakazungumza wasiokuwa na elimu ya kisheria. Kwa ajili hiyo kikundi cha wanachuoni hawakupendelea kuzungumza kuhusu jambo hilo. Rai hiyo imepokewa kutoka kwa Ibn 'Abbaas, al-Qaasim bin Muhammad bin Abi Bakr asw-Swiddiyq, Muhammad bin al-Hanafiyyah na wengineo (Ahmad).

 

Imepokewa na Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake kutoka kwa Jariyr bin Haazim: Nimemsikia Abu Rajaa' al-'Utwaardi akisema kuwa amemsikia Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) akisema: "Alipokuwa juu ya Mimbar, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 'Jambo la Ummah litaendelea kuwa zuri – au karibu na hilo – maadamu hawatazungumza kuhusu watoto na kudura (Qadar)". Akasema Ibn Hibbaan: "Hii inamaanisha watoto wa mushirikina".

 

Hivyo ndivyo alivyopokea Abu Bakr al-Bazzaar kwa njia ya Jariyr bin Haazim, kisha akasema: "Wamepokea kikundi kutoka kwa Abu Rajaa' kutoka kwa Ibn 'Abbaas, ikiwa ni Mawquuf" (Kashf al-Astaar 3: 35).

 

Hili ni suala ambalo linarudi hukumu yake kwa Muumba wetu, Allaah Aliyetukuka, naye Atamuhukumu kila mmoja na hakuna atakayedhulumiwa hata chembe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share