Mume Amemuambia Asizae Tena, Huku Ameoa Mke Wa Pili Ambaye Anazaa, Naye Ameshika Mimba, Je Aitoe?

SWALI:

 

Assalamu alaykum warahmatu llahi taala wabarakaatu. Mimi nina swali langu ambalo naomba lipewe kipaumbele kujibiwa inshaallah mimi ni mwanamke mwenye watoto 6 na nakaa ugenini uingereza, wakati nimezaa mtoto wa tano mume wangu akanambia nisizae tena, lakini baada ya myaka mitatu nikachukua ujauzito mwengine nikazaa mtoto wa sita. Na miezi miwili iliyopita nimejua kama kaoa afrika na wakati ananambia mie nisizae yeye kule anazaa na mkewe na wana watoto 2, na sasa hivi mie nina mimba ya mwezi mmoja sasa nifanye nini na huyu mwanamme hataki mie nizae nae na ananambie nichukue majira lakini mimi sichukui. Sasa nifanyeje naruhusiwa kuitoa hii mimba ambayo baba haitaki? Naomba mnijibu haraka inshaallah

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwa na mume asiyetaka uzae. Baada ya kusoma uliyoyaandika dada yetu inaonekana kama kwamba mume baada ya kuoa mke mwengine, amekosa mapenzi kwako kwani hayo si mambo wa mume kumfanyia mke aliyezaa watoto sita naye. Ni jambo la ajabu kwa mume kuzaa na mke mdogo lakini kutotaka mke wa kwanza azae naye. Isitoshe, hivyo sio kufanya haki na uadilifu baina ya wake, amekosa kutimiza haki ipasavyo na wala hana haki ya kisheria kumzuia mke asizae kwa sababu zisizokubalika.

 

 

 

Kwa hiyo, ushauri wetu mwanzo ni kuweza kumkabili mumeo bila ya kumtaja mke wa pili. Iwe suala ni baina yako wewe na mumeo. Jambo hilo linatakiwa liwe wazi kwa ajili ya kupata suluhisho kuhusu tatizo hilo ulilo nalo. Inatakiwa uzungumze naye kwa njia ya ulaini, upole, busara na maneno matamu ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Huenda mkakubaliana muwe na muhula wa miaka kadhaa kabla ya kupata mtoto mwengine lakini kufunga kabisa ni jambo ambalo halifai. Inatakiwa kila mmoja awe wazi kwa mwenziwe ili kupatikane ufumbuzi wa suala hilo.

 

 

 

Ama katika kuzaa mwenye kucheza dauru kubwa ni mume kuliko mke; kwani ni mbegu za uzazi za mwanamme ndizo zenye kuingia kwa mwanamke. Na haifai mwanamke kutoa mimba wakati kiumbe kishatiwa roho isipokuwa ikiwa mzazi ameambiwa na daktari mwaminifu kuwa kubeba mimba kutamletea matatizo na pengine hata kumfanya aage dunia. Fahamu kuwa kuua kiumbe ni katika madhambi makubwa katika Uislamu.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) :

 

 

 

((وَلا تَقْتُلُوا أَوْلادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلاقٍ نَحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ((

 

((Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa)) [Al-Israa: 17]

 

                                                                                                                 

 

 

 

Linalotakiwa kwako ni kuibeba mimba hadi kuzaa, nasi tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akupe subira na uvumilivu, Amlainishe mumeo aweze kuona kosa lake na awadumishe katika mapenzi na muweze kuendelea kuzaa na kuwalea watoto kwa hali iliyo nzuri, Aamiyn.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share