Mashairi: Ndoa

           

Ndoa   

‘Abdallah Bin Eifan

         (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salaamu zangu natuma, zifike kila mahali,

Tunaziomba rehema, za Mola zituwasili,  

Hapo siku ya Qiyaama, tuwe chini ya kivuli,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Oa mke Muumini, funga ndoa tawakali,

Mke aloshika dini, na kila siku kuswali,

Hijaab iwe kichwani, afunike yote mwili,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Usitafute uzuri, au yule mwenye mali,

Chagua tabia nzuri, alotulia akili,

Aloleleka vizuri, kidini na kiasili,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Tafuta mke haraka, ukijiona kamili,

Ikufikie baraka, ya Mola Wako Jalali,

Utulie kwa hakika, tabia mbaya badili,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Fadhila zake ni nyingi, uliza kila pahali,

Huo ndio ni msingi, wa maisha ya halali,

Ni kinga kwa mambo mengi, kwa madhambi mbalimbali,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Kuoa ni utulivu, tumeshaona dalili,

Huyaondoa maovu, na mambo huwa sahali,

Hukufanya mtulivu, shida ikikukabili,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Wajibu wako timiza, nyumbani mpo wawili,

Mkikaa kuzungumza, na mambo kuyajadili,

Mjaribu kueleza, muelezane ukweli,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Mume ni msimamizi, kwa mali na kila hali,

Ayaonyeshe mapenzi, maneno kama asali,

Katika masimulizi, asiseme kwa ukali,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Mungu awape watoto, hao ni rasilmali,

Mke ni mama watoto, awe mwema na mkali,

Awatazame watoto, wasikuwe kijahili,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Mke ni nguzo nyumbani, kama vile matofali,

Na mume ndio rubani, huona yaliyo mbali,

Kamba ya Mola shikeni, ibada iwe awali,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

Mola Watunze vigoli, pamoja na wanawali,

Wawe kama wa awali, kama zama za Rasuli,

Nimemaliza kauli, hapa nafunga kufuli,

Funga ndoa tawakali, oa mke Muumini.

 

 

 

 

Share