Kubainisha Wingi Wa Njia Za Kheri (Riyaadhus Swaalihiyn)

 

 

 

 

Kutoka Katika Kitabu ‘Riyaadhus Swaalihiyn

 

Imekusanywa na ‘Abdallaah Mu’aawiyah

 

 

 

 

 

2- KUBAINISHA WINGI WA NJIA ZA KHERI

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

« وما تفعلوا من خير فإن الله به عليم »

« Na kheri yoyote mnayoifanya, basi Allaah Anaijua vyema daima »

 

« وما تفعلوا من خير يعلمه الله »

« Na kheri yoyote mnayoifanya, Allaah Anaijua »

 

Mtunzi (Allaah Amrehemu) anasema:

 

"Mlango wa kubainisha wingi wa njia za kheri"

Kheri ina njia nyingi, na hii ni miongoni mwa Fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa waja Wake ili fadhila kwao ziwe ni za aina mbalimbali, malipo na thawabu kemkem.

Misingi ya njia hizi ni tatu:

- Ima juhudi za kimwili

- Ima utoaji wa mali

- Au mchanganyo wa yote mawili.

Juhudi za kimwili ni vile vitendo vya mwili kama vile Swalah, Swawm, Jihaad na mfano wake.

Ama utoaji mali, ni kama vile Zakaah, Sadaqah, matumizi na mfano wa hayo.

Ama mchanganyo wa yote mawili ni kama kutumia silaha katika jihadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani hilo linakuwa ni  kwa mali na kwa nafsi.

Lakini aina za misingi hii ni nyingi sana ili aina za matendo mema ziwe za aina mbalimbali kwa waja ili wasichoke.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

« فاستبقوا الخيرات »

« Basi shindanieni mambo ya kheri »

« إنهم كانوا يسارعون في الخيرات »

« Hakika wao walikuwa wakiharakia katika mambo ya kheri »

 

Yanayoashiria tuliyoyasema ni kwamba utakuta katika watu, mtu ambaye amezoea kuswali; utamkuta akiswali sana. Mwengine utamkuta amezoea kusoma Qur-aan na anaisoma kwa wingi. Mwengine utamkuta ana utashi wa kusoma na kutafuta elimu ambayo kwa wakati wetu huu, inaweza kuwa ndio ‘amali bora zaidi ya kimwili, kwa vile watu hivi leo wanahitaji elimu ya shari’ah kutokana na kukithiri ujinga na kukithiri watu wanaojiona kuwa ni wasomi na Maulamaa hali ya kuwa hawana elimu yoyote isipokuwa bidhaa duni. Sisi tunahitaji wanafunzi watakaokuwa na elimu madhubuti iliyosimama juu ya Qur-aan na Hadiyth ili waijibishe fujo hii iliyozagaa mijini na vijijini.

Na kwa haya, tunaona kwamba kutafuta elimu hivi leo, ndio ‘amali bora zaidi ya kuwafikia viumbe, ndio bora zaidi kuliko Sadaqah, ndio bora zaidi kuliko Jihaad, bali ndio Jihaad ya kikweli, kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amekufanya kuwa sawa na Jihaad katika njia ya Allaah.

Na dalili ya hilo, ni neno Lake (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

« وما كان المؤمنون لينفروا كافة»

« Na wala haiwafalii Waumini kutoka wote »

 

Na hitimisho ni kwamba umma wa Kiislamu ni lazima uwe na Maulamaa waliobobea na wenye misingi imara ya elimu. Ama ikiwa mambo yatabakia hivi katika fujo, basi umma utakuwa katika hatari kubwa na wala dini haitalingamana kwa watu.

 

………………………………….

……………….

 

 

 

HADIYTH

 

Imepokelewa toka kwa Abu Dharri Jundub bin Junaadah (Allaah Amridhie) akisema:

 

قلت يا رسول الله، أي الأعمال أفضل؟ قال: ((الإيمان با لله والجهاد في سبيله)). قلت: أي الرقاب أفضل؟ قال: ((أنفسها عند أهلها، واكثرها ثمنا)). قلت: فإن لم أفعل؟ قال: ((تعين صانعا أو تصنع لأخرق)) قلت: يا رسول الله أرأيت إن ضعفت عن بعض العمل؟ قال: ((تكف شرك عن الناس فإنها صدقة منك على نفسك)). متفق عليه.

 

"Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni ‘amali zipi bora zaidi? Akasema: Kumwamini Allaah na Jihaad katika njia Yake. Nikasema: Ni watumwa gani bora zaidi (kuachwa huru)? Akasema: Ni wale wenye kupendwa zaidi na watu wao na wenye bei kubwa zaidi. Nikasema: Na kama sikufanya? Akasema: Msaidie mwenye kufanya jambo au mtengenezee asiyeweza kufanya vizuri. Nikasema: Ewe Mtume wa Allaah! Je, unasemaji ikiwa nitashindwa kufanya baadhi ya kazi? Akasema: Zuia shari yako kwa watu, kwani hiyo ni Sadaqah yako juu ya nafsi yako".

 

Mtunzi (Allaah Amrehemu) katika mlango wa kukithiri kheri, katika aliyoyanukulu toka kwa Abu Dharri (Allaah Amridhie) anaeleza kwamba Abu Dharri alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni ‘amali gani iliyo bora zaidi? Akasema:  ((Kumwamini Allaah na jihadi katika njia Yake)).

Na Maswahaba wanamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ‘amali bora zaidi ili wafanye na wala si kama waliokuja baada yao, kwani hawa huenda wakauliza kuhusu ‘amali bora zaidi, lakini wao hawatendi. Ama Maswahaba, bila shaka wao wanafanya. Na ndio huyu Ibn Mas’uud anamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni ipi ‘amali inayopendwa zaidi kwa Allaah? Akamwambia:

((Kuswali katika wakati wake)).

Nikasema: "Kisha ipi"? Akasema:

((Kuwatendea wema wazazi)).

Nikasema: "Kisha ipi"? Akasema: ((Kupigana jihadi katika Njia ya Allaah)).

 

Na huyu pia vile vile Abu Dharri (Allaah Amridhie) anamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ‘amali bora zaidi. Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akambainishia kuwa ‘amali bora zaidi ni kumwamini Allaah na Jihaad katika njia Yake. Kisha akamuuliza kuhusu watumwa, ni mtumwa gani aliye bora zaidi? Yaani, ni lipi bora zaidi katika kumwachilia huru mtumwa? Akasema:

((Ni wale wenye kupendwa zaidi na watu wao na wenye bei kubwa zaidi)).

 

Mtumwa huyu amekusanyikiwa sifa ya kupendwa na thamani kubwa. Na mfano wa mtumwa huyu, hamtoi isipokuwa mtu mwenye imani yenye nguvu.

Na hii ni kama neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

« لن تنالوا البر حتى تنفقوا مما تحبون »

« Hamtoupata wema mpaka mtoe mvipendavyo »

 

Na Ibn ´Umar (Allaah Amridhie) alikuwa kinapompendeza kitu katika mali yake, hukitoa kwa ajili ya kuifuata Aayah hii.

Kisha Abu Dharri (Allaah Amridhie) alimuuliza kuhusu kama hakupata, yaani mtumwa mwenye sifa hizi, akamwambia:

((Msaidie mwenye kufanya jambo au mtengenezee asiyeweza kufanya vizuri)).

Basi hili pia ni Sadaqah na ni katika matendo mema.

Akasema: "Na kama sikufanya?" Akasema:

((Zuia shari yako kwa watu, kwani hiyo ni Sadaqah yako juu ya nafsi yako)).

Na hili ndilo la chini zaidi mwanaadamu kuizuia shari yake kwa mwingine, watu wakasalimika naye.

 

_____________________________

______________

 

Share