Uadilifu Wa Maswahaba Na Utatanishi Wa Hadiyth Ya Hodhi

 

Imekusanywa Na Kutafsiriwa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’ay

Na Kupitiwa Na Abu 'Abdillaah

 

Yaliyomo

Utangulizi 1

Hadithi Ya Hodhi 2

Daraja Yao.. 3

Sifa Zao Ndani Ya Qur-aan.. 4

Sifa Zao Ndani Ya Sunnah.. 5

Katika Kauli Za Maulamaa.. 6

Wanafiki 9

Wenye Shaka Na Imani Dhaifu.. 10

Nani Atakayeondolewa?. 11

Alikuwa Akiwajua.. 15

Hitimisho.. 18

 

 

Utangulizi

Zipo baadhi ya hadithi zenye utatanishi au zenye kubeba maana zaidi ya moja, ambazo wakristo katika tovuti zao huzitumia kwa kuzifasiri hadithi hizo kwa maslahi yao, au kwa maana wanayoitaka wao, kinyume na maana yake ya kweli, kwa ajili ya kuupiga vita Uislamu.

 

Kinachoskitisha zaidi ni kuwa wapo baadhi ya wanaodai ni Waislamu ambao kwa kutaka maslahi yao, bila kujali athari wanayoiacha, utawakuta wakipoteza wakati wao mkubwa wakifanya utafiti na kunukuu hadithi za aina hizo huku wakitaja baadhi ya makosa ya kibinaadamu yaliyowahi kutendwa na baadhi ya Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum), kisha wanayakuza makosa hayo na kuyafanya kuwa ni dalili ya ubaya wa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

 

Yareti kama wakati wao wangeliupoteza katika kufanya utafiti juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu kama vile Abu Jahal au mnafiki Abdullahi bin Saluul au Firauni au Haaman au Abu Lu'ulua al Majusiy, aliyemuuwa Khalifa wa pili wa Waislamu Umar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu). Bali kinyume na hivyo, utawaona wanaunyamazia uadui wao watu hao, juu ya kuwa ukafiri wao umethibiti ndani ya Qur-aan tukufu na ndani ya mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na badala yake wanaziunguza juhudi zao katika kujaribu kuwapaka matope Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Kwa kufanya hivyo wanawapa makafiri silaha kali pamoja na ushahidi wanaoutaka katika kuupiga vita Uislamu na kuwapiga vita waliotuletea Dini hii, kwa sababu kwa kuwatuhumu Maswahaba bila ya uhakika wala ushahidi ulio wazi, ni kuutuhumu Uislamu waliotuletea Maswahaba hao (Radhiya Llaahu ‘anhum) baada ya kuupokea kutoka kwa sahibu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Hadithi Ya Hodhi

Miongoni mwa hadithi wanayoitumia katika ubabaishaji wao huo ni ile hadithi maarufu ya Hodhi, na namna Malaika watakavyowarudisha watu watakaotaka kunywa ndani ya hodhi hilo la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakidai kuwa hadithi hiyo inawakusudia Maswahaba hawa (Radhiya Llaahu ‘anhum) sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na marafiki zake na wenzake alioanza nao tokea siku ile ya mwanzo ya kuwalingania watu katika Dini hii tukufu.

 

Imepokelewa katika hadithi hiyo kuwa Siku ya Qiyaamah, wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atakapokuwa anawanywisha watu maji kutoka katika hodhi lake, watakuja Malaika na kuwaondoa makundi kati yao, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atakaposema:

"Hawa ni katika Maswahaba wangu."

Malaika watajibu:

"Je Unajua waliyoyazua baada yako?”

 

Na katika riwaya nyingine, Malaika watasema:

"Walirtaddi hawa wakarudi nyuma."

 

Anasema Ibni ‘Abdil Barr: "Maana hasa ya hadithi hizi ni kuwa kila mwenye kuzusha mambo katika Dini, atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)."

 

Tukiendelea na kuichambua Shub-ha hii inayowakanganya baadhi ya watu wakadhani kuwa watakaoondolewa penye hodhi ni hawa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) waliosimama naye tokea siku za mwanzo kisha wakaendelea kusimama naye katika shida zake zote na vita vyote dhidi ya makafiri; vita vya Badr, vita vya Bani Qaynuqaa, vita vya Uhud, vita Khandaq, Fat-hu Makkah, Hunayn na vita mbali mbali. Hawa ambao baada ya kufariki kwa sahibu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) waliendelea kuisimamia Dini hii kidete na kuipigania kwa hali zao na mali zao mpaka ikaenea ulimwengu mzima.

 

Daraja Yao

Daraja ya Maswahaba na heshima yao katika Dini ni jambo lisilokubali kujadiliwa na Muislamu yeyote mkweli mwenye kupenda haki, kwa sababu hawa ndio ambao Mwenyezi Mungu Aliwahusisha kwa kuwafanya kuwa sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakamsadiki na kumfuata na kumnusuru na wakaifuata nuru aliyokuja nayo, na wakafanya kila juhudi kwa kujitolea roho zao na mali zao kwa ajili ya kuipigania Dini hii tukufu mpaka ilipokamilika.

Hawa ndio wale waliosifiwa na Mwenyezi Mungu walipoambiwa kuwa wao ni umma bora kupita zote zilizoletwa kwa ajili ya watu. Na Mwenyezi Mungu Akaridhika nao.

 

Maswahaba ni waaminifu wa umma huu walioibeba shari’ah na kuieneza ulimwenguni kote mpaka ikatufikia sisi hivi sasa. Hii Qur-aan tuliyo nayo na haya mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yametufikia kupitia kwao (Radhiya Llaahu ‘anhum).

 

Kwa hivyo kitendo cha kuwatilia shaka Maswahaba hawa watukufu katika uadilifu wao ni katika kuipiga vita Dini na kuwafanya watu wasiamini masdari za Dini tulizopokea kutoka kwa Maswahaba hao watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum). Kwa sababu Qur-aan tukufu na Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), yote tumeyapata kupitia kwao.

Ndiyo maana Maulamaa wa Kiislamu wanatutaka tuwe na msimamo imara dhidi ya kila mwenye kuwatuhumu Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Inasikitisha kuona kuwa wapo miongoni mwa wanaodai kuwa ni Waislamu wenye kuwatuhumu baadhi ya Maswahaba, na wanafanya hivyo makusudi kwa ajili ya kukifikia kile wanachokitaka tu, na wakazitumia hizi hadithi za hodhi katika kujaribu kuwapaka matope Maswahaba hawa watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).

Katika kujaribu kuharibu sifa za Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum), wakazitumia hadithi mfano wa hii inayosema:

"Wakati mimi nimesimama, litakuja kundi, nitakapowajua, atatoka mtu kutoka kwangu na kusema: 'Twendeni', Nitasema: 'Wapi?' Atasema: 'Motoni wallahi.' Nitasema: 'Wana makosa gani?' Atasema: 'Hawa wamertaddi na kurudi nyuma baada yako.."

Al-Bukhaariy  na wengine

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Qur-aan

Maulamaa wanasema:

Wa kwanza kutoa hukmu Yake kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum), ni watu waadilifu ni Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kama ilivyoandikwa ndani ya Qur-aan tukufu na kama ilivyokuja kwa njia Mutawaatirah katika Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na miongoni mwa hukmu hizo ni kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliposema:

 

مُحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلا مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَانًا سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ذَلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَى عَلَى سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

 

“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu Amewaahidi walioamini na wakatenda mema”

Al-Fat-h: 29

 

Na Akasema:

وَالسَّابِقُونَ الأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَداً ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

 

“Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Muhaajiriyn na Answaar, na waliowafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu Ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

At-Tawbah: 100

 

Na Akasema:

لَـكِنِ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ جَاهَدُواْ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ وَأُوْلَـئِكَ لَهُمُ الْخَيْرَاتُ وَأُوْلَـئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

 

“Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye walipigania Jihaad kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakaopata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.”

At-Tawbah: 88

 

Na Akasema:

لَقَدْ رَضِيَ اللَّهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا

 

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu Amewapa radhi Waumini walipofungamana nawe chini ya mti, na Alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi Akateremsha utulivu juu yao, na Akawalipa kwa Ushindi wa karibu.”

Al-Fat-h: 18

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Sunnah

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Kheri ya watu ni wa karne yangu kisha wanaowafuata kisha wanaowafuata."

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Na kauli yake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

"Msiwatukane Swahaba wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya MwenyeziMungu kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao".

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Na akasema:

"Allaah Allaah! (nakuusieni) juu ya Swahaba wangu. Msiwageuze kuwa malengo yenu baada ya kuondoka kwangu. Kwani mwenye kuwapenda basi kwa kunipenda mimi (ndiyo) amewapenda, na mwenye kuwachukia basi kwa kunichukia mimi (ndiyo) amewachukia. Na mwenye kuwaudhi ameniudhi (na) mimi, na mwenye kuniudhi mimi amemuudhi Allaah, na mwenye kumuudhi Allaah, anakaribia Kumnyakua."

At-Tirmidhiy

 

Zipo hadithi nyingi za namna hii zenye kuwasifia na kueleza juu ya fadhila zao mbali mbali na mitihani waliyopambana nayo, na kututaka wafuasi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwaheshimu na kuwakirimu na kutowaudhi wala kuwageuza kuwa ni malengo yetu tunayoyatumia kila tunapotaka kuipitisha batil yetu. Na nasaha zote hizi zinatoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

 

Katika Kauli Za Maulamaa

Amesema Imam Ibn Najjaar:

"Aliyesifiwa namna hii na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), itakuwaje tena asiwe muadilifu. Ikiwa mbele ya mahakama wanatosha mashahidi wawili tu kuthibitisha uadilifu wa mtu, itakuwaje basi ikiwa ushahidi unatoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi (Subhaanahu wa Ta’ala)."

Sharhi ya Kawkab Al-Muniyr (2/475)

 

Anasema Al-Khatwiyb Al-Baghdaadiy:

"Usafi wa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) na uadilifu wao hauna lazma ya kusifiwa na wanaadamu baada ya kusifiwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyeangalia ndani ya nafsi zao Akatujulisha juu ya ukweli wao.

Na hata kama Mwenyezi Mungu Asingetujulisha juu ya sifa zao na kuridhika Kwake nao, basi kule kupigana kwao Jihaad kwa mali zao na nafsi zao, wamewaua baba zao na watoto wao waliopigana upande wa makafiri, haya yanatokana na yakini waliyokuwa nayo ndani ya nyoyo zao juu ya nusra ya Mwenyezi Mungu iliyowajia."

Al-Kifaayah fiy ‘Ilm An-Nihaayah: 48-49

 

Kwa hivyo kuzichukulia zile hadithi za hodhi kuwa waliokusudiwa ni hawa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) waliomsadiki na kumuamini, wakamsaidia na kumnusuru, kunakuwa ni kuzikataa aya zote na riwaya zote zilizo sahihi zenye kutubainishia fadhila zao na heshima yao mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Kuwatuhumu Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) ni mfano wa kuukataa ushahidi wa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa sababu itakuwaje Mwenyezi Mungu Atujulishe juu ya watu Alioridhika nao na kutujulisha juu ya fadhila zao na kwamba Atawaingiza katika Pepo Yake, kisha Asijuwe kuwa watu hao siku moja watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuzua nk.

Na huko pia ni kuzikanusha kauli za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyetujulisha juu ya kuridhika na Sahibu zake na kuwabashiria Pepo aliposema:

"Abu Bakr (yumo) Peponi, na ‘Umar (yumo) Peponi na ‘Uthmaan (yumo) Peponi na ‘Aliy (yumo) Peponi na Twalhah (yumo) Peponi na Az-Zubayr (yumo) Peponi na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (yumo) Peponi na Sa’ad (yumo) Peponi na Sa’iyd (yumo) Peponi na Abu ‘Ubaydah (yumo) Peponi"

Muslim na At-Tirmidhiy na Imaam Ahmad na wengine

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alifariki dunia akiwa ameridhika nao.

Na akasema (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):

"Haingii Motoni aliyeshiriki katika vita vya Badr."

Imam Ahmad na At-Twabaraaniy na wengine

 

Hivyo kweli inawezekana maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yapingane yenyewe kwa yenyewe? Leo amuambie kuwa wewe utaingia Peponi, na kesho amkute katika watakaorudishwa mbele ya hodhi?

Huku ni kukanusha wazi wazi maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Tutakwenda wapi na ile riwaya ya Attabarani kutoka kwa Abu Dar'daa (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa alimuambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, muombe Allah anijaalie nisiwe katika hao"

Akasema: "Wewe si katika hao."

 

Je, inawezekana kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) asijuwe hali ya Maswahaba wengine akaweza kujua hali ya Abu Dar'daa alipomjulisha kuwa hatokuwa miongoni mwa watakao ondolewa penye hodhi?

 

 

Wanafiki

Waliowahi kuonana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hawakuwa watu wa aina moja. Wapo miongoni mwao waliokuwa wanafiki waliokuwa wakijidhihirisha kinyume na walivyo, juu ya kuwa walikuwa wakishiriki vitani.

Mwenyezi Mungu Anasema:

إِذَا جَاءَكَ الْـمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللهِ وَاللهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْـمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ {المُنَافِقون: 1}.

“Wanapokujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo.”

Al-Munaafiquun: 1

 

Na wanapokuwa vitani huwa wakisema:

يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الاَعَزُّ مِنْهَا الاذَلَّ وَلِلَّهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لا يَعْلَمُونَ {المُنَافِقون: 8}.

“Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume Wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.”

Al-Munaafiquun: 8

 

 

Wenye Shaka Na Imani Dhaifu

Walikuwepo pia waliokuwa wakitia shaka, na pia walikuwepo wenye imani dhaifu miongoni mwa mabedui ambao wengi wao walirtaddi baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kufariki dunia.

Mwenyezi Mungu Anasema:

وَمِمَّنْ حَوْلَكُمْ مِنَ الاعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْـمَدِينَةِ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لا تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُمْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَى عَذَابٍ عَظِيمٍ- التوبة

“Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madiynah pia wapo waliobobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi Tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.”

At-Tawbah: 102

 

Hadithi zimeeleza wazi wazi wasfu na sababu za watu watakoondolewa penye hodhi, na wasfu huo haukubaliani na wasfu wa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliolelewa na kufundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na mpaka alipofariki dunia alikuwa radhi nao.

Na hii ni dalili kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) hawana uhusiano wowote na hadithi hizi, kwani hapana Swahaba hata mmoja aliyertaddi wala aliyezusha.

 

‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhum) wanaowatuhumiwa kuwa walizusha, wao walichofanya ni kuhuisha Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na wala hawajazusha jambo jipya katika Dini. Na hao tulisema kwamba tumeamrishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kufuata mwenendo wao.

Anasema Imam Al-Khutwaabiy:

"Hapana hata Swahaba mmoja aliyertaddi, bali waliortaddi ni makabila ya kibedui wasiowahi kuipigania Dini, na kwa ajili hiyo haipasi kuwatuhumu Maswahaba wale maarufu."

Fat-hul-Baariy 00/385

 

Anasema Imam Al-Baghdaadiy:

"Wamekubaliana maulamaa wote wa Kisunni ‘Ijmaa’ kuwa waliortaddi baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kufariki dunia walikuwa ni watu wa kabila la Bani Kindah na Haniyfah na Fizaarah na Bani Asad na Bani Bakar bin Waail. Hawa hawakuwa miongoni mwa watu wa Madiynah wala watu wa Makkah kabla ya kutekwa mji wa Makkah. Na kishari’ah wanaoitwa Muhajiriyn ni wale tu waliohaajir kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kabla ya Fat-hu Makkah."

Al-Farqu baynal Firaq

 

 

Nani Atakayeondolewa?

Wamekhitalifiana Maulamaa juu ya nani atakayeondolewa penye hodhi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) baada ya wote kukubaliana kuwa waliokusudiwa si Maswahaba hawa tunaowajua sisi.

 

Amesema Imam An-Nawawiy (Mwenyezi Mungu Amrehemu) katika sharh yake ya Muslim 3/136 -137 katika kuisherehesha hadithi hii ambayo ndani yake imo kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema: "Unajua namna waliyozusha baada yako?" 'Waliokusudiwa ni wanafiki waliortaddi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atakapowaita ataambiwa: "Hawa sio uliahidiwa, kwani hawa walibadilisha."

 

Na rai nyingine inasema kuwa watu hao ni wale waliokuwa Waislamu wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kisha wakartaddi baada ya kufariki kwake. Na atakapowaita, ataambiwa kuwa walirtaddi baada yake.

 

Rai ya tatu ni kuwa; hawa ni watu waliotenda maasi makubwa na Bida'h wakafariki kabla ya kutubu, juu ya kuwa walikuwa Waislamu.

Kauli kama hizi pia alizitaja Al-Qurtuby katika Al-Mufhim 1/503

 

Ikajulikana kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) hawamo katika wasfu huu. Na kama mtu atarudi kusoma wasfu wa nani Swahaba uliotajwa na Maulamaa mbali mbali atauona uhakika wa hayo.

Maulamaa wanasema kuwa Swahaba ni: "Mtu aliyemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa Muislamu na akafariki dunia akiwa katika hali hiyo."

 

Wasfu huu unawatoa wanafiki na waliortaddi, kwani wao si Maswahaba aslan. Watakuwaje Maswahaba wakati Maswahaba ni maadui wa waliortaddi na maadui wa wanafiki. Waliwapiga vita mpaka Mwenyezi Mungu Alipowapa ushindi juu yao. Na haya yalitokea baada ya kufariki dunia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wakati waliportaddi makabila mengi ya Kiarabu.

 

Na pia kuhusu kitendo cha Bida'h, ambayo ni sababu mojawapo ya kuondoshwa hodhini. Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikuwa msitari wa mbele kupiga vita kila aina ya Bida'h, bali matendo ya Bida'h hayajaenea isipokuwa baada ya kumalizika zama zao Maswahaba hawa (Radhiya Llaahu ‘anhum), na dalili ya maneno haya ni kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

"Nyota ndizo zinazolinda mbingu, zitakapoondoka, mbingu zitajiwa na kile kilichoahidiwa, na mimi ni mlinzi wa Swahibu zangu, nitakapo ondoka watakuja Swahibu zangu. Na Swahibu zangu ni walinzi wa ummah wangu, watakapoondoka, umati wangu utajiwa na kile walichoahidiwa."

Muslim, Imam Ahmad, At-Tirmidhiy na wengine.

 

Anasema Imam An-Nawawiy:

(Na Swahibu zangu ni walinzi wa ummah wangu, watakapoondoka, ummah wangu watajiwa na kile walichoahidiwa.) "Maana yake ni kuwa baada ya kuondoka Maswahaba watakuja wazushi na fitan ..."

 

Misimamo imara kama hii ya Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum), ambao baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kufariki dunia, walipopambana na maadui, na wakati huo huo walipambana na waliortaddi, na wakati huo huo  walifungua nchi nyingi na nyoyo nyingi, yote haya ni dalili kuwa wao ndio hasa wanaostahiki kunywa maji ndani ya hodhi.

 

Inawezekana pia kuwa watakoondolewa penye hodhi ni watu wenye wasfu ule wa kurtaddi, kwa sababu katika hadithi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Nitaambiwa kuwa hawa walirtaddi baada yako."

 

Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema kuwa sababu ya kuondoshwa penye hodhi ni kwa kurtaddi na kufanya matendo ya Bida'h, kwa hivyo bila shaka yoyote watakaoondoshwa hapo ni wale waliortaddi na waliozusha, na hapana hata mmoja kati ya Maswahaba hawa aliyenukuliwa kuwa alirtaddi.

 

Anasema Imaam Ibni ‘Abdil-Barr:

"Yeyote atakayezusha (atakayeingiza Bida'h yake) katika Dini, atakuwa miongoni mwa watakao ondoshwa penye hodhi."

 

Amesema Al-Qurtuby katika At-Tadhkirah 1/348:

"Maulamaa wetu wote wamesema kuwa; kila aliyertaddi katika Dini au aliyezusha Bida'h yake, kile asichokitolea amri Yake Mwenyezi Mungu, huyo atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi."

 

 

Alikuwa Akiwajua

Kule kusema kuwa alikuwa akiwajua, si lazima kumaanishe kuwa aliwahi kuwaona, bali aliwajua kwa alama maalum kama ilivyokuja katika Swahiyh Muslim kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

"Watarudishwa katika ummah wangu ninaowajua kama mtu anavyowajua ngamia wake." Wakamuuliza: "Utatujua?" Akasema: "Ndiyo, mtakuwa na alama hawana alama hizo wengine isipokuwa nyinyi. Mtarudishwa kutoka kwangu mkiwa weupe hamna madoa kwa athari ya Wudhuu, na wengine miongoni mwenu watazuiliwa hawatoweza kunifikia. Nitasema: "Ewe Mola wangu! Hawa ni Swahibu zangu." Atanijibu Malaika: "Unajua waliyozua baada yako?"

 

Kwa hivyo pale Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema: "miongoni mwenu", alikusudia 'miongoni mwa ummah wake', na maana yake ni kuwa; watafufuliwa ummah wake wote kwa alama za Wudhuu, na maana yake ni kuwa watafufuliwa pamoja na Waislamu wenzao, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atawajua kutokana na athari yao ya Wudhuu.

 

Nne: Riwaya hizi zimepokelewa kutoka vitabu sahih kutoka kwa hao Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum), akiwemo ‘Umar na Abu Hurayrah na ‘Aaishah na Ummu Salamah na Hudhayfah na Abu Sa’iyd Al-Khudriyy na Ibni Mas’uud na Anas na Sahal bin Sa’ad na Ibn ‘Abbaas na Mu'awiyah na wengine (Radhiya Llaahu ‘anhum).

 

Sasa ikiwa hawa ndio waliokusudiwa kuwa ndio watakaofukuzwa penye hodhi, inaingia akili kweli waje kutuhadithia na kutuhakikishia kuwa maneno haya wameyasikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), juu ya kuwa ndani ya hadithi hizi wanatuhumiwa kuwa watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuingiza Bida'h?

 

Tano: Wangelikuwa waliokusudiwa katika hadithi hizi ni Maswahaba ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwahutubia na kuwahadithia juu ya matukio haya, asingelikuwa na haja ya kusema: "Watarudishwa makundi ya watu kutoka kwangu." Au "Watu miongoni mwa Swahibu zangu watarudishwa penye hodhi." Au akasema: "Kisha atachukuliwa mmojawapo miongoni mwa Swahibu zangu." Badala yake angeliwaambia moja kwa moja bila kuwaficha, akawaambia kwa mfano: "Mtaondolewa penye hodhi, na kupelekwa mbali nami." Au "Fulani na fulani mtaondolewa penye hodhi." Na maneno yenye mfano huo, hii ikiwa ni dalili nyingine kuwa Maswahaba sio hawa waliokusudiwa katika riwaya hizi.

 

Sita: Lafdhi zilizokuja katika riwaya hizi kama vile 'Rahtw'   رهط na maana yake ni kikundi cha watu wasiotimia kumi nk. Ni dalili kuwa watakaoondolewa ni wachache sana.

 

Saba: Wengine wakatoa hata majina ya baadhi ya Maswahaba watakaotolewa penye hodhi. Na sisi tunawauliza; Wametoa wapi kauli za kuwahusisha baadhi ya Maswahaba kuwa wao ndio watakaoondolewa penye hodhi, na kwamba wao ndio waliortaddi na kuzusha mambo katika Dini, kisha wakawapangia wengine kuwa hao hawataondolewa? Wakati hadithi hazikutaja kwa majina yupi ataondolewa na yupi atakayebaki. Ushahidi walioutumia dhidi ya wenzao unaweza pia kutumiwa dhidi ya wanaowataka wao, juu ya kuwa sisi hatusema hivyo, hasa kwa vile hapana nassi inayoeleza kwa uwazi kuwa fulani ataondolewa na fulani atabaki.  Hadithi sahihi zimetuthibitishia kusifiwa kwa Maswahaba wote kwa ujumla, na kututhibitishia pia kuwa wao ni watu wa Peponi.

 

Kwa hivyo tunasema; Hao Maswahaba mnaowadhania kuwa watarudishwa penye hodhi, zipo dalili nyingi sana kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah zenye kuwasifia na kuwatakasa kwamba wao ndio walioamini hasa na kututhibitishia kwa dalili isiyokuwa na shaka kuwa wao ni watu wa Peponi.

 

Kutokana na haya, haki inadhihiri, na utatanishi unatoweka kwa sababu ya ushahidi usikuwa na uzito wowote.

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Atupe mwisho mwema na Atufufue chini ya bendera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).

 

 

Hitimisho

Kwa kumaliza tunasema:

Kwanza; waliokusudiwa kuwa ni Maswahaba katika hadithi hizi si Maswahaba bali ni wanafiki waliokuwa wakijifanya Waislamu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Mwenyezi Mungu amesema:

وَمِمَّنْ حَوْلَكُمْ مِنَ الاعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْـمَدِينَةِ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لا تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُمْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَى عَذَابٍ عَظِيمٍ- التوبة

“Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madiynah pia wapo waliobobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.”

At-Tawbah: 102

 

Pili; waliokusudiwa ni wale waliortaddi baada ya kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Inajulikana kuwa wengi miongoni mwa makabila ya Kiarabu yalirtaddi baada ya kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na hawa ndio kwa ajili yao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atasema:

"Swahibu zangu hawa." Na ataambiwa: "Hujui wewe waliyozusha baada yako. Waliendelea hawa kurtaddi tokea ulipofariki dunia."

 

Tatu; inaweza kumaanisha pia kuwa kila aliyemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hata kama hakuwa Swahaba kwa maana ya neno hilo, na dalili ni yule mkuu wa wanafiki ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul aliposema:

يَقُولُونَ لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الاَعَزُّ مِنْهَا الاذَلَّ وَلِلَّهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لا يَعْلَمُونَ {المُنَافِقون: 8}.

“Wanasema: Tukirejea Madiynah mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume Wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.

Al-Munafiquun - 8

 

 

 

Share