Mume Hana Uzazi, Naye Kashika Mimba Ya Zinaa, Amjulishe Mumewe Au Atoe Mimba?

SWALI:

Assalam alaikum,

Namshukuru Mungu Mola wa viumbe vyote.Ama baada ya haya nina tatizo naomba nisaidiwe mimi ni mwanamke mbaye nimeolewa na huu ni mwaka wa 3 lakini sikujaaliwa kupata mtoto na kwa upande wangu sikuwa na tatizo ila mume wangu ndio mwenye tatizo la kizazi lakini anatumia dawa za sunna. Kwa bahati mbaya na kwahamu niliyokuwa nayo ya mtoto nikafanya kosa nikatembea nnje siku 1 na wala sikukusudia kuwa nitakuwa na mimba bilisi tuu kanihadaa,baada ya 2 weeks nikajihisi nina mimba na hivi ni miezi 2.

jamani sasa mtoto wa mume au wa nje nifanyeje,nilipomueleza mume alifurahi sana lakini naogopa nitasema nini mimi kwake na kwa Mungu sasa mnanishauri vipi nifanye. au niitowe pia naogopa dhambi mbili kwa pamoja kuuwa na kuzini nje nisaidieni.natarajia majibu ya kuniongoza mazuri NA MUNGU ATANISAIDIA.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalah Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mimba ya zinaa.

 

 Mara nyingi sisi hufanya makosa yaliyo makubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka nasi tukawa ni wenye kusema bahati mbaya au Iblisi ndiye aliyekushawishi. Kudhania hivyo halitusaidii sisi na lolote wala chochote bali linatupatia sisi muhula na nafasi ya kufanya mengine na kisha kutoa hoja hizo hizo.

 

Haiwezekani kuwa ukawa umefanya tendo kama la zinaa kisha useme sikukusudia kwani kitendo hicho kinajumlisha mambo mengi sana. Mwanzo unaanza kumtongoza mwanamme au yeye akutongoze, mzungumze, mpeane miadi na mfanye kitendo chenyewe ambacho ni kibaya sana. Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wametuhimiza sana kuwa na subira katika mambo yetu yote. Kutokuwa na subira ndiko kumekutia katika njia panda. Na lau kama ungekuwa ni mwenye kuifikiria ile Aayah ya Suratush Shuuraa (42): 49-50 hungekuwa na tatizo kwani ungefahamu ya kuwa watoto wote wanatoka kwa Allaah. Hivyo, tatizo la ni kuhusu hilo na kuhangaika kutafuta madawa n.k.?

 

Muislamu hutakiwa na kutarajiwa awe na imani kuwa Allaah Humtunuku Amtakaye watoto na Humfanya Amtakaye tasa kwa rehma na uadilifu Wake kama inavyothibitisha Qur-aan:

"Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allaah; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia Amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia Amtakaye watoto wa kiume. Au Huwachanganya wanaume na wanawake, na Akamfanya Amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza". Ash-Shuraa: 49-50.

Hivyo basi hakuna makisio ya miaka wala muda kuwa ndio muda wa mwisho wa kukata tamaa kwa Muislamu kutunukiwa mtoto; kwani imethibiti kawaida kuwa watu hukaa baada ya kukaa zaidi ya miaka kumi ya ndoa yao na wakaja kutunukiwa watoto baada ya hapo.

Umesema, Kwa bahati mbaya na kwahamu niliyokuwa nayo ya mtoto nikafanya kosa nikatembea nnje

Ndugu yetu, hiyo haikuwa bahati mbaya bali ni malipo kwa asiyekuwa na imani kuwa Alilolikataza Allaah ni vyema tujiepushe nalo na kama ukipingana na hayo basi huenda Akakulipa hapa duniani kwa kukufedhehi kama ulivyofedheheka na hakuna anayekusuduia kushika mimba lakini Ibiliys hukushawishi na kukuhakikishia kuwa mara moja tu hakuna kitachotokea kwani uko na mumeo miaka mingapi na hukushika mimba basi jaribu tu hakuna kitu na sasa rafiki yako Ibiliys kakuacha mkono na anakujia kwa njia nyingine; njia ya kujisitiri na kutoa mimba.

Huyo mtoto uliyezaa nje ya ndoa hatambuliki kisheria, asli mtoto ni wa mwenye kitanda lakini wewe unaelewa vizuri kuwa si wa mumeo bali umemtia katika familia isiyomuhusu na imethibiti katika Hadiyth za Mtume (Swalah Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

 

عن أبي هريرة  رضي الله عنه عن النبي صلى الله   عليه السلام   حين نزلت آية المتلاعنين : ((أيما امرأة أدخلت على قوم من ليس منهم فليست من الله في شيء ولن يدخلها الله جنته وأيما رجل جحد ولده وهو ينظر إليه احتجب الله منه وفضحه على رؤوس الأولين والآخرين))

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ilipoteremsha Aayah ya waliolaaniwa akasema ((Mwanamke yeyote atakayeingiza katika watu asiyekuwemo katika wao basi hana kitu kwa Allaah na hatoingizwa na Allaah katika pepo Yake, na mwanamume yeyote akimkataa mtoto wake na yeye anamuona, basi Allaah Atamfungia (rehma Zake)  na Atamfedhehesha juu ya vichwa vya viumbe kuanzia wa mwanzo mpaka wa mwisho)) [Abu Daawuud, na Haakim kitabu cha Twalaaq, hadiythi namba 2814]

 

Na wewe bila ya shaka yoyote ile ushamtia katika famila asiyekuwemo yaani umechukua mimba kwa uzinifu na hali unaye mume basi umemuingizia katika familia yake asiyekuwa wake.

 

Na umesema kuwa ulipomweleza mume wako alifurahi sana, fahamu kuwa ni haki yake kufurahi lakini hukumueleza ukweli kwani mtoto ni wa mtu mwengine na si wa aliyekuoa na hilo ndilo ulilotakiwa kumueleza kama kweli ulikuwa na la kumueleza na kumfurahisha na huna njia ya kumueleza na hilo si tatizo kwani unaweza kuitafuta njia ya kumueleza na kumfahamisha kuwa hiyo mimba si yake bali ya mtu fulani.

Umesema, lakini naogopa nitasema nini mimi kwake na kwa Mungu,

Kumbuka hata rafiki yako (Ibiliys) aliyekuacha mkono baada ya kukutia katika dhambi la zinaa pia hudai kuwa anamuogopa Allaah kama inavyothibitisha Qur-aan kwa kusema:

"… Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namuogopa Allaah, Mola Mlezi wa walimwengu wote." Al-Hashr: 16.

Ushauri tunaoweza kukupa ni kama huu: Umetenda kosa lenye kustahiki adhabu iliyowekwa na Allaah nayo ni kupigwa mawe mpaka ukafa kwani wewe ni mzinifu mwenye mume au aliyeolewa au aliyewahi kuolewa; kwa kuwa hakuna pa kupitishiwa hukumu hiyo, hii haina maana kuwa umesameheka bali utaikuta huko mbele ya Allaah kama hukutubia na kukubaliwa tawbah yako, hivvyo basi njia ya kufanya ni kuomba tawbah, tawbah ya kweli kweli na kujuta kwa tendo hilo.

 

Kitendo ulichokifanya kimekufikisha katika njia panda na hilo limekufanya wewe uanze kufikiria maovu: Je, nitoe mimba au niseme uongo kwa mume wangu? Kuua kiumbe ni katika dhambi kubwa na kuhusu uongo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema kuwa Muumini hawezi kabisa kusema uongo. Njia iliyobaki ni kumwambia kweli mume wako, upate radhi za Allaah Aliyetukuka kuliko kumwambia uongo ukapata radhi ya mume lakini ukakasirikiwa na Allaah Aliyetukuka. Kisha ukisema uongo utakuwa umefanya dhuluma kwani huenda mkazaa na mumeo watoto kwani hakuna ugonjwa usiokuwa na dawa na hapo anapoaga dunia mtoto wako huyu wa kwanza wa nje ya ndoa akamrithi babake wakati ambapo katika sheria hafai kumrithi.

 

 

Ushauri wetu ni kuwa umtake msamaha mumeo na  kumuombea kwa Allaah awe na moyo wa kukukubalia na kukusamehe na katika kukusamehe pia anaweza akaamua kukuacha kwani hujaonyesha ikhlaas katika maisha yenu na inaonyesha una fadhilisha dunia mbele ya Aakhirah na hukuwa na elimu ya nani unayemuasi. Lakini huenda

 

Ama kutoa mamba, ni jambo lisilofaa kabisa na ni madhambi mengine ambayo utakuwa unayatafuta, soma hapa chini suala hilo:

Kutoa Mimba - Hukmu Na Kafara Yake

Pia soma jibu hapa chini linalohusiana na hili swali lako:

Nimekwenda Nje Ya Ndoa, Nimjulishe Mume Wangu?

Hivyo, muombe mume wako msamaha na muombe Allaah tawbah ya kweli na inshaAllaah Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa Kurehemu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share