Maulidi: Mjadala Baina Ya Salafi Na Sufi Kuhusu Maulidi

 

Mjadala Baina Ya Salafi Na Sufi Kuhusu Maulidi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Sufi:               

Hamwishi nyinyi Mawahabi kupinga Maulidi!

 

Salafi:           

Mawahabi? Kwani unavyojua wewe nini maana ya Uwahabi?

 

Sufi:                

Si ndio dhehebu linalopinga Maulidi?

 

Salafi:           

Maskini, ndio hivyo wengi hamjui maana yake mnapachika tu jina na wengineo mkidhani kuwa Wahabi ni dhehebu au kundi au kuna watu wanajiita hivyo? Tunafahamu nyinyi Masufi mnajiita Masufi na hamna ishkali katika hilo, Ibaadhi wanajiita Ibaadhi na hawana tatizo na hilo, Shia wanajiita Shia na wanaridhia hilo, lakini hakuna watu wanaojiita Wahabi wala hawaridhii hilo japo baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kama kushikamana na Sunnah za Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Uwahabi, basi hilo si tatizo. Lakini hakuna aliyetangulia katika Wanachuoni aliyejiita Wahabi. Basi hebu nikufahamishe hao waliotunga jina la Uwahabi, ni Masufi wenzako na Mashia na wakinasibisha jina hilo na mlinganiaji Mwanachuoni Muhammad bin Al-Wahhaaab ambaye amezaliwa mji wa ‘Uyaynah huko Saudia, alilinganiya watu wake waliokuwa wakifanya bid’ah nyingi na wakiabudu na kuomba kwenye makaburi na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Alilingania haki na akawatoa watu katika kiza cha shirki na bid’ah kwa kuwaelekeza katika Sunnah na Tawhiyd. Alipowalingania watu wake, wengi wao walimkanusha, lakini Da’wah yake ilikubaliwa katika kila pande za ulimwengu na Allaah Aliipa Tawfiyq kubwa. Na wale wazushi na washirikina ndio waliompinga na  ndio wakaja kuzua jina hilo la Uwahabi na kuwapachika wale wote wenye kufuata Manhaj hiyo aliyokuja nayo Imaam huyo, kuwa hao ni ‘Mawahabi’ ilhali yeye amekuja na mafunzo ya Qur-aan na Sunnah. Ajabu kubwa hao waliopachika wenzao majina, ndio hao hao wanawazushia kila anayefuata Sunnah na kupinga bid’ah kuwa ni Wahabi; hadi kufikia kuwapachika wale waliomtangulia Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) kuwa ni Mawahabi! Kwa hiyo, Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim,  Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam Ibn Al-Qayyim, na wengi wengine waliofariki kabla ya miaka mingi ya kuzaliwa Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab nao wakapachikwa kuwa ni Mawahabi!

 

Sufi:

Tuache hayo, sasa basi kwanini mnadai Maulidi ni bid’ah?

 

Salafi:           

Ndio, kwa sababu si Sunnah.

 

Sufi:               

Kwani je, kila lilokuwa si Sunnah kwenu ni bid’ah?

 

Salafi:            

Naam! Ikiwa ni ‘ibaadah.

 

Sufi:               

Unakusudia nini “ikiwa ni ‘ibaadah?”

 

Salafi:            

Ni 'amali yoyote ile inayoitakidiwa kuwa unamwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwayo au ‘amali unayotegemea kumridhisha kwayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au kupata thawabu.

 

Sufi:               

Basi kwa hiyo gari, miwani ni bid’ah? Na hali zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) watu walikuwa wakipanda ngamia.

 

Salafi:            

Hayo si ‘ibaadah, bali ni mambo ya kidunia na yanayohitajika kutumiwa kwa ajili ya kutekeleza ‘ibaadah. Mfano ngamia; Watu watawezaje kufika Makkah kutekeleza ‘ibaadah ya ‘Umrah na Hajj, na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameamrisha watu wafike huko kutoka kila pande za dunia kutekeleza fardhi hiyo ya Uislamu? Soma Aayah katika Suwratul-Hajj (22:27). Na Akawapa ujuzi na uwezo wana Aadam kuunda merikebu za kufikia huko kama ndege, gari, meli n.k. Na Akabashiria hayo katika Suwrah An-Nahl (16: 8):

 وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴿٨﴾

“Na Anaumba msivyovijua.”

 

Aayah hii Wafasiri wa Qur-aan kama Imaam As-Sa’diy (Rahimahu Allaah) amesema: “Ni ambavyo baada ya kumalizika kuteremshwa Qur-aan; vitu ambavyo watakuwa viumbe watavipanda katika nchi kavu na baharini, na angani na watavitumia katika manufaa yao na vyenye masilahi yao...”

 

Sufi:               

Yaa Akhiy! Sisi tunamdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Maulidi na tunamswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), sasa vipi ni bid’ah?

 

Salafi:            

Kwani sisi tumekukataza usimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)? Au tunakutakaza mtindo au njia unayotumia kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)?

 

Sufi:              

Sijakufahamu!

 

Salafi:            

Sisi hatukukatazi kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); unayo Qu-raan, na unazo Adkhaar (nyiradi) na du’aa zilizothibiti katika Sunnah. Lakini tunalokukataza ni jinsi unavyomdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na maovu, na shirki, na uzushi mnayoyasoma katika Maulidi ambayo mnayaitakidi.

Na tunapinga mnavyoitakidi kuwa tarehe 12 Rabiy’ul-Awwal ni siku aliyozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Sufi:             

Pingamizi zenu zimezidi!

 

Salafi:            

Hapana! Bali ni nyinyi mmezidi kukhalifu Sunnah nasi tunafanya juhudi kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kupendelea kukuongoeni katika ya haki, na tunakhofia kupotea kwa Sunnah.

 

Sufi:              

Haya! Na yepi mnayoyapinga katika Maulidi yenyewe?

 

Salafi:            

Kwanza ni mkusanyiko wenu wa kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Je kuna yeyote katika Swahaba kuanzia Abuu Bakr mpaka wa mwisho wake kabisa aliyefanya hayo?

  

Sufi:               

Hakuna!

 

Salafi:            

Na je, hivi mtakuwa nyinyi mnampenda zaidi kuliko walivyompenda Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na hali wao walikuwa tayari kupoteza nafsi zao na mali zao kwa ajili ya kumnusuru na kuinusuru Dini ya Kiislamu?

 

Sufi:            

Na kauli gani hizo au itikadi mnazozipinga katika Maulidi?

 

Salafi:            

Itikadi yenu kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anahudhuria Maulidi. Hayo pale mnapomuinukia kwa dalili kuwa mnainuka na kumuamkia mnaposema:

مرحبا يانور عيني مرحبا   مرحبا جد الحسين مرحبا

“Karibu Ee nuru ya jcho langu, karibu! “Karibu babu yake Husayn, karibu!”

 Na mnasema pia:

هذا الحبيب مع الاحباب قد حضرا وسامح الكل فيما قد مضى وجرى

“Huyu ni kipenzi yuko pamoja na wapenzi, amehudhuruia na amesamehe kila yaliyopita na yanayoendelea.”

 

 

Kwani kuna mja anaweza kusamehe madhambi ya  waja na hali yeye mwenyewe ni mja na si Allaah?

Na pia kuna kauli na maneno mengineyo ya shirki mfano kauli yenu katika Maulidi:

 الف صلى الله عليك يانبي يامجلي الهم والكرب

“Allaah Akuswalie mara elfu ee Nabiy, Ee mwenye kuondosha dhiki na janga!”

 

Na mnaumuita Allaah 'Huwa Huwa' (Yeye Yeye)!

    

Na Mnasema pale kila mnapoita:

 

'Yaa Huwa' (Ee Yeye) na hali Yeye kasema, Ee mja wangu mimi ni Allaah.

 

Na pia kuna maneno na kauli nyingi za kiashiki. Na wengi wenu maskini hamjui wanayoyasema watunga Maulidi humo!

 

Sufi:              

Enhee! Na vipi mnasema kuwa tarehe 12 Rabiy’ul-Awwal haikuthibiti kuwa ni siku aliyozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

Salafi:            

Naam! Kwani Wanavyuoni wamekubaliana kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa ‘Aam Al-Fiyl’ (Mwaka wa tembo) lakini wamekhitilafiana kuhusu tarehe. Na kuna kauli tofuati mbali mbali, na wala haikuthibiti hata katika Hadiyth moja Swahiyh. Na zile Hadiyth ambazo zimetaja, basi ni Hadiyth dhaifu. Kuna waliosema ni tarehe 9 Rabiy’ul-Awwal, kuna waliosema ni tarehe 12 Rabiy’ul-Awwal, na kuna waliokhitilafiana hata mwezi aliozaliwa. Kuna waliosema ni mwezi wa Swafar, wengine wamesema Ramadhwaan n.k.  Na ikiwa ni tarehe 12 Rabiy’ul-Awwal ambayo wengi wenu mnaitakidi, basi siku hiyo ndiyo ambayo imethibiti kabisa kuwa ndio siku aliyofariki. Sasa je, mnasherehekea mazazi yake au mauti yake?

 

Basi kwanini mnashikilia siku hiyo ya tarehe 12 Rabiy'ul-Awwal pamoja na kuwa kuna tofauti (ya tarehe aliyozaliwa)? Lakini hili la tarehe si muhimu kwetu, wala hatujaalii kuwa ni nukta ya mgogoro, lakini ni kiasi tu cha ziada katika kuwabainishieni nyinyi na wengine.

 

Sufi:               

Haya! Na je kila ‘ibaadah kwani lazima iwe katika matendo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

Salafi:            

Bila shaka! Kwa sababu Swahaba katika zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wanapotenda 'amali basi alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ima akiwafikiana nayo kwa kauli yake au kuinyamazia. Vinginevyo akiwakataza.

  

Sufi:              

Nipe mfano ya kauli yako hiyo kuwa alikuwa akiwafikiana nao 'amali au akiwanyamazia au akiwakataza.

 

Salafi:            

Alikuwa akiwakubalia 'amali au akiwanyamazia mfano kunyamaza kwake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pale Swahaba mmoja aliposema baada ya kurukuu:

رَبَّنـا وَلَكَ الحَمْـدُ حَمْـداً كَثـيراً طَيِّـباً مُـبارَكاً فيه

Rabbanaa walakal-hamdu, hamdan kathiyran twayyiban mubaarakan fiyhi

Ee Rabb wetu, ni Himidi ni Zako, Himidi nyingi, nzuri, zenye Baraka

Mpaka mwisho wake.

 

Na maana ya kuwanyamazia ni kuwa alipoona baadhi ya ’ibaadah walizofanya Swahaba hawakuwakataza wao kutenda hilo, na hilo hujulikana kama kitendo cha Swahaba katika zama zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam).

Ama kuwakataza kwake ni mfano pale Swahaba watatu waliotaka kufanya ‘ibaadah kwa Allaah, waache starehe walizohalalishiwa. Akasema mmoja wao: “Sitooa wanawake kamwe!” Mwengine akasema: “Nitafunga Swawm milele na sitofuturu kamwe!” Mwengine akasema: “Nitasimama kuswali usiku kucha sitolala!”

Basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawakataza na akasema: “Hakika mimi nafunga Swawm na nafungua, na naoa wanawake, na naamka usiku kuswali na nalala. Basi atakayejiepusha na Sunnah zangu, huyo si miongoni mwangu.”

 

Sufi:               

Lakini sisi tunampenda Nabiy na tunataka kuhuisha kumbukumbu zake.

 

Salafi:          

Na sisi pia tunampenda Nabiy na tunataka kuhusisha kumbukumbu zake kwa kudhihirisha Sunnah zake na kumtii na kuacha kumuasi.

 

Sufi:               

Lazima tuwe na kumbukumbu zake ili kuwafungamanisha watu naye. 

 

Salafi:            

Je, kuwafungamanisha watu na yeye kunakuwa kwa siku moja katika mwaka? Kwanini hamuwaiti watu katika masiku yote ya mwaka washikamane na Sunnah na kuacha kumpinga?

 

Sufi:            

Hayo yanafaa na haya yanafaa.

 

Salafi:            

Hapana!  Hapana!   Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

"Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah.” [Aal-‘Imraan: 31].  Na wala Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema: “Fanyeni kumbukumbu ya mazazi yangu!”

 

Sufi:             

Lakini Maulidi ni bid’ah hasanah (uzushi mzuri).

 

Salafi:            

Hakuna katika Uislamu bid’ah hasanah (uzushi mzuri) kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema katika kila khutbah yake: “Kila uzushi ni upotofu na kila upotofu ni motoni.”

 

Sufi:           

Mbona basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 “Atakayehuisha kitendo kizuri katika Uislamu atapata thawabu na thawabu ya kila atakayekifanyia kazi?” 

 

Salafi:       

Naam, amesema lakini Hadiyth hiyo inasema: “Kitendo kizuri” haikusema “bid-ah hasanah” (uzushi mzuri).

 

Sufi:               

Unanichanganya sasa kwa hoja zako nyingi!

 

Salafi:            

Ama sisi hatuchanganyikiwi! Hoja zetu zote zina dalili za waziwazi si kama hoja zenu!  Na ingekuwa moyo wako unataka kukubali haki usingechanganyikiwa kamwe!  Na chukua faida hizi:

Kwanza: Hadiyth imehadithiwa na Imaam Muslim katika Mlango wa Swadaqah. Na imeleezea kuwa: “Watu wa kabila la Mudhwarr walikuwa mafakiri na wakajisitiri miili yao kwa nguo za sufi zenye mistari, wakaja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Masjid, uso wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ukabadilika kwa kukosa furaha, yaani ukadhihirisha huzuni. Akasimama akawaswalisha watu kisha akawatolea khutbah akawahimiza watoe swadaqah. Wa kwanza katika waliotoa swadaqah zao ni Swahaba aliyesemekana ni kutoka Answaar akaja na chakula na nguo kutolea swadaqah. Kisha Swahaba wengineo wakamfuata kutoa swadaqah, hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akafurahi na uso wake ukarudi kuwa mzuri wenye furaha na ndipo aliposema:

“Atakayehuisha kitendo kizuri katika Uislamu atapata thawabu na thawabu ya kila atakayekifanyia kazi mpaka Siku ya Qiyaamah…. ” 

Sasa je, swadaqah ni bid’ah (uzushi) mpya?  

 

Sufi:              

Hapana.

 

Salafi:            

Kwa hiyo tumefahamu kuwa mashindano hapo ya Maswahaba katika kutekeleza Sunnah; na inaonesha kupendekezwa mashindano wafanye Waislamu (katika mambo ya khayr).

Na Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: “Inamaanisha: “Atakayehuisha Sunnah itakayokufa baada yangu…”

 

Na Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) alitoa mfano mzuri kuhusu Hadiyth hiyo akasema, ni mfano mtu kaenda katika kitongoji na akakuta watu wamezoea kunyoa ndevu na akawapa dalili za umuhimu na uwajibu wa ndevu kutoka katika Ahaadiyth kisha watu hao wakaanza kufuga ndevu; basi mtu huyo atakuwa amehuisha Sunnah ambayo ilikuwa imefishwa katika eneo hilo...

 

 

 

Mwisho wa Mjadala

 

************************

 

Tanbihi:

Mijadala aina hii ni mingi na iko katika mifumo tofauti lakini aghlabu hoja za watetezi wa Mawlidi zinafanana ni hizo kwa hizo, lakini majibu dhidi ya hoja hizo ni mengi na dalili ni nyingi. Mfano wa moja ya mjadala bora ni baina ya Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) na mmoja katika watetezi wa Maulidi ambao umo pia katika tovuti yenu ya alhidaaya. Unapatikana katika kiungo hapa chini:

 

Mjadala Baina Imaam Al-Albaaniy Na Msherehekeaji Maulidi​

http://alhidaaya.com/sw/node/7606   

 

 

 

Share