Mawlid: Kusherehekea Kuzaliwa Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Mawlid (Kusherehekea Kuzaliwa Kwa Mtume)

Imetarjumiwa na Naaswir Haamid

 

 

Kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume ni bid'ah (uzushi ndani ya diyn); Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakupata kuwaamrisha wengine kufanya hivyo, na wala hakuwa na Maswahaba pembeni mwake wenye kufanya jambo hilo na hivyo hakuna ruhusa iliyotolewa (ikiwemo ile ya kuridhia).

Hatutakiwi kutofautisha miongoni mwa Mtume yeyote. Kwa mfano tofauti ya hadhi, kama vile mmoja ni bora kuliko mwengine. Hili linapelekea kwenye ibada ya kishirikina, kama vile walivyofanya Wakristo walipoanza kumuabudia Yesu badala ya kumtambua kama ni Mtume tu. Ukweli ni kwamba wamechupa hatua mbali zaidi… na waliendelea kumuabudia, hadi hatua tunayoiona leo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msinitukuze Kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Mjumbe Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Lililo muhimu baina ya kila Mtume na/au Mjumbe ni UJUMBE.

 

 

HATARI YA KUZUSHA MAMBO NDANI YA DIYN

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Maneno bora  ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika diyn) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake] 

 

 

USITOFAUTISHE BAINA YA MITUME/WAJUMBE

 

Qur-aan Tukufu inasema:

{{Mtume ameamni yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waislamu, (pia wameamini hayo): wote wamemwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Yake; (nao hao Waislamu na Mtume wao husema), "Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume Yake (wote tunawaamini)." Na husema: "Tumesikia na tumetii. (Tunakuomba) msamaha, Mola wetu! Na marejeo ni Kwako."}} [Al-Baqarah: 285]

 

{{Semeni nyinyi (Waislamu waambiwe Mayahudi na Manasara; waambieni): "Tumemawamni Mwenyezi Mungu na yale yaliyoteremeshiwa, na yale yaliyoteremshwa kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl, na Is-haaq na Ya’aquub na kizazi (chake Ya’aquub); na waliyopewa Muusa na 'Iysa na pia yale waliyopewa Manabii (wengine) kutoka kwa Mola wao; hatutafautishi baina ya yoyote katika hao. (Wote tunawaamini); na sisi tumenyenyekea Kwake."}} [Al-Baqarah: 136]

 

{{Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume Yake wala wasimfarikishe yoyote katika wao (bali wamewaamini wote), hao Atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.}} [An-Nisaa: 152]

 

{{Na (kumbukheni khabari hii nayo:) Tulipochukua ahadi yenu; kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtawatoa watu wema katika miji yenu; nanyi mkakubali (wala msifuate). Na mnajua (kuwa mlikubali wala msifuate).}} [Al-Baqarah: 84]

 

 

USHIRIKINA WA KUKITHIRISHA KUMSWALIA MTUME

 

Hivyo, sasa, tunawauliza wale wanaosisitiza kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume… wakiwa na ithibati zilizo wazi bila ya kutofautisha baina ya Mitume… kwa nini hawasherehekei kuzaliwa kwa Mitume WOTE? Mfano 'Iysa? Unaweza kusherehekea tarehe 25 ya Disemba au kuchagua tarehe nyengine kama hawahitajii hii. Ahaa, sasa nimeona, munazo (hoja) nzuri za kutosherehekea kuzaliwa kwa 'Iysa?? Labda sababu ya kwamba musisherehekee kuzaliwa kwa 'Iysa, ndizo hizo hizo za kwamba musisherehekee kuzaliwa kwa Muhammad? Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Basi Anapowapa (mtoto) mwema (kamili) wanamfanyia Mungu washirika katika kile alichowapa (naye ni yule mtoto). Ametukuka Mwenyezi Mungu na huko kushirikisha kwao.}} [Al-A'Raaf: 90]

 

Ushahidi wa wazi kabisa. Lakini baadhi yao wanaita "mapenzi" na huko ni kwenda mbali kwa yale waliyoamrishwa.

 

Kukithiri kumsifu mtu inazuiliwa. Inaangukia mara moja kwenye shirki. Kufanya jambo lolote kupindukia mpaka wa kile tulichoamrishwa kufanya, ni kuchupa mipaka na kujikalifisha nafsi yake mwenyewe.

 

Bedui mmoja alikuja kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza kuhusu wudhuu. Alifafanua (akiosha kila kiungo cha mwili wake) mara tatu, na kusema: "Hivyo ndio (namna) ya wudhuu. Na anayefanya zaidi ya hivi amefanya kosa, kuchupa mpaka na kujikalifisha (mwenyewe)." [Imepokewa na Nasa'i, Ibn Maajah na Abu Daawuud]

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Enyi watu wa Kitabu (Mayahudi na Manaswara)! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli…}} [An-Nisaa: 171]

 

 

 

WALE WANAOSEMA: "NITAMPENDA ZAIDI YAKO, KWA KUTOMTII"

 

Ni lazima tumpende Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko Mitume wengine yoyote, na pale Mjumbe wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaposema:

Imesimuliwa na Abu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Naapa kwa Yule Ambaye maisha yangu yamo Mikononi Mwake, hakuna mmoja atakayeamini hadi anipende mimi kuliko baba yake na watoto wake." [Imepokewa na al-Bukhaariy]

 

Hii ina maana kwamba TARATIBU zake, SUNNAH zake – (ni bora zaidi) kuliko ukaribu wa kifamilia; kumbuka, tunaonesha mapenzi kwa kuwa watiifu. Kwa mfano, huwezi kwenda kumpiga mtu katika kichwa chake na kisha kusema: "lakini unajua kwamba nakupenda kweli kweli." Au, wadhalilishaji wanavyofanya, wanapiga kipigo kwa mwenza na kisha wanakiita kitendo hicho ni kitendo cha mapenzi (ndivyo, baadhi yao wanasema haswa kwamba NDIO SABABU ya kumpiga!)

 

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefikisha Ujumbe bora. Alikuwa na dhamana malumu. Lakini yeye, mwenyewe, alikuwa ni mtu kama alivyo mwengine – masikini, asiyejua hata kusoma - isipokuwa alikuwa na sifa malumu ya hayaa. Hilo linaweza kusemwa kuwepo kwa Mitume na Wajumbe wote; walikuwa na hayaa nyingi. Sifa hii – hayaa – inaweza kutumika. Hakuna sifa nyengine inayoweza kutumika kumpa heshima mwengine juu ya mwengine. Hivyo, tunaweza kusema kwamba Mitume wote walikuwa ni wacha Mungu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Enyi watu! Kwa hakika Tumekuumbeni (nyote) kwa (yule) mwanamume (mmoja, Adamu) na (yule) mwanamke (mmoja; Hawwaa). Na Tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane (tu basi, siyo mkejeliane). Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi. Kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari (za mambo yote).}} [Al-Hujuraat: 13]

 

Imesimuliwa na Abu Dharr kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwambia: "Nyinyi sio wabora kuliko watu wenye ngozi nyekundu au nyeusi isipokuwa pale mutakapowazidi kwa uchaji Mungu." [Imepokewa na At-Tirmidhiyy]

 

Sifa kubwa ya Masufi wa sasa ni kuwa na "mapenzi" kwa Mtume sana hadi wanajihusisha na shirki pamoja na mapenzi haya. Hata hivyo, sio sahihi kuwa na kiwango hicho cha mapenzi pale inaposababisha kuchupa mipaka na kuingiza uasi.

 

 

'IYD MBILI ZINACHUKUA NAFASI YA SIKUKUU ZOTE

 

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaeleza ya kwamba alipohama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah walikuwa na siku mbili walizokuwa wakicheza ndani yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika Allaah Aliyetukuka Amewabadilishia siku zilizo bora kuliko hizo – Siku ya Fitr ('Iydul Fitwr baada ya kufunga mwezi wa Ramadhaan) na Siku ya Adh-haa ('Iyd kubwa ya baada ya Hijjah)” [Imepokelewa na Abu Daawuud]

 

 

FATWA KUTOKA KWA SHAYKH BIN 'UTHAIMIYN[1]

 

Mwanachuoni mkubwa Muhammad Swaalih bin 'Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) aliulizwa kuhusiana na sherehe za kuzaliwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambapo alijibu:

 

Kwa kuanzia, siku haswa ya kuzaliwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haijulikani kwa uhakika. Isipokuwa, wachunguzi wa sasa wamethibitisha kwamba alikufa tarehe 9 ya Rabi'ul Awwal na sio tarehe 12 (kama inavyoaminika sana), na hivyo hakuna msingi wa historia kwa kunasibisha tarehe 12 na sherehe.

 

Tukienda mbali zaidi, sherehe hizi hazina msingi ndani ya mafunzo ya diyn, kwani kama ingeshurutishwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliifanyia kazi au kuliamrisha ummah wake kufanya hivyo. Kama angekuwa amefanya au ameamrisha taifa lake kufanya hivyo, ingekuwepo na (kila) sababu ya kuiendeleza, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amesema:

 

{{Hakika Sisi ndio tulioteremsha mauidha haya (hii Qur-aan); na hakika Sisi ndio tutakayoyalinda.}} [Al-Hijri: 9]

 

Kwa vile (jambo) hili halijasimuliwa, tunakuja kufahamu kwamba halijatokana na diyn ya Allaah. Kama sio kutokana na diyn ya Allaah, basi hapana ruhusa kwetu sisi kumuabudia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kuomba kuwa karibu Naye kwa mtindo huu. Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ametuwekea njia malumu kwetu kuifuata ili kupata Radhi Zake, ambayo pia ni njia ya Mjumbe wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa nini iruhusike kwetu sisi, wakati sisi ni waja tu, kutengeneza njia nyengine inayopelekea kwenye Radhi za Allaah kutokana na nafsi zetu wenyewe (yaani sio iliyoshushwa)? Hakika ni uasi dhidi ya Haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuweka Sheria ndani ya diyn Yake ambayo sio sehemu ya hilo. Juu ya hivyo, hili linaingiza ukanushaji wa yale Aliyoyasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ndani ya Qur-aan:

 

{{Leo Nimekukamilishieni Diyn yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Diyn yenu.}} [Al-Maaidah: 3]

 

Iwapo sherehe hizi zimetokana na Ukamilifu wa Diyn, basi ni lazima itakuwa ilikuwepo kabla ya kifo cha Mjumbe wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kama haitokani na Ukamilifu wa Diyn, basi haiwezekani kwamba ikawa inatokana na diyn, kwani Allaah Amekwisha sema: "Leo Nimekukamilishieni Diyn yenu". Yeyote anayedai kwamba ni sehemu ya Ukamilifu wa Diyn iliyotokea baada ya kifo cha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi dai lake linapelekea kukana Aayah hii ya Qur-aan. Bila ya shaka yoyote kuwa wale wanaosherehekea kuzaliwa kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wanapendelea kuongeza mambo, kukithirisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),  kuonesha mapenzi kwake yeye, na kuzidisha hisia zao ili kudhihirisha yaliyomo ndani ya nyoyo zao kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Matendo yote haya ni matendo ya ibada. Mapenzi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ibada ambayo inahitajika kwa ajili ya iymaan, kwani iymaan ya mtu haikamiliki hadi ampende Mtume kuliko nafsi yake, mtoto wake, baba yake, na viumbe vyote. Kupamba ibada, kuiga matendo na kumswalia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) yote ni matendo ya ibada na yanatokana na diyn, kama ilivyo kuonesha hisia kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa vile (matendo hayo) yanamkaribisha mja kwa diyn ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Kinachofuata hapo ni kwamba sherehe za kuzaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa lengo la kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumswalia Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanatambulika kama ni matendo ya ibada, na kwa vile ni matendo ya ibada basi hakuna ruhusa ya kuzusha chochote kipya ndani ya diyn ambacho hakina mnasaba. Hivyo, sherehe za kuzaliwa ni uzushi na zinazuiwa. Pia, tunasikia ripoti kadhaa kwamba sherehe hizi zina matendo mengi yasiyofaa ndani yake, ambayo sio ya diyn, hisia za mtu, wala mtu yeyote mwenye akili timamu atayafanya kuyaruhusu. Wanaimba nyimbo na mashairi ambayo yanaenda mbali kabisa dhidi ya Mtume, mbali zaidi hadi kumtukuza kuliko Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na hifadhi haiombwi isipokuwa kwa Allaah. Pia tunasikia kuhusu ujinga wa baadhi ya washiriki, kwamba pale msomaji anaposimulia hadithi ya kuzaliwa kwake na kufikia sehemu ya kutoka tumboni mwa mama yake, wote wanasimama pamoja kwa heshima wakisema na kuamini kwamba roho na karama zake za Ujumbe wa Allaah, zimehudhuria pamoja nao kwenye sherehe, na kwamba wanasimama bila ya desturi malumu. Hili hakika ni wazimu na ushirikina ulio wazi. Pia, sio mnasaba kumsimamia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa vile alikuwa halipendelei hilo. Maswahaaba, waliokuwa wakimpenda na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko mtu mwengine yeyote, katu hawatomsimamia pale akiwa yuhai pamoja nao kwa kukasirika kwake (kutokana na jambo hilo), basi ni ujinga ulioje wa ushirikina huu usiokuwa na msingi wowote?

 

Sherehe za kuzaliwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni uzushi mkubwa usiopata kutokea hadi baada ya vizazi vitatu vya wacha Mungu baada ya kifo cha Mjumbe wa Allaah, na ni sherehe iliyojaa mambo yasiyopendeza na ya kiajabu ambayo yanapingana na msingi wa diyn ya Kiislamu, baya zaidi ni mchanganyiko na mwingiliano wa wanaume na wanawake pamoja ndani ya eneo moja (pamoja) na (kuwepo kwa) matendo mengi yasiyokubalika.

 

 

[1] Majmuu’ Fataawaa, Muhammad bin Swaalih al-'Uthaymiyn juz. 2/ uk.297-300

 

Share