Kitoka Nyumba Hupewa Mke Mkubwa Pindi Mume Anapooa Mke Wa Pili?

SWALI:

 

Assalam alaikum warahmatullahi wabarakatu..........

 

Swala langu ni kuhusu "Kitoka nyumba" ...hii ni kama ada ambayo watu wanasema kuwa anapewa mke mkubwa na mumewe atakapo kuwa yule mume ameowa mke wa pili......Je hili jambo ni la sawa ama ni uzushi tu.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kitoka nyumba kwa mke wa kwanza baada ya mume kuoa mke wa pili.

Kuhusu Kitoka Nyumba au Kupewa mke Mut’ah (Mataa’ kwa wingi) hii Mut’ah ina maana ni kile ‘Kiliwazo’ na pia inajulikana kama ‘Kitoka Nyumba’ au ‘Masurufu Talaka’ ambacho anapewa mwanamke pindi anapoachwa na mumewe   kama Alivyotaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ))

((Na wanawake walioachwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa wacha Mungu)) [al-Baqarah: 241]

 

Nayo inahusu katika talaka ya mke yeyote yule ikiwa wa kwanza au wa pili, au watatu au wane.

 

Na ikiwa hicho Kitoka nyumba au haki katika sehemu nyingine za Afrika Mashariki ni pesa au kitu kingine chochote ambacho anapatiwa mke mkubwa pindi mume anapooa mke mwingine na imezoeleka hivyo basi hiyo itakuwa ni ada ambayo inatumika katika baadhi ya makabila isiyopingana na sheria ya Kiislamu. Hili ni chimbuko katika sheria yetu ya Kiislamu inayojulikana kamaUrf (ada au desturi). Hivyo ikiwa wamekubaliana hayo watu wa maeneo Fulani basi hakuna tatizo maadam haipingani na Shari’ah ya Kiislam. Lakini lisiwe ni jambo la kulazimishana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share