Baba Amempa Mkewe Wa Pili Dhahabu Za Mama Yetu - Naye Baba Kafariki Je Tunayo Haki Kumdai Mama Wa Kambo Hizo Dhahabu?

SWALI:

 

Salaam alaykum! Mimi nina swali, wakati marehem mama yangu amefariki aliacha vitu vya dhahabu na sisi kipindi hicho tulikuwa wadogo sana, baada ya muda baba akaja akapata mwanamke mwingine akachukuwa dhahabu za mama yetu akampa yule mwanamke sasa hivi na baba nae kashafariki pia, na pia kwa sasa tunaakili zetu je tunaweza kumdai yule mwanamke hizo dhahabu? Shukrani

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi za dhahabu za mama yenu.

Kabla hatujaingia katika kujibu lako tungependa kumnasihi kila mmoja na sisi wenyewe pia tuwe na adabu tunapowaita mama zetu. Haifai kwetu sisi kuwaita mama wa kambo kuwa ni mwanamke badala ya mama. Kwa hali yoyote ile mwanamke yeyote anayeolewa na baba ya mmoja wetu anakuwa ni mama, kwani huwezi kumuoa hata baba akiaga dunia. Hivyo, inatakiwa tuwape heshima wanayostahiki.

 

Swali lililo juu halieleweki vyema kwani hukutueleza kama vitu hivyo vya dhahabu vilikuwa ni vya mama au alikuwa amepewa na baba kwa matumizi tu.

Tuchukue ni vyake miliki yake kwa hivyo itakuwa nanyi mpate haki yenu kulingana na idadi yenu mlivyo. Ikiwa ni hivyo baba yenu pia atakuwa ana haki ya dhahabu hizo, naye atapata robo ya mali ya mama yenu. Kwa jinsi hiyo nanyi mtakuwa na haki ya dhahabu hizo.

 

Ikiwa ni hivyo mlivyosema basi baba yenu atakuwa na makosa nanyi mnatakiwa mumsamehe baba yenu kwa kosa hilo. Ikiwa mmeshamsamehe baba yenu kwa kosa hilo mnaweza kufanya moja kati ya mawili:

 

1.     Kumsamehe na kumuachia mama yenu hizo dhahabu na kutomdai.

2.     Kumdai haki yenu lakini kwa njia iliyo nzuri ya hekima si kwa ujeuri wala matusi.

 

Ikiwa mmechukua njia ya pili itabidi mwende nyinyi wenyewe kwa mama yenu, au mumtumie watu wazima wenye busara au kwenda kwa Qaadhi ili mpate haki yenu hiyo. Hata hivyo, njia ya mwisho si nzuri kwani mtakuwa mumekiuka nidhamu iliyopo.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awape ilhamu ya kufuata njia iliyo bora.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share