Mama Amesababisha Kifo Cha Mume Je, Anayo Haki Kurithi?

SWALI

Assalam Alaykum

Naomba kupatiwa jibu la suala langu lifuatalo. Mama katika familia amepika chakula na baada ya kuliwa kilisababisha kuumwa na kufariki kwa mume wake na mtoto wake mmoja. Huyu mama yeye hakula hiki chakula sababu hakipendi na ni kawaida yake kutokula chakula hicho na pia madaktari wamethibitisha kuwa vifo hivyo vimesababishwa na “food poisoning” ilotokana na vimelea (bacteria). Jee katika mazingira hayo huyu mama anayo haki ya kurithi mali ya mumewe? Wabillah Tawfiq

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu jambo ambalo linaonekana ni kama la jinai. Jinai ya nafsi inafahamika kuwa ni uadui kwa mwanadamu kwa kutoa roho yake, au kuviharibu baadhi ya viungo vyake, au kumsababishia jeraha mwilini mwake.

Ni haramu kuitoa roho ya mwanadamu bila ya haki au kukiharibu kiungo miongoni mwa viungo vyake au kusababisha madhara yoyote kwa mwili wake. Hakuna kosa kubwa mno baada ya shirki na ukafiri zaidi ya kumuua Muislamu. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): “Na mwenye kumuua Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahanamu humo atadumu, na Allaah Amemkasirikia, na Amemlaani, na Amemuandalia adhabu kubwa” (4: 93).

Kumwaga damu ya mwanadamu mwengine hata asiyekuwa Muislamu haifai pasi na haki, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Kwa sababu ya hayo Tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliyemuua mtu bila ya yeye kuua, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote” (5: 32).

Na kauli yake (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam): “Kosa la kwanza kuhukumiwa siku ya Qiyaama litahusu damu” (al-Bukhaariy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na al-Haakim).

 Wanachuoni na mafakihi wote wameigawa jinai katika sehemu tatu. Nazo ni kama zifuatazo:

  1. Al-‘Amd (Kusudi): Maana yake ni kuwa mtu anakusudia kumuua Muumini au kumdhuru akampiga kwa chuma au fimbo au kumlisha sumu akafa kwa sumu hiyo au kutumia ala yoyote ambayo kwa kawaida inaua. Na hukumu ya hii jinai, itampasa mtu kisasi kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): “Na humo Tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho, na jicho kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa majaraha kisasi. Lakini atakaye samehe basi itakuwa ni kafara kwake” (5: 45). Na kauli ya Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam): “Mwenye kuuliwa na mtu wake au kujeruhiwa ana khiyari kufanya moja ya matatu: Ima kisasi au diya au asamehe” (Ahmad, Abu Daawuud na Ibn Maajah).

Huyu anawajibika mambo yafuatayo:

-         Anapata dhambi.

-         Hatokuwa mwenye kurithi.

-         Anafaa atoe kafara.

-         Atoe diya au apate msamaha.

  1. Shibhul ‘Amd (Baina ya Makusudi na Bahati Mbaya): Hii ni mtu amekusudia jinai chini ya kuua au kujeruhi. Hii ni kutumia ala ambayo kwa kawaida haiui, hivyo mhalifu amekusudia kumpiga mwenziwe lakini sio kuua. Mfano ni kumpiga mtu ngumi au kichwa au ukulele usoni mwake au akamtisha na akafa kwa hilo. Hukumu ya jinai ya aina hii ni diya-fidia itakayotolewa na ndugu wa muuaji na muuaji mwenyewe afanye kafara, kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka: “Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipokuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka” (4: 92). Na asiyeweza kumkomboa mtumwa basi, “Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Allaah” (4: 92).

Huyu naye anakuwa:

-         Mwenye kupata dhambi kwani ameua nafsi iliyo haramu.

-         Diya nzito.

Mwenye kuua kwa shibhul ‘Amd ima kwa fimbo au kijiwe anafaa atoe fidia ya ngamia mia moja, arobaini miongoni mwao wakiwa na mimba” (Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

  1. Al-Khatwa-a (Bahati Mbaya): Hii ni kwa Muislamu kufanya linaloruhusiwa kisheria kama vile kulenga shabaha au kuwinda au kukata nyama silaha ikaanguka na mtu akafa. Hukumu ya aina hii ya jinai ni sawa na hukumu ya pili isipokuwa diya-fidia yake inakuwa nyepesi na mwenye kufanya kosa hili hana dhambi tofauti na ile ya pili kwani aina ile diya inakuwa nzito na mfanya kosa hilo ana dhambi. Zipo aina mbili nazo ni: (i) Anatoa kafara kwa aliyeua na diya kutoka kwa watu wake, nayo ni kumuua Muumini katika safu isiyokuwa ya makafiri au kaumu ambayo tuna mapatano nayo. (ii) Aina hii, wajibu ni wa diya tu, nayo ni kumuua Muumini katika safu ya makafiri akidhania ni kafiri.

Kifo cha watu kula chakula inakuwa ni bahati mbaya kwani mke hakukusudia hilo kabisa. Katika hilo linaweza kuja swali: Je aliyenunua chakula ni nani? Mara nyingi inawezekana kuwa ni mume mwenyewe au mtumishi, kazi ya mke ilikuwa ni kupika tu chakula kile alichotaka mume au alichoamua yeye mwenyewe. Kwa hiyo, mke huyu atarithi wala hatawajibika kafara yoyote.

Mbali na kusema hayo tungependa kujua kulikuwa na uhusiano gani baina ye mke na aliyefariki. Je, uhusiano wake ulikuwa mzuri au hawakuwa ni wenye uhusiano mwema?

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share