Mambo 10 Yanayomtoa Mtu Katika Uislam

 

BismiLlaahi Rahmaani Rahiim

 

 Mambo Yanayomtoa Mtu Katika Uislaam

 

Muhammad  Bin 'Abdil-Wahhaab Sulaymaan At-Tamiymiy

 

Alhidaaya.com

 

 

Jua ya kwamba mambo yanayomtoa Muislamu katika Uislamu ni mambo kumi:

 

Moja: Ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka katika ibada, Anasema Allaah:

 

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]

 

Na Anasema Allaah:

 ۖإِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah: 72]

 

na miongoni mwa hizo shirki ni kuchinja kwa asiyekuwa Allaah kama anayechinja kwa ajili ya majini au makaburi.

 

Pili: Mwenye kufanya baina yake na Allaah viunganishi akawa anaviomba viunganishi hivyo na kuvitaka uombezi na kuvitegemea, basi hakika mtu huyo amekufuru kwa makubaliano ya wanavyuoni.

 

Tatu: Asiyewakufurisha washirikina au akawa ana shaka katika ukafiri wao au akaupitisha (akausahihisha) ukafiri wao amekufuru.

 

Nne: Mwenye kuamini kwamba muongozo wa asiyekuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio muongozo ulio kamili kuliko muongozo wa Nabiy au ya kwamba hukmu ya mwengine ni bora kuliko hukmu yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama yule anayefadhilisha hukmu za Matwaghuut kuliko hukmu yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi mtu huyo ni kafiri.

 

Tano: Mwenye kuchukia chochote katika aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akatekeleza amekufuru.

 

Sita: Mwenye kufanyia mzaha (shere) kwa chochote katika dini ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au akafanya utani katika thawabu au katika adhabu za Allaah amekufuru. Na dalili ni neno Lake Allaah:

 

ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli     Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” [At-Tawbah: 65-66]

 

Saba: Uchawi; na miongoni mwa huo uchawi ni  uchawi  wa kutenganisha na kupendanisha basi yeyote mwenye kufanya huo uchawi au akauridhia amekufuru. Anasema Allaah:

 

 ۚوَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ

Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.  [Al-Baqarah: 102]

 

Nane: Kusaidiana na kuwa pamoja na washirikina dhidi ya Waislamu, na dalili ni:

 

 وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Maaidah: 51]

 

Tisa: Mwenye kuamini ya kwamba baadhi ya watu wanaweza kutoka katika shari’ah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama vile alivyoweza kutoka Al-Khidhr katika shari’ah ya Muwsaa basi mtu hiyo ni kafiri.

 

Kumi: Kuikataa na kuipa mgongo dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na akawa hajifunzi chochote katika dini. Na dalili ni neno Lake Allaah:

 

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا ۚ إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ

Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayaat za Rabb wake, kisha akazikengeukia? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu. [As-Sajdah: 22]

 

Na wala hakuna tofauti katika mambo haya yanayomtoa Muislamu katika Uislamu kwa yule anayefanya utani au anayefanya kwa kweli au anayeogopa ila anayetenzwa nguvu (kama kushikiwa silaha na akalizimishwa kufanya mambo hayo). Na yote hayo tuliyoyataja ni katika mambo makubwa yanayohatarisha na yanayotokea sana, kwa hivyo yapaswa kwa Muislamu kujihadhari nayo na ayaogope kwa nafsi yake.

 

Twajilinda kwa Allaah kwa hasira Zake na adhabu Zake kali na Rahma na Amani zimfikie kiumbe bora Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake na Swahaba wake wote.

 

Share