Skip navigation.
Home kabah

Jini, Shaytwaan Na Mchawi

 

Imekusanywa Na Muhammad Faraj

 

 

Yaliyomo

 

JINA LAKE.. 2

IMANI JUU YA GHAIBU.. 2

USHAHIDI WA KUWEPO MAJINI KATIKA QUR-AAN TUKUFU.. 2

USHAHIDI WA KUWEPO KWA MAJINI KATIKA MAFUNDISHO YA MTU (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) 'SUNNAH' 3

DALILI KATIKA QUR-AAN KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO.. 4

DALILI KATIKA MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA LLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM)

KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO   4

MAJINI WANAZALIANA.. 4

WAMEUMBWA KABLA YA BINADAMU

UHUSIANO BAINA YA JINNI NA SHETANI. 5

IBILISI NI KATIKA MALAIKA?. 6

AINA ZA MAJINI. 7

MWAHALI WANAPOISHI. 7

WANAKULA NA KUNYWA.. 7

WANA UWEZO WA KUJIGEUZA.. 8

WAMO MIONGONI MWAO WANAWAKE NA WANAUME.. 9 WANAOWA ?. 10

MAJINI WANAKUFA?. 10

WAMO MIONGONI MWAO WAISLAMU NA MAKAFIRI. 11

WAISLAMU KATIKA MAJINI WATAINGIA PEPONI?. 11

MAJINI WANAWAOGOPA WANADAMU.. 12

KUWEZA KWA MAJINI KUSIKIA HABARI ZA MBINGUNI. 13

UCHAWI. 13

NINI MAANA YA UCHAWI?. 13

VIPI UTAWEZA KUMJUA MCHAWI. 16

DALILI KUWA UCHAWI UPO, KUTOKA KATIKA QUR-AAN NA KATIKA SUNNAH (MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA LLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM)

SOMA BAHATI YAKO (NYOTA YAKO) LUCKY STARS.. 18

UCHAWI UMEANZA ZAMA ZA NABII SULAYMAAN?. 19

UCHAWI NI KUFRU.. 19

HUKUMU YA UCHAWI KATIKA DINI YA KIISLAMU.. 21

KUJIKINGA NA SHARI ZA WACHAWI NA MAJINI WAO.. 22

DUA ZINAMKUMBA SHETANI. 24

DHIKRU ALLAAH.. 24

USIINGIZE NDANI YA NYUMBA YAKO VIFUATAVYO

 

 

JINA LAKE

Ameitwa JINNI kwa sababu ya kutokuonekana kwake na watu, na hii ni kwa sababu kila kisichoonekana kwa jicho la binadamu katika lugha ya kiarabu jina lake hutokana (hutoholewa) na herufi mbili hizi; (Jiym) na (Nuun).

Kwa mfano; 'Bustani' huitwa 'janna' kwa sababu ya kuzungukwa kwake na majani kila upande pasiweze kuonekana ndani. Elimu ya uzazi huitwa 'Ilmul ajinna', kwa sababu ya kutokuonekana kwa kile kilichokuwemo tumboni mwa mzazi. Hata mwendawazimu naye huitwa 'majinun' kwa sababu ya kutoweka kwa akili yake. Na Majinni nao wamepewa jina hilo kwa sababu ya kutokuonekana kwao kwa macho ya binadamu.

Ukichunguza utaona kuwa maneno yote hayo; 'Janna, ajinna, majinun, jinni', yana herufi ya 'Jiym na Nuun' ndani yake.

 

IMANI JUU YA GHAIBU

Kuamini juu ya ghaibu (yasiyoonekana) ni katika misingi ya itikadi ya Dini.

MwenyeziMungu Anasema:

"ALIF LAAM MYM. Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake.Ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu. Ambao huyaamini yasiyoonekana (maadam yamesemwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake) na husimamisha Sala na hutoa katika yale Tuliyowapa".

Al Baqarah

 

Katika aya hizi, MwenyeziMungu ametaja baadhi ya sifa za wacha Mungu ikiwemo ikiwemo sifa hii ya kuamini Ghaibu.

Na maana ya neno 'Ghaibu', ni yale tusiyoweza kuyaona tuliyofundishwa na MwenyeziMungu Subhaanahu waTaala au Mtume Wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

USHAHIDI WA KUWEPO MAJINI KATIKA QUR-AAN TUKUFU

Katika Qur-aan MwenyeziMungu Anasema:

"Na (wakumbushe) tulipokuletea kundi la majini (kuja kwako) kusikiliza Qur-aan."

Al Ahqaf  - 29

 

Na Akasema:

"(Siku ya Qiyaamah wataambiwa) “Enyi makundi ya majini na wanaadamu! Je, hawajakufikieni Mitume miongoni mwenu kukubainishieni Aya zangu?"

Al An am 130

 

USHAHIDI WA KUWEPO KWA MAJINI KATIKA MAFUNDISHO YA MTU (SWALLA LLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM) 'SUNNAH'

 

Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wameelezea Maimam Bukhari na Muslim katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni Abbas (Radhiya Llaahu anhu) amesema:

"Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu:

"Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni".

Wenziwao wakasema:

"Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni.”

Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, waislamu walikuwa wakiswali Swala ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema:

"Hii (Qur-aan) wallahi, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni."

Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia;

"Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu"

Mwenyezi Mungu Amesema katika Suratul Jinn aya ya mwanzo:

"Sema:“Imefunuliwa kwangu kuwa kundi moja la majini lilisikia (Qur-aan) likasema; “Hakika tumesikia Qur-aan ya ajabu.”

Suratul Jinn - 1

 

Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme nk. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.

 

DALILI KATIKA QUR-AAN KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO

Ndani ya Qur-aan mna dalili nyingi zinazotujulisha kuwa Jinni ameumbwa kwa moto, na tutazitaja baadhi ya dalili hizo:

MwenyeziMungu Amesema:

"Akasema (Ibilisi); Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo".

Al Aaraf -12

Na Akasema:

"Na akawaumba Majinni kwa ulimi wa moto".

Ar Rahman _ 12

 

DALILI KATIKA MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA LLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM) KUWA JINNI AMEUMBWA KWA MOTO

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametujulisha pia kuwa Majini wameumbwa kwa moto, na tutataja baadhi ya kauli zake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam);

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Wameumbwa Malaika kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na  Adam ameumbwa kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)."

Muslim

 

MAJINI WANAZALIANA 

MwenyeziMungu Anasema:

"Je! Mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa marafiki (zenu) badala yangu hali wao ni maadui zenu? Ni mbaya kabisa kwa madhalimu badala (hii)".

Al Kahf - 50

 

Kauli ya MwenyeziMungu katika aya hii pale aliposema 'NA KIZAZI CHAKE'. inamaanisha kwamba majini wanazaliana.

 

WAMEUMBWA KABLA YA BINADAMU

MwenyeziMungu Anasema:

"Na tulimuumba mwanadamu kwa udongo mkavu unaotoa sauti (unapogongwa), unaotokana na matope meusi yaliyovunda.

Na majini tuliwaumba KABLA, kwa moto wa upepo wenye joto (kubwa kabisa)."

AlHijr- 26-27

 

Kwa hivyo majini waliumbwa kabla yetu na waliishi katika ardhi hii hata kabla ya kuumbwa kwa Adam (Alayhis salaam), na hii ndiyo maana Mwenyezi Mungu alipowaarifu Malaika kuwa anataka kuumba viumbe katika ardhi wakasema:

"Utaweka watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu."

AlBaqarah - 30

 

Malaika waliuliza suala hili si kwa ajili ya kupinga amri ya MwenyeziMungu au kwa kumuonea wivu mwanadamu, bali waliuliza kwa ajili ya kutaka kuijua hekima ya kuumbwa viumbe hawa, na hii ni kwa sababu walielewa kutokana na viumbe vilivyotangulia vilivyoishi ardhini, kwamba vina sifa ya ufisadi na umwagaji wa damu.

Anasema Ibni Kathiyr (huyu ni katika maulamaa na mfasiri mkubwa wa Qur-aan) kwamba kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, Majinni na viumbe wasiokuwa wanadamu walikuwa wakiishi ardhini na kwamba walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa pamoja na umwagaji wa damu.

Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

"Majinni waliishi ardhini kabla ya wanaadamu na walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa na MwenyeziMungu akawaondoa na kuwaleta wanadamu."

Maneno kama haya pia yalisemwa na Hassan AlBasry (Radhiya Llaahu ‘anhu), na akaongeza kusema:

"Hii ndiyo maana Malaika wakamuuliza Mola wao suali hilo."

 

 

UHUSIANO BAINA YA JINNI NA SHETANI

Shetani na Jinni asili yao ni moja, hapana hitilafu baina ya maulamaa kuhusu jambo hili, isipokuwa wamekhitalafiana katika suala; “Je Ibilisi ndiye baba wa Majinni (asili yao)  mfano wa Adam  ambaye ni baba yetu na asili yetu ?)”

Majibu;

Iblisi si asili yao, bali yeye ni miongoni mwao.

MweyeziMungu Anasema:

"Basi wakamsujudia isipokuwa Iblisi; yeye alikuwa miongoni mwa majini."

Al Kahf -50

 

Kwa vile Mwenyezi Mungu Amemtaja Iblisi kuwa ni MIONGONI mwa majini, kwa hivyo yeye ni mmoja wao na si asili yao kama mfano wa Adam (Alayhis salaam) alivyokuwa asili ya wanadamu.

 

Tulisema kuwa wameitwa 'Majinni ' kwa sababu ya kutokuonekana kwao na sisi tumeitwa 'Insan' kwa sababu ya kusahau kwetu, kwani neno 'Insan', asili yake linatokana na neno 'Nisiyan', na maana yake ni Kusahau.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Adam alisahau na vizazi vyake vikasahau."

Ama neno 'Shetani', katika lugha ya kiarabu maana yake ni 'Kila anayeasi na kupinga au kuzuwia au kushawishi viumbe wasiifuate njia ya MwenyeziMungu', awe Jinni au Mwanadamu.

MwenyeziMungu Anasema:

"Na nama hii tumemfanyia kila Nabii maadui (nao ni) mashetani katika watu na (mashetani katika) majini. Baadhi yao wanawafunulia wenziwao maneno ya kupambapamba ili kuwadanganya."

Al An am 112

 

IBILISI NI KATIKA MALAIKA?

Iblisi si katika Malaika, bali ni miongoni mwa Majinni kutokana na dalili zifuatazo:

MwenyeziMungu Anasema:

"Basi wakamsujudia isipokuwa Iblisi; yeye alikuwa miongoni mwa majini."

Al Kahf -50

 

Na Akasema:

"Hawamuasi MwenyeziMungu kwa amri zake; na wanatenda wanavyoamrishwa (yote)."

AtTahrym - 6

 

Kutokana na aya hii, tunapata ushahidi mwingine kuwa; Malaika hawamuasi Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo Ibilisi angelikuwa Malaika, asingemuasi Mola wake bali angetenda kama alivyoamrishwa. Lakini yeye alitenda kinyume na hivo. Alimuasi MwenyeziMungu pale alipokataa kumsujudia baba yetu Adam (Alayhis salaam), akasema:

"Akasema (Ibilisi)‘; 'Mimi ni bora kuliko yeye  (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo."

Al Aaraf - 12

 

Na hapa pia tunapata ushahidi mwingi pia kuwa Iblisi si miongoni mwa Malaika, kwani Malaika wameumbwa kwa Nuru na Mashetani wameumbwa kwa moto.

Katika aya iliyotangulia Iblisi alisema:

'Mimi ni bora kuliko yeye (Mimi) umeniumba kwa moto."

Angelikuwa yeye ni miongoni mwa Malaika angelisema;

 “Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa Nuru".

 

Kwa sababu Malaika wameumbwa kwa Nuru kama alivyosema Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) katika hadithi iliyotangulia:

"Malaika wameumbwa kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na Adam (ameumbwa) kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)."

Muslim na Ahmad bin Hanbal

 

 

AINA ZA MAJINI

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Majini (wako) namna tatu, namna moja wana mabawa wanaruka na namna (nyengine) majoka na n’ge na namna nyengine hawaishi mahala pamoja na hupenda kuhama."

Al Tabarani na Al Hakim na Al Bayhaqi na imesahihishwa na Sh. Al Albani

 

MAHALI WANAPOISHI

Majini wanaishi katika majangwa na katika sehemu za kutupa taka, kwa sababu wao wanakula mabaki ya vyakula vya binadamu.

Zimepokelewa hadithi nyingi pia kwa njia ya Ibni Abbas na Ibni Masaood (Radhiya Llaahu ‘anhum) kwamba Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akienda jangwani na kuwasemesha Majinni na kuwalingania katika dini ya Kiislamu na kuwataka wamuabudu MwenyeziMungu mmoja wa kweli.

Majinni wanapenda pia kuishi vyooni, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha dua ya kusoma kabla ya mtu kuigia chooni, akasema:

Mmoja wenu anapoingia chooni basi aseme;

"ALlaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith."

Na maana yake;

“MwenyeziMungu najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake.”

Bukhari na Muslim.

 

Majini pia wanaishi katika Mashimo:

Kutoka kwa Qatada kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Mmoja wenu asikojowe ndani ya shimo."

Na alipoiulizwa kuna ubaya gani mtu kukojoa ndani ya shimo akasema:

"Inasemekana kuwa Majinni wanapenda kuishi humo."

Annasaiy

 

WANAKULA NA KUNYWA

 

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Mmoja wenu anapokula, basi ale kwa (mkono wa) kulia na anapokunywa anywe kwa (mkono wa) kulia, kwa sababu shetani anakula kwa kushoto na kunywa kwa kushoto."

Muslim

 

Na akasema:

"Mtu anapoingia nyumbani akasema; 'Bismillah', na anapokula (akasema Bismillah), shetani husema; 'Hatuna makazi humu (ndani ya nyumba hii), na hatuna chakula cha usiku'. Ama anapoingia asiseme; 'Bismillah', shetani husema; 'Tumepata makazi humu', na asiposema Bismillah pale anapokula, basi (shetani) husema; 'Tumepata makazi na chakula".

Muslim

 

WANA UWEZO WA KUJIGEUZA

Kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda (chakula cha) zaka ya Ramadhani, akaja mtu akawa anaiba katika chakula kile, nikamkamata na kumuambia kwamba nitampeleka kwa Mtume wa MwenyeziMungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), akasema: 'Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi na shida nyingi."

Anasema (AbuHuraira (Radhiya Llaahu ‘anhu):

"Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:

“Ewe Abu Huraira umefanya nini na mfungwa wako jana?"

"Akasema:

 "Nikamwambia:

"Ewe Mtume wa MwenyeziMungu, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Ama huyu amekudanganya na atarudi.”

Nikajuwa kwamba atarudi kwa sababu Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema hivyo. Nikamtegea, akaja tena siku ya pili kuiba chakula, nikamkamata, nikamuambia nitakupeleka kwa Mtume wa MwenyeziMungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Akaniambia:

“Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi sitorudia tena.”

Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Ewe Abu Huraira umefanya nini na mfungwa wako jana?”

Nikamuambia:

"Ewe Mtume wa MwenyeziMungu, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

 "Ama huyu amekudanganya na atarudi."

Nikamkamata mara ya tatu akiwa anaiba (tena) chakula, nikamuambia:

"Nitakupeleka kwa Mtume wa MwenyeziMungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na hii ni mara ya tatu na kila mara unasema hutorudia kisha unarudia."

Akasema:

"Niache nikufundishe maneno MwenyeziMungu atakufaa nayo."

Nikamuuliza;

“Maneno gani hayo?"

Akasema:

“Unapokuwa juu ya tandilo lako soma Ayatul Kursy - ALlaahu laa ilaaha illa huwal hayyul qayuum - mpaka mwisho na itaendelea kukuhifadhi aya hii na hatokukaribia shetani mpaka utakapoamka.”

Nikamuacha aende zake.

Asubuhi yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:

“Amefanyaje mfungwa wako jana?”

Nikamuambia:

"Ewe Mtume wa MwenyeziMungu amejidai eti amenifundisha maneno ambayo MwenyeziMungu Atanifaa nayo, basi nikamuacha huru."

Akaniuliza;

“Ni maneno gani hayo?”

Nikasema:

"Ameniambia:

“Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Ayatul Kursy mpaka mwisho na MwenyeziMungu ataendelea kukuhifadhi nayo na hatokukaribia shetani mpaka utakapoamka."

 Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

"Ama yeye amesema kweli ingawaje ni muongo. Unamjua nani uliyekuwa ukizungumza naye siku tatu hizi ewe Aba Huraira?"

Nikajibu:

"La simjuwi".

Akasema:

“Yule ni shetani.”

Bukhari

 

Kwa vile shetani huyu aliyekuwa akiiba alikuwa akimjia Abu Huraira (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwa sura ya binadamu, basi hii ni dalili kwamba majini wanao uwezo wa kujibadilisha umbile lao.

 

 

WAMO MIONGONI MWAO WANAWAKE NA WANAUME

Katika hadithi niliyoitaja hapo juu Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

"Anapoingia mmoja wenu chooni, basi aseme:

“MwenyeziMungu najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake

Bukhari na Muslim

 

WANAOWA?

Majini wanaoana na kuzaliana, na ushahidi umo ndani Qur-aan katika kauli Yake Subhanahu wa Taala Aliposema:

"Je! Mnamfanya yeye (Ibilisi) na kizazi chake kuwa marafiki (zenu) badala yangu hali wao ni maadui zenu? Ni mbaya kabisa kwa madhalimu badala (hii)."

Al Kahaf - 50

 

Hata hivyo Maulamaa wengi hawakubali majini waowane na wanadamu.

Pana kisa cha mwanamke mmoja kutoka Yemen alikuwa akidai kwamba anajiwa na jinni na kwamba jinni huyo anataka kumuowa. Alipoulizwa Imam Malik kuhusu jambo hili akasema:

“Sioni kifungu chochote cha sheria kinachoharamisha, isipokuwa nakuogopeeni fitna (Mitihani).”

 

Maulamaa wamesema kuwa kauli ya Imam Malik hii inatujulisha juu ya hofu yake, kwani mwanamke yeyote anaweza kujipatia mimba kwa njia zisizo za halali, kisha akasema kwamba ameolewa na jinni na kwa njia hii uhuni utazidi na fitna zitaenea.

Maulamaa wengine wamekataa kabisa fikra ya kuoana baina ya majini na wanadamu wakiegemea kauli ya MwenyeziMungu Isemayo:

"Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mupate utulivu kwao."

ArRum - 21

 

Na Akasema:

"Na MwenyeziMungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto na wajukuu."

AnNahl - 72

 

Katika aya hizi MwenyeziMungu anatufahamisha kwamba ametuumbia wake zetu katika jinsi yetu, wakati Majinni si katika Jinsi yetu.

Na akasema; Ili mupate utulivu kwao", wakati mwanadamu hawezi kupata utulivu kwa jinni, maana siku zote mtu hupata utulivu kwa kiumbe aliye mfano wake na majini si mfano wetu.

 

MAJINI WANAKUFA?

MwenyeziMungu Anasema:

"Kila kilichopo juu yake (ardhi na mbingu) kitatoweka (kitaondoka)."

Arrahman - 26

Na Akasema:

"Hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye; kila kitu kitakufa isipokuwa Yeye (MwenyeziMungu basi)."

Al Qasas - 88

 

Inavyojulikana ni kwamba Iblisi yuhai mpaka siku ya Qiyaamah.

MwenyeziMungu Amesema:

"Akasema (Iblisi); “Mola wangu! basi nipe nafasi (nisife) mpaka siku watakayofufuliwa (viumbe) vyote.”

Akasema (Mwenyezi Mungu); “Hakika wewe (nimekwisha kukufanya) katika wale waliopewa nafasi.

Mpaka siku ya wakati uliowekwa (ukifika wakati huo utakufa).”

AlHjr - 36 -37-38

 

Kwa hivyo Ibilisi ataishi mpaka siku maalum anayoijua MwenyeziMungu peke yake kisha atakufa, na majini nao pia wanazaliana na wanakufa kama sisi.

 

 

WAMO MIONGONI MWAO WAISLAMU NA MAKAFIRI

MwenyeziMungu Amesema:

"Nasi wamo miongoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu wanaokengeuka. Waliosilimu hao ndio waliotafuta uwongofu."

AlJinn - 14

 

Na Akasema:

"Na hakika katika sisi wamo walio wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tumekuwa njia mbali mbali."

AlJinn -11

 

Katika kuifasiri aya hii, anasema Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu):

"Kauli ya MwenyeziMungu;“Tumekuwa njia mbali mbali”, maana yake ni “Makafiri na Waislamu”.

Baadhi ya maulamaa wanasema:

"Dini mbali mbali na madhehebu mbali mbali."

 

 

WAISLAMU KATIKA MAJINI WATAINGIA PEPONI?

Katika tafsiri yake Ibni Kathyir amesema:

"Waislamu miongoni mwa Majini wataingia Peponi kama Waislamu katika wanadamu "Na dalili yake pamoja na dalili za maulamaa wengine ni kauli ya MwenyeziMungu akitujulisha juu ya hali ya wanawake wa Peponi Aliposema:

"Hajawagusa binadamu yoyote kabla yao (hao waume zao) wala jinni."

ArRAhman 74

 

Na Aliposema:

"Na Mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake atapata mabustani (Pepo) mawili. Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)?"

Ar Rahman - 46-47

MwenyeziMungu Amejaalia jazaa ya majini na binadamu wema kuwa ni pepo, na majini waliijibu aya hii kwa kumshukuru MwenyeziMungu  wakasema:

"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."

 

Hii ni hadithi iliyosimuliwa na Imam Attirmidhy kutoka kwa Jabir (Radhiya Llaahu anhu)  kwamba amesema:

"Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliisoma SutratuRahman mpaka mwisho kisha akasema: ‘Mbona mumenyamaza kimya, Majini wamekuwa bora kuliko nyinyi kwa kujibu kila ninapowasomea aya hii:

"Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)?"

Wao huijibu kwa kusema:

"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."

Imesimuliwa na Attirmidhy na Al Bazaar na AlHakim na pia Ibni Jaryr na Sheikh Al Albani amesema kwamba hadithi hii ni njema.

 

Dalili inayopatikana kutoka katika aya hizi ni kwamba;  Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)  alikuwa akiwapa Majini mafundisho ya Dini , na kuwafahamisha kwamba pana jaza ya Pepo kwa Mwenye kuogopa.

Kama Majini hawatoingia Peponi hapangekuwa na haja ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwatokea na kuwapa mafunzo ya dini na kuwajulisha juu ya Pepo inayowangoja wale wanaomuogopa MwenyeziMungu.

 

 

MAJINI WANAWAOGOPA WANADAMU

Ameeleze Ibn Abi Al Dunya kwamba Mujahid amesema:

‘Usiku mmoja nilikuwa nikiswali akanitokea mfano wa mtoto mdogo mbele yangu nikamshika kwa nguvu zangu zote akainuka na kuuruka ukuta hata nilisikia kishindo cha kuanguka kwake.’  Akaendela kusema: ‘Wao (majini) wanakuogopeni kama nyinyi mnavyowaogopa."

Imepokelewa kutoka kwa Mujahid kuwa alisema:

‘Shetani anakuogopeni kuliko nyinyi mnavyomuogopa akikukaribia usimregezee akakupanda, bali shindana naye na hatimae ataondoka."

 

KUWEZA KWA MAJINI KUSIKIA HABARI ZA MBINGUNI

Imepokelewa kutoka kwa Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwamba alisema:

‘Amenihadithia mmoja katika masahaba wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa, usiku mmoja walipokuwa wamekaa pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) nyota moja ikaanguka na kun’gara. Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:

"Mlikuwa mkisemaje wakati wa ujahilia (kabla ya kuja Uislamu?"

Wakajibu:

"Tulikuwa tukisema; Usiku wa leo amezaliwa mtu mtukufu na amekufa mtu mtukufu."

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:

"Bali haiangushwi nyota kwa ajili ya kifo cha mtu wala kwa kuzaliwa kwa mtu, lakini Mola wetu Aliyetukuka anapotoa amri, Malaika wabebao Arshi husabbih (husema Subhana llah), na viumbe vya mbinguni vyote humsabihi MwenyeziMungu pia, kisha husabihi viumbe wa mbingu za chini mpaka habari inapofika katika mbingu ya dunia, majini huzipata habari hizo na huwatupia mabwana zao nazo ni habari za kweli, lakini wao huongeza habari za uongo juu yake.”

Kutokana na Bibi Aisha (Radhiya Llaahu ‘anha), amesema:

"Niliuliza:

"Ewe Mtume wa MwenyeziMungu, makuhani walikuwa wakituelezea baadhi ya mambo na yalikuwa ni ya kweli."

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

"Hiyo ni habari ya kweli ameipokea jini akamtupia bwana wake na kuongezea uongo mara Mia."

Imetolewa na Maimam Bukhari na Muslim na Ahmad na AlBayhaqiy

 

 

UCHAWI

 

NINI MAANA YA UCHAWI?

Al Azhari ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya kiarabu iitwayo “LisanulArab” amesema:

“Neno “Uchawi”, kwa kiarabu “As Sihr”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na shetani na kwa msaada wake (shetani)”, na akasema pia kuwa; “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli.”

Ama Sahaba Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

"Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki."

Hayo ni katika kamusi za lugha.

 

Amma katika kamusi ya dini, maana ya neno Uchawi (As Sihr), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Al Razi kuwa;

"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)."

Amma Sheikh Wahiyd Abdulsalaam Bali, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'Al Saarim Al Batar fiy muhaarabat Al Saharatul ashraar', na kitabu kiitwacho "Al wiqaya mina l jinni wa shaytan", ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika elimu ya majini na mashetani na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:

"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kwa kila anachotaka."

 

Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na shetani ayatende ili ajikurubishe naye ni:

 Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni

 Aandike baadhi ya aya za Qur-aan kwa damu ya hedhi.

 Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aya za Qur-aan penye nyayo za miguu.

 Au aiandike suratulFatiha kinyume nyume.

 Asali bila ya Udhuu.

 Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la MwenyeziMungu kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na shetani.

 Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia.

 Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake

 

Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama.

Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajji akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji.

Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy.

Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi ende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.

Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa akenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.

Yule kijana alistuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia:

"Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?"

"Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."

Yule kijana akajibu:

"Mimi ninamsujudia Mwenyezi Mungu peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia."

Ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jini yule.

 

Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake atumikiwe kwa kutendewa matendo ya kufru, na maulamaa wanasema:

"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi shetani humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majini au kwa kiarabu wanaitwa "Maradatul Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi, na kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi."

Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na shetani ni marafiki na washirika katika kumuasi MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu Anasema:

"Na (wakumbushe) siku atakapowakusanya wote (akawaambia): "Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu". Na marafiki wao katika wanaadamu (watagombania) waseme:  "Mola wetu! Tulinufaishana sisi na wao na tumefikia muda wetu uliotuwekea". Basi (Mungu) atasema; "Moto ndio makazi yenu, mtakaa humo milele", ila apende MwenyeziMungu (kuwarehemu), hakika Mola wako ndiye Mwenye hikima (na) ndiye ajuaye.”

Al An - Am - 128

 

 

VIPI UTAWEZA KUMJUA MCHAWI

Zifuatazo ni dalili zitazokuwezesha kutofautisha baina ya mganga na mchawi. Utakapoona mojawapo ya dalili zufuatazo utambuwe kuwa huyo ni mchawi bila shaka yeyote na wala si shekhe au mganga:-

 Mchawi huuliza jina la mgonjwa na jina la mama yake

 Huchukua baadhi ya vitu vya mgonjwa kama vile nguo za nje au za ndani au kitambaa cha kufutia jasho n.k.

 Hutaka mnyama mwenye sifa maalum au rangi maalum ili achinjwe na hapigiwi Bismillahi anapochinjwa

 Huandika hirizi

 Husema maneno yasiyojulikana

 Humtaka mgonjwa aepukane na watu muda maalum na akae katika chumba kisichofikiwa na juwa

 Mara nyengine humtaka mgonjwa asiguse maji muda wa siku arubaini hivi (anasema Sheikh Wahiyd Abdulsalaam Bali kwamba akikutaka ufanye hivyo ujue kwamba Jinni anayemtumikia mchawi huyo ni mkiristo)

 Humpa mgonjwa vitu ili avifukie ardhini

 Humpa mgonjwa karatasi aziunguze kisha ajifukize na moshi wake

 Mara nyengine humwambia mgonjwa jina lake na mji anaoishi

 Huandika maneno katika karatasi na kumwambia mgonjwa azichemshe na kunywa maji yake

UKIONA DALILI HIZI KWA MGANGA UMJUE HAPOHAPO KUWA NI MCHAWI NA UEPUKANE NAYE

 

Anasema Sheikh Wahiyd Abdulasalaam Bali:

"Ukiutizama uso wa mchawi utakiona kiza cha kufru kilivyotanda katika uso huo mfano wa mawingu meusi.”

Anaendelea kusema Sheikh huyo:

“Kwa wale wanaowajua wachawi, wanawaona siku zote wakiwa katika dhiki, shida, matatizo katika siha zao, matatizo na wake zao au watoto wao na siku zote hawana raha wala utulivu.”

MwenyeziMungu Anasema:

"Na hakika kulikuwa na wanaume miongoni mwa wanaadamu wakijikinga kwa wanaume miongoni mwa majini kwa hivyo wakawazidishia taklifu (taabu)."

AlJinn - 6

Na Anasema:

"Na atakayejiepusha na mawaidha yangu basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki."

Twa ha 124

 

 

DALILI KUWA UCHAWI UPO, KUTOKA KATIKA QUR-AAN NA KATIKA SUNNAH (MAFUNDISHO YA MTUME (SWALLA LLAAHU ‘ALAYHI WA SALLAM)

Katika Surat Yunus aya ya 77 MwenyeziMungu Anasema:

"Akasema Musa:"Mnasema (hivi) juu ya haki ilipokujieni, (kuwa) Huu ni uchawi? (Mbona umefaulu basi) Na wachawi hawafaulu."

 

Hii ni dalili kwamba uchawi upo na MwenyeziMungu anatufundisha katika aya hii kwamba uchawi haufaulu.

Na katika sutaul Falaq Akasema:

"Na (najikinga na) shari ya wale wanaopuliza mafundoni."

 

Katika kuifasiri aya hii, mmoja katika maulamaa wakubwa wa tafsiri ya Qur-aan Imam Al Qurtuby amesema:

"Maana ya neno "Naffaathaat", ni wachawi wanapopuliza katika nyuzi huku wakizipiga fundo.”

Na Ibni Kathiyr katika tafsiri yake akinukuu kutoka kwa Ikrimah na Mujahid na Al Hassan Al Basry (Radhiya Llaahu ‘anhum) amesema:

"Hawa wanaopuliza mafundoni ni wachawi, na MwenyeziMungu anatuamrisha tujiepushe na shari zao.”

 

Amma hadithi za Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zinazotufahamisha kwamba uchawi upo na kwamba uchawi ni katika madhambi makubwa sana, ni hizi zifuatazo:

 Kutoka kwa Abi Huraira (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Jieupusheni na (mambo) saba Yaangamizayo.'

 Wakasema:

'Ni yepi hayo ewe Mjumbe wa MwenyeziMungu?"

Akasema:

"Kumshirikisha MwenyeziMungu, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharimishwa na MwenyeziMungu ila kwa haki yake, kula riba, kula mali ya yatima, kurudi nyuma (kukimbia) katika vita vya Jihadi (huku ukiwaacha wenzio wanapigana), na kuwasingizia uwongo wanawake wema wasio na makosa."

Bukhari na Muslim

 

Ndugu yangu Muislamu, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema kuwa mambo hayo 'Yanayomuangamiza', maana yake ni kuwa yanamuangamiza mtu katika moto wa Jahannam.

Ukirudia kuisoma tena hadithi hiyo utaona kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ameutanguliza uchawi kabla ya dhambi ya kuuwa, ingawaje kuuwa ni dhambi kubwa sana, na MwenyeziMungu Anasema katika Suratu Nnisaa aya ya 93:

"Atakayemuuwa Muislamu kusudi, basi jaza yake ni Jahannam atakuwa humo milele na MwenyeziMungu Ataghadhibika naye na Atamlaani na amemtayarishia adhabu kubwa."

 

Juu ya ukubwa wa dhambi hiyo ya kuuwa, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ameipa uzito zaidi dhambi ya Uchawi kwa kuiweka nafasi ya pili baada ya Shirki na kabla ya dhambi ya kuuwa.

 

SOMA BAHATI YAKO (NYOTA YAKO) LUCKY STARS

Katika hadithi ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Dawood na Ibni Majah hadithi ambayo Sheikh Al Albani ameitaja kuwa ni "hadithi njema", na hadithi hii pia ni dalili kwamba elimu ya kutabiri kwa nyota ambayo huandikwa katika magazeti na watu hupenda kusoma kwa kutaka kujua bahati zao, kitendo hiki ni haramu na yeyote atakayesoma nyota yake, basi swala zake hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini, hii ikiwa anasoma na huku haziamini, amma akisoma na huku anaziamini, basi anaingia katika hukumu ya aliyemuendea mtabiri na kumuuliza jambo, na anakuwa amekwisha kufuru yote aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota (utabiri) amejifunza sehemu ya uchawi, akiongeza atakachoongeza (katika uchawi au nyota)."

 

Na hii ni kwa sababu wanaosoma elimu ya nyota (utabiri) wanaamini kwamba katika nyota wanaishi majini ambao ni masultani na wakuu, na wanaitakidi kuwa mambo yetu yote husababishwa na harakati za nyota hizo kila zinapotaharaki kutoka mahali kuelekea pengine. Kwa ajili hiyo wao huzingoja nyota hizo masaa mengi ya usiku ili wapate kuandika talasimu zao, na huku ni sawa na kuziabudu nyota hizo.

(Pana tofauti baina ya elimu ya anga za juu (Astronomy) ambayo haina ubaya wowote ndani yake, na elimu ya nyota (Astrology) - utabiri - ambayo ni haramu).

Ushahidi Mwengine unapatikana katika hadithi iliyosimuliwa na Umran bin Hussain (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyesema kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Hayuko pamoja nasi mwenye kuamini juu ya nukhsi (waarabu walikuwa wanapotaka kusafiri humrusha ndege na akielekea upande wa kulia basi husafiri, amma akielekea upande wa kushoto huamini ni ukorofi na kuivunja safari yake), na pia hayuko pamoja nasi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa, na atakayemuendea mtabiri na akamsadiki asemayo basi kesha kufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)."

Al Bazaar.

 

Katika hadithi hizi Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anatukataza tusiwaendee wachawi wala watabiri wa aina yoyote ile kwa kuwauliza juu ya jambo lolote lile, hata kama atajibadilisha na kujiita AlHajj Fulani au Sheikh Fulani au Maalim Fulani au Mganga Fulani na hii ni kutokana na kufru zao wanazozifanya kwa kuwasujudia majini na kuridhishana nao ili wawatumikie.

Na hii ni dalili kwamba uchawi upo, maana kama haupo, basi Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) asingetukataza kufanya kisichokuwepo.

Pia hadithi hizi zinatufahamisha kwamba mambo haya ni haramu na atakayeyatenda anakuwa amekwishayakanusha yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa sababu aliyokuja nayo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kwamba hapana aijuwae ghaibu isipokuwa MwenyeziMungu Subhaanahu wa Taala.

Hadithi ziko nyingi sana, lakini hizi pamoja na aya zilizotangulia zinatosha kuwa ni dalili kwamba yote hayo yametajwa katika Qur-aan na katika mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

 

 

UCHAWI UMEANZA ZAMA ZA NABII SULAYMAAN?

Wachawi wanaposoma talasimu zao huwadanganya watu kwa kuanza kusoma baadhi ya aya au sura ndogo ndogo za Qur-aan na kulitajataja jina la Nabii SULAYMAAN na utawasikia daima wanamnasibisha Mtume huyu (Alayhis salaam) na kufru zao hizo ili wajinga wanaowafuata wadhani kwamba hayo yamo katika dini.

Uchawi haujaanza zama za Nabii Sulaymaan kama wachawi wanavyozuwa na kumsingizia Nabii Huyu wa MwenyeziMungu, bali ulikuwepo kabla yake kwa miaka elfu nyingi.

Uchawi ulikuwepo tokea zama za Nabii Saleh (Alayhis salaam) aliyekuja kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka elfu nyingi.

MwenyeziMungu Anasema:

"Wakasema: (kumuambia Nabii Saleh); "Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa."

Ash Shuaraa - 153

 

 

UCHAWI NI KUFRU

Wachawi na wafuasi wao hupenda kumsingizia Nabii SULAYMAANi kwa kuinasibisha na kufru yao hiyo na Mtume huyu mtukufu ambaye MwenyeziMungu alimpa ufalme ambao hajaupata mwengine baada yake kwa kumpa uwezo wa kuwatiisha majini, upepo, na uwezo wa kujua lugha za wanyama n.k.

MwenyezMungu Anasema:

"Basi tukamtiishia upepo unaokwenda pole pole kwa amri yake, anakotaka kufika (unamfikisha).

Pia tukamtiishia mashetani, kila ajengaye na azamiaye (lulu).

Na wengine wafungwao minyororoni (wanapokhalifu amri zake).”

Swaad - 36-38

 

Katika tasfiri yake, Ibni Kathiyr amenukuu kauli ya Ibni Abbas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa amesema:

"Asif - alikuwa mwandishi wa Nabii Sulaymaan na alikuwa akilijuwa jina tukufu la MwenyeziMungu (Al ismul aadham), na alikuwa akiandika kila kitu katika daftari kwa amri ya Nabii Sulaymaan na kulificha daftari hilo chini ya kiti cha Nabii Sulaymaani. Alipofariki Nabii SULAYMAAN, majini wakayatoa maandishi hayo wakachanganya na kuandika baina ya kila mistari miwili uchawi na kufru yao, kisha wakawaambia watu wao kuwa hayo ndiyo maandishi ya Nabii Sulaymaan na ndiyo aliyokuwa akiyatenda, na Mayahudi wakayasadiki maneno hayo, wakawa wanamtangazia Nabii huyu kuwa ni mchawi.

Mpaka alipokuja Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuteremshiwa aya ya 102 katika Suratul Baqarah:

MwenyeziMungu Anasema:

"Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani (wakadai kuwa yalikuwa) katika ufalme wa (Nabii) Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru (Kwa sababu uchawi ni kufru) bali mashetani ndio waliokufuru wakiwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakiujua wenyewe tangu zamani) na (uchawi) ulioteremshwa kwa Malaika wawili Haruta na Maruta katika (mji wa) Babil (Babylon). Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie "Hakika sisi ni mtihani (wa kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru. "Wakajifunza kwao (mashetani) ambayo kwa mambo hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo) Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya MwenyeziMungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa.

Na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia (starehe za) nafsi zao (za Akhera). Laiti wangalijua, (hakika wasingefanya hivi)."

 

Anasema Sheikh Abdulla Saleh Al Farsy katika tafsiri yake kwamba Aya hii inaonyesha wazi kuwa:

Uchawi ni amali ya ukafiri

Mchawi hawezi kumdhuru mtu ila kwa idhini ya MwenyeziMungu

Mchawi mwenyewe anadhurika kwa uchawi wake

 

Katika aya hii MwenyeziMungu anatufahamisha pia kuwa uchawi ulikuwepo kabla ya Nabi Sulaymaan kwa miaka mingi, tokea zama za ustaarabu wa Babiloni walipoteremshwa Malaika wawili, Haruta na Maruta ili kuwaonyesha watu na kuwafahamisha nini uchawi, wapate kuujuwa mara watakapouona na wasiufuate, na hii ni kwa sababu uchawi ni kufru.

Watu waliacha kufuata nasaha za Malaika hao na wakajifunza yale ambayo yatawadhuru na wala hayatawafaa, ingawaje walikuwa wakijuwa kuwa aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera.

Wachawi mpaka hivi sasa wanajaribu kuunasibisha uchawi wao na Nabii Sulaymaan pamoja na Malaika hawa wawili.

Tatizo kubwa hupatikana pale wachawi wanapofanya uganga wao pale wanaposema maneno yao ya kichawi. Wao huchanganya maneno hayo na baadhi ya aya za Qur-aan na wanaofanyiwa uganga hudhania kwamba Qur-aan ndiyo inayosomwa na kwa ajili hiyo na kutokana na ujinga wao, huhadaika na kujiingiza nao katika shirki.

 

 

HUKUMU YA UCHAWI KATIKA DINI YA KIISLAMU

Anasema Imam Malik (Rahimahu Llah) katika kitabu chake AlMuwata:

"Mchawi anayefanya uchawi mwenyewe, hukumu yake ni kuuwawa, ama yule anayemuendea mchawi, huyo hauwawi."

 

Ibni Qudama naye anasema;

"Hukumu ya mchawi ni kuuawa."

 

Hukmu kama hizi pia zimepokelewa kutoka Masahaba mbali mbali kama vile Umar, Uthmaan, Ibni Umar na wengine (Radhiya Llaahu anhum).

 

Hukumu hii ya kuuwawa kwa mchawi pia ameitamka Imam Ahmed bin Hambal (Rahimahu Llah).

Na imepokelewa kutoka kwa masahaba mbali mbali kwamba Umar bin Al Khataab (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliwaandikia masahaba kuwaamrisha wamuuwe kila mchawi mwanamke au mwanamume. Anasema mmoja katika masahaba kwamba baada ya kupata maandishi hayo waliwakamata na kuwaua wachawi watatu."

Amma Imam Shafi (Rahimahu Llah), yeye anaona kuwa mchawi asiuliwe isipokuwa akikiri mwenyewe kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

Kutokana na yaliyotangulia infahamika kwamba Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhu) pamoja na maulamaa wengi wanaona kwamba hukumu ya mchawi ni kuuliwa, isipokuwa Imam Shafi (Rahimahu Llah), yeye anaona kuwa auliwe tu ikiwa mchawi huyo atakiri kwamba ameuwa kwa uchawi wake.

 

 

KUJIKINGA NA SHARI ZA WACHAWI NA MAJINI WAO

Zifuatazo ni baadhi ya Njia za kujikinga na waovu hao:

 

 

KUSAFISHA NIA

Ibilisi alipohukumiwa kupotea kwa sababu ya kuasi kwake, aliahidi kuwapoteza viumbe wote isipokuwa wale waliosafika kikweli.

Ibilisi akasema kumwambia MwenyeziMungu:

"Isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli."

 

Kusafisha nia (Al Ikhlas), maana yake ni kuzihusisha Ibada zote kwa moyo wote kwa ajili ya MwenyeziMungu peke yake, siyo kujionyesha mbele za watu kuwa ni Mcha Mungu na unapokuwa peke yako unamuasi.

Al Junaid, mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake amesema:

"MwenyeziMungu ana waja wake wenye akili, walipopata akili wakaifanyia kazi, walipofanya kazi wakaitakasa kazi hiyo na kule kuitakasa kwao kukawaingiza katika milango ya kheri yote."

 

KUTIA UDHU

Katika hadithi nyingi Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha juu ya umuhimu wa kubaki na udhu kila mtu anapoweza kwa ajili ya kupata thawabu na kwa ajili ya kujikinga na kila shari.

 

SWALA KATIKA JAMAA

KusWali sWala za jamaa msikitini, maana Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha kwamba mbwa mwitu (shetani) huwala kondoo wanaotembea mbali na wenzao.

 

SWALA ZA SUNNAH

Swala za Sunnah uziswali nyumbani, usiiache nyumba yako ikawa kama kaburi, na unaposwali nyumbani shetani hulia na kutoka nje ya nyumba yako huku akisema;

"Sina pa kulala humu, wala sina pa kula humu".

 

 

KUMUOMBA MWENYEZIMUNGU

Kumuomba MwenyeziMungu kila mara shetani anapotaka kukuchezea na kila unapoingia mahali pachafu. Kwa mfano:

Unapoingia chooni uisome dua ifuatayo:

"ALlaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith). Na maana yake; (MwenyeziMungu mimi najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake).

 

Kabla ya kulala usome Suratul Ikhlaas, Suratul Falaq na Suratul Naas pamoja na AyatulKursy, maana hadithi sahihi tuliyoitaja mwanzo wa darsi hii inasema kuwa anayeisoma aya hii, MwenyeziMungu anaendelea kumhifadhi mpaka asubuhi anapoamka.

Ni vizuri pia kuzisoma aya tano za mwanzo za SuratulBaqarah kisha Ayatul Kursy kisha kuzisoma aya tatu za mwisho za Suratul Baqarah na MwenyeziMungu Atakulinda na majini pamoja na uchawi katika siku nzima.

Kuzisoma dua mbali mbali kama vile:

(Audhu bikalimati llahi ttaamah min kulli shaytanin wa haammah wa min kulli aynin laammah).

Na maana yake ni;

"Najikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kila shetani na (kila) mdudu anayesota (kama vile nge na nyoka nk. na kwa kila jicho linalodhuru).

(Bismillahi lladhiy laa yadhuru ma-a smihiy shayun fil ardhi walaa fiy ssamaa wahuwa ssamiyl aliym).

Unapotoka nje ya nyumba usome:

(Bismillah tawakkaltu ala llah walaa haula walaa quwwata illa billah)

                               

KUSOMA QUR-AAN

Qur-aan ni kinga kubwa sana, na Muislamu anatakiwa daima awe anaisoma nyumbani kwake.

Hapana kitukufu anachokiogopa Shetani kuliko Qur-aan, dua, pamoja na Ibada zinazokusogeza karibu na Mola wako. Na kila mtu anapokuwa mbali na Mola wake anakuwa karibu sana na shetani.

Kwa kupiga mfano;

Mtu anapita njiani akakumbana na mbwa mkali anayebweka huku akiwa amemzuwilia njia. Bila shaka mtu huyo atashindwa na hila ya kumuondosha ili apite na zake; bali ataogopa asitafunwe na mbwa huyo. Lakini mtu huyo mara atakapotambua kuwa mwenye mbwa huyo yupo karibu, na kwamba akimuomba amwondoe njiani basi kwa ukelele wake mmoja tu, mbwa huyo ataondoka taratibu na kumpisha apite, bila shaka atamuomba msaada wake.

Mfano huu ni mfano wako wewe binadamu unapomuomba Mola wako akukinge na mashetani.

 

 

DUA ZINAMKUMBA SHETANI

Kama vile shetani anavyoweza kuwakumba wanadamu walioghafilika na kumdhukuru MwenyeziMungu, shetani naye pia hukumbwa na dua za wanaomdhukuru MwenyeziMungu:

Imeelezwa na maulamaa kuwa, shetani anapojaribu kumsogelea mchaMungu mwenye kumdhukuru Mola wake kila wakati kwa ajili ya kumkumba, basi dua zake humkumba shetani huyo na kumuangusha chini. Kisha mashetani wenzake hukusanyika na kuulizana:

"Amepatwa na nini huyu?"

Wenzao huwajibu:

"Amekumbwa na binadamu."

 

DHIKRU ALLAH

Kwa kumaliza napenda kujikumbusha nafsi yangu kwanza na pia kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu pia kwamba, hakuna kinga kubwa inayomkinga mtu kutokana na kila balaa baada ya Qur-aan kama kumdhukuru MwenyeziMungu.

Kumdhukuru unapolala, unapoamka, unapotoka nyumbani, unapositushwa na jambo, unapofurashishwa. Katika kila jambo lako jema au lisilo jema, bali hata katika kumuasi Mola wako unapomkumbuka MwenyeziMungu na kukumbuka uwezo Wake juu yako na neema Zake juu yako mara utayaacha maasi hayo.

Na ukumbuke kwamba kwa msaada wake Yeye tu Subhanahu wa Taala utaweza kujikinga na kila balaa.

 

 

USIINGIZE NDANI YA NYUMBA YAKO VIFUATAVYO

Mwisho kabisa ningependa kukumbusha kuwa ndani ya nyuma yako usije ukaingiza yafuatayo;

Usitundike picha yeyote ile.

Usisikilize nyimbo.

Usiweke baraza za kusema watu au kutukana watu.

Usitizame filam za sinema nk.

Hayo yote yanakaribisha mashetani katika nyumba yako na yanafukuza Malaika.

MwenyeziMungu Anasema:

"Na kama wasiwasi wa shetani ukikusumbua basi sema (AudhuBillahi), jikinge kwa MwenyeziMungu (na kuchezewa na shetani), Bila shaka Yeye ndiye asikiaye na ajuaye.

Hakika wale wanaomuogopa (MwenyeziMungu) zinapowagusa pepesi za shetani, mara hukumbuka, tahamaki wamekweshaona njia.

Na ndugu zao (wale walioasi) wanawavutia katika upotofu (upotevu kisha wao hawaachi).”

Al Aaraf 200-202

Hivi ndivyo ilivyo, wale wanaoasi daima hawapendi kuona wenziwao wanaokoka na wanajaribu kila njia kuwavutia katika maasi, lakini Mwenye kuomba msaada wa MwenyeziMungu basi Mola wake Atamuokoa.

 

 

Rudi Juu