Zayd Bin Haarith (رضي الله عنه) Sababu Ya Kutajwa Kwake Katika Qur-aan

SWALI:

 

Assalam aleykum ndugu zangu ktk imani nilikuwa naomba niulizie kwamba kuna kitu gani swahaba zaayid bin haarith alikifanya mpaka ikafikia atajwe ktk quran. Na ni sulah gani?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kutajwa kwa Zayd bin al-Haarithah katika Qur-aan.

 

 

Mwanzo tufahamu kuwa Zayd bin al-Haarithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa ni mtumwa wa Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha). Na pindi Bi-Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipoolewa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihawilishwa Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kuwa mtumwa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Utumwa wake haukuwa ni wa watumwa walivyokuwa wakifanyiwa wakati huo. Wazazi wake walikuja kumtafuta walipoelezewa kuwa yupo Makkah, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia wazazi wake kuwa atawapatia bure ikiwa kijana wao ataamua kuwafuata wao, lakini mtoto Zayd akakataa kwenda na wazazi wake na kuamua kubaki kuishi na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kabla ya kupatiwa utume wake. Kwa ajili hiyo, akawa anajulikana kuwa ni mtoto wake kuanzia siku hiyo, hivyo kujulikana jina lake kuwa Zayd bin Muhammad. Baadaye jambo hilo la kuwaita watoto kwa majina ya mababa wasiokuwa baba zao likaja kuondoshwa kwa kauli ya Aliyetukuka:

Waiteni kwa ubini wa baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Allaah” (Al-Ahzaab: 5). Kuanzia wakati huo jina la Zayd likabadilika na kuwa Zayd bin al-Haarithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama ilivyokuwa hapo awali.

 

Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimpenda sana Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitaka kumuozesha binti ya shangazi yake aliyekuwa akiitwa Zaynab bint Jahsh (Radhiya Allaahu ‘anha). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kumposea lakini mwanamke mwenyewe alikataa pamoja na familia yake kwa kuwa wakati mmoja Zayd alikuwa mtumwa. Hata hivyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kumtakia mpaka ikatoka hukumu kutoka kwa Allaah Aliyetukuka:

Haiwi kwa mwanamme aliyeamini wala mwanamke aliyeamini, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kuamuasi Allaah na Mtume Wake, hakika amepotea upotofu ulio wazi kabisa” (Al-Ahzaab: 36).

Kwa kuteremka Aayah hii, Zaynab (Radhiya Allaahu ‘anha) pamoja na familia yake wakawa ni wenye kukubali posa hiyo iliyoletwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, ndoa hiyo ilikuwa na changamoto pamoja na matatizo mengi. Kila wakati Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa anakuja kumshitakia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anamnasihi akae naye na avumilie kwani baada ya subira hiyo huenda kukapatikana kheri. Lakini ndoa hiyo haikudumu na ikabidi Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) amuache mkewe. Na kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya hapo aliagiziwa kumuoa mke wa mtoto wake wa kupanga ili kuondoa ada mbaya, Allaah Aliyetukuka Alitaja jina la Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) ili kufungamanisha matukio hiyo mawili.

 

Kuhusu hayo yote, Allaah Aliyetukuka Anatuelezea yafuatayo:

Na wakumbushe ulipomwambia yule ambaye Allaah Amemneemesha na wewe ukamneemesha kwa kumpa uungwana: ‘Shikamana na mkeo na umche Allaah (yaani usimuache)’ na ukaficha katika nafsi yako aliyotaka Allaah kuyatoa, na ukawachelea watu, hali Allaah ndiye Mwenye haki ya kumchelea. Basi alipokwisha Zayd haja yake na mwanamke huyo, Tulikuoza wewe ili isiwe taabu kwa Waislamu kuwaoa wake za watoto wao wa kupanga wanapokuwa hawana nao. Na amri ya Allaah ni yenye kutekelezwa” (Al-Ahzaab: 37).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share