Skip navigation.
Home kabah

Mirungi - Majani Ya Mashetani

 

                ‘Abdallah Bin Eifan

             (Jeddah, Saudi Arabia)

 

       

Salaamu zangu narusha, angani na ardhini,

Napenda kuwakumbusha, kuhusu haya majani,

Mirungi inavyotisha, kwa madhara ya mwilini,

Majani ya mashetani, mirungi  nawakumbusha.

 

Mirungi nawakumbusha, majani ya mashetani,

Mirungi  inasumbusha, chakula hukitamani,

Usingizi inarusha, upo macho taabani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Akili inazungusha, kama mwehu barazani,

Mashavu inavimbisha, kama pulizo yakini,

Mawazo ya kupotosha, yanakujia kichwani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

“Nakhwa” inapandisha, majasho tupu usoni,

Wakati inapitisha, wala faida huoni,

Maradhi husababisha, na magonjwa ya tumboni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Haina haja kubisha, wamo pia wanandani,

Wasichana hujitwisha, na mirungi mikononi,

Upate kumridhisha, mnunulie sokoni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Usiku anavyokesha, kama bundi wa porini,

Hungoja kwenye dirisha, mke yupo dirishani,

Lini bwana atabisha, mlango apite ndani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Uongo wanavumisha, eti “akher” hutamani,

Na kumbe hudhoofisha, uume wake wa chini,

Yote ni kubabaisha, atamdanganya nani ?

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Hapo anakorofisha, “uhusiano” chumbani,

Na mke anapandisha, apandapo kitandani,

Na mume ameshakwisha, hafai tena jamani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Inaharibu maisha, hukufanya tafrani,

Sana inahangaisha, ukikosa mdomoni,

Tafuta wa kukopesha, hana pesa mfukoni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Anashindwa kujilisha, lakini yupo mbioni,

Ona hujidhalilisha, anaomba masikini,

Mdomo unamwasha, hajuwi afanye nini ?

Majani ya mashetani, mirungi nawajulisha.

 

Watoto hujifundisha, kuanzia utotoni,

Tabu kujirekebisha, wakifika ukubwani,

Hakika yasikitisha, wanakuwa hatarini,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Dini imeharamisha, Mashekhe waulizeni,

Visa vyake vinatosha, kuiita maluuni,

Watu hujikalifisha, huleta shida nyumbani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Mirungi wanaotesha, Ethiopia hadi Yemeni,

Na Kenya nawajulisha, ipo Meru milimani,

Halafu husafirisha, kwa ndege kila makani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Somalia huifikisha, kwa kupitia angani,

Tanzania hupitisha, kwa kuvuka mipakani,

Inawasili Arusha, na kutoroshwa nchini,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

Shairi nasimamisha, kwenda mbele natamani,

Wakati umeshakwisha, nakimbilia kazini,

Mungu Atatusafisha, Rehema Zake ombeni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

 

 

MARUNGI HAYANA

MARUNGI HAYANA KHERI.

1)Marungi hayana kheri Twendapo tuyakashifu
Yana na nyingi khatari Mapesa kuyasarifu
Hayajali utiriri Izara na upotofu.

2)Marungi mti mbaya Uraibu wa machafu
Yatakukosesha haya Na kukufanya dhaifu
Maovu kuyaridhiya Kufuata uzinifu.

3)Marungi ulevi wake Ni handasi za kichwani
Kupitapo mwanamke Umekaa barazani
Utadadisi yafike Yule ni mke wa nani?

4)Handasi zinapopanda Huupendi ushindani
Utaridhia kuponda Rafiki na majirani
Uziboboke kwa inda Siri zako za nyumbani.

5)Tena huwa mrahimu uwambiwalo hewallah
Maagano yakatimu Kesho huwa lahaula
Kwa kuambata naumu Hutaki hata chakula.

6)Marungi unapo yala Swala hukupiga chenga
Shetwani hukutawala Kwa tamasha za kuchonga
Ukajibu masuwala Ya dini na kuyapinga.

7)Pia huwa mtatufu Hadithi kuzitongowa
Aya ukazikhalifu Tafsiri kuzikosoa
Wendani wakakusifu Na mato ukakodowa.

8)Siasa za kilimwengu Wewe zote wazijua
Kuzipanga kwa mafungu Na nyegine kuzizua
Uwe walipika jungu Na wengine wapakua.

9)Ni nyingi sifa za rungi Wakati hauruhusu
Watanganyapo na bangi Mlaji huwa habusu
Kwa kuzubaa kwa wingi Kilo kubakisha nusu.

10)Beti kumi za shairi Zatosha enyi wendani
Nami hapa takariri Niliyosema mwanzoni
Marungi hayana kheri Zindukani kwa maoni.

Abuu salim (Abdallah Timimi).

Nakupa shukuri nyingi, ndugu

Nakupa shukuri nyingi, ndugu Bin Eifani
Kwa shairi la merungi, majani ya mashetani
Ni kama kuvuta bangi, yaathirivyo mwilini
Yana madhara mwilini, tuyapingeni merungi

Merungi yana aibu, ukweli wabainika
Yanaleta maswaibu, aila zatenganika
Mwishowe ndio sababu, ndowa nyingi kuvunjika
Yana madhara mwilini, tuyapingeni merungi

Sina mengi ya kusema, kauli nasimamisha
Tumuombeni Karima, azidi kutunemesha
Tutambue yalo mema, maovu kutuepusha
Yana madhara mwilini, tuyapingeni merungi

Rudi Juu