Mke Anatoka Bila Ruhusa Ya Mume, Akimwambia Anasema Anazidisha Sheria Isiyokuweko

 

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum wa rahmatullah wabarakatuh..

Kwanza ningechukua fursa hii kuwapongeza kwa bidii munaoifanya hapa na Mola subhana wataalah awaajalie kila la Tawfiq Inshaallah..

Mimi nafanya kazi saudia nimeoa na Alhamdulillah tumebarikiwa mtoto mmoja, na mke wangu yuwaishi kenya na familia yake... Kuna jambo ambalo kila tukilizungumza basi huleta mvutano baina yetu wawili, nimejaribu sana kumueleza lakini bado sijafaulu...nalo ni kuniomba ruhusa ya kutoka nyumbani na kuenda mishuari ambapo amenijibu kuwa mimi niko mbali na pia nimezidi na masheria mengi kupita kiasi.. Je ni kweli asemayo? Tafadhali nataka ushauri wenu...Shukran wajazakallahu khairan.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mkeo kutoka bila ya ruhusa yako kwenda katika mishuari zake.

Matatizo haya hutokea mara nyingi kwa mke kutokuwa na ufahamu na ujuzi wa Dini ya Kiislamu. Au mara nyingine huwa kweli ana elimu lakini hushindwa kufuata kimatendo kwa sababu moja au nyingine. Au huenda akawa na elimu, lakini akakosa Dini. Kwa ajili hiyo Imaam al-Bukhaariy, ana mlango katika Swahiyh yake wenye kichwa cha habari, “Elimu Kabla Ya ‘Amali”. Hata hivyo, huenda mtu akawa na elimu lakini akawa hana ‘amali kwa sababu ya kutokuwa na ikhlaasw.

 

Ni juu ya mke kumtii mumewe katika mambo yasiyo ya maasi, kwani hakuna utiifu katika maasiya. Ikiwa mume hakutoa ruhusa mbali na kuwa yu mbali na mkewe ni wajibu wa mke kutii amri hiyo.

Hata hivyo, haifai kwa mume kuweka vikwazo vya kupita kiasi, kama kumzuia kwenda kwa wazazi wake na mahali ambapo anaweza kupata elimu ya Kidini. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

Wakikutiini, basi msiwatafutie njia” (an-Nisaa’ [4]: 34). Hii inamaanisha kuwa lau wake zenu watakutiini kwa mnayowaamrisha basi msiwatafutieni njia za kuwadhuru.

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Mbora wa wanawake wote ni yule ambaye unapomuangalia hukufurahisha, na unapomuamrisha hukutii na unapokuwa haupo naye, hukulindia nafsi yake na mali yako” (Abu Daawuud).

 

Hivyo, mke wako anafaa kishari’ah awe ni mwenye kukutii na asiwe ni mwenye kutoka bila ya ruhusa yako.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share