Kuongeza Bei Ya Bidhaa Kinyume Na Aliyoweka Mwenyewe Kwa Kuzidisha Bei Au Kupunguza

SWALI LA KWANZA:

 

Kwa uwezo wa ALLAH SUBHANA WATAALAH, natumai mnaendelea vizuri na shughuli zenu za kutuelimisha waumini wenzenu. Swali langu ni kama ifuatavyo, nafanya kazi katika duka la kuuza vitu, je inafaa kuongeza bei tofauti na ile iliyoandikwa na boss wangu kwa mfano kitu kinauzwa $ 100 mimi nikauza $ 120 je iko kwenye hukmu gani? Naomba mnijuze tafadhali, wahadha Assalam Alaykum warahmatullah wa barakatu

 

SWALI LA PILI:

 

Nafanya kazi katika sehemu ya kuuza vitu, bosi wangu akaweka baadhi ya vitu 50% nauliza inafaa mimi kuuza chini ya hiyo 50%? kwa mfano nikauza kwa 30% je hizo pesa ni halali kuchukua au haramu? Naomba ufafanuzi inshaalah.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuongeza bei ya bidhaa kuliko iliyowekwa na mwenyewe. Mwanzo inatakiwa tufahamu kuwa biashara ikiwa bidhaa ni za halali ni kazi iliyohalalishwa na Muumba wetu, Allaah Aliyetukuka. Na pato pamoja na faida yake ni halali kwa mwenye hiyo biashara hiyo bila utata wowote.

 

Muajiriwa anatakiwa awe muaminifu kwa muajiri wake. Na lau atahisi kuwa bidhaa hiyo inauzwa ghali sana inafaa azungumze na mwenyewe ili aridhike na hiyo bei unayomshauri yeye. Mtazame Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) alivyosifiwa katika Qur-aan:

 

Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu” (28: 26).

 

Ikiwa utaongeza bei bila ya kumueleza mwenye duka huo utakuwa udanganyifu ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Yeyote atakayetudanganya basi si katika sisi” (Muslim).

Na kwa kuwa huo ni udanganyifu, hiyo nyongeza haitakuwa ni halali kwako na kuitumia utaingia katika dhambi la wizi ambalo ni kosa kubwa.

Hali kadhalika na hilo swali la pili ni hivyo hivyo, ikiwa kupunguza kwako bei kwa aslimia hizo na ikawa ni kinyume na makubaliano na mwajiri basi utakuwa umekosea, na unapopunguza bila shaka pengo litaonekana na ikijulikana pia itavunja uaminifu wako katika kazi hiyo na kuweza kuipoteza kazi yako, na hata kama haitojulikana, vilevile ni makosa.

Hivyo, ridhika na kuweka bei iliyowekwa na mwenye biashara ili usalimike hapa duniani na Kesho Akhera.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share