Maulidi: Anataka Kufahamishwa Usomaji Sahihi Wa Maulidi Au Namna Sahihi Ya Kusherehekea

 

Maulidi: Anataka Kufahamishwa Usomaji Sahihi

Wa Maulidi Au Namna Sahihi Ya Kusherehekea

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali

 

Ndugu Zetu Wa Al Hidaya Tunashukuru Sana Kwa Juhudi Mnazo Zichukua Katika Sababu 21 Za Kumuezesha Muislam Kuto Hudhuria Sherehe Za Maulid Tumezifaham Ahsanteni Sana Sisi Hapa Muscat Oman Tulikua Tunaona Maulid Hayasomwi Kama Yanavyo Somwa Huko Nyumbani Afrika Mashariki Tunaomba Al Hidaya Iwafahamishe Ndugu Zetu Namna Sahihi Ya Kusoma Maulid

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hakika ni kuwa hakuna njia sahihi ya kusoma Mawlid kwani ni jambo ambalo lilizushwa karne tano baada ya kuaga dunia Rasuli wa Allaah, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mashia waliokuwa wakitawala Misri wakati huo. Hawa watu ni wapinga Sunnah wakubwa mpaka Waislamu waliokuwa wakipata na vitabu kama vya Imaam Maalik mfano al-Muwatwtwaa’ walikuwa wanaadhibiwa.

 

Kitu muhimu katika mwezi huu wa Mfungo Sita (Rabi’ul Awwal) si kutazama njia sahihi za kusoma Mawlid bali ni kutazama nitafanya nini mimi kuweza kufuata Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na tujie kuwa wana-historia wa Kiislamu wametofautiana kuhusu siku na hata mwezi aliozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, tunavyofikiria njia sahihi tutapata utata wa lini basi kuyasoma hayo Mawlid. Kwa minajili hiyo tutakuwa tunajitia katika janga ambalo hatutokuwa na suluhisho.

 

Njia muafaka ya sisi kufanya katika mwezi huu au mwaka mzima ni:

 

1.     Kuisoma Qur-aan pamoja na kuielewa na kufanya juhudi katika kutekeleza yaliyo ndani na kuacha yaliyokatazwa.

 

2.   Kumjua Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusoma Siyrah yake, kuielewa na kujitahidi katika kumuiga kwa yale aliyoyafanya na kuyaacha yale aliyoyakataza. Na katika kuisoma ni muhimu kupata vitabu vilivyo sahihi kuhusu suala hilo.

 

3.    Katika kumuiga ni kufunga siku ya Jumatatu, kwani amesema katika Hadiyth ya Muslim kuwa ndio siku aliyozaliwa.

 

4.     Kuyaeneza yale aliyoyafundisha kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu

 

5.   Pesa na gharama kubwa zinazotumika katika kuyaandaa Mawlid na kulishana, zitumike kusaidia mayatima na kujengea Madrassah na kusaidia wanafunzi wasiojiweza na mengine ya manufaa kama hayo.

 

Ikiwa tutafanya hayo yaliyo juu basi faida yake itakuwa ni kubwa sana kwa maisha yetu hapa duniani na kesho Aakhirah kuliko kutazama njia iliyo sahihi ya kusoma Mawlid au kutafuta kurekebisha vitabu vya Mawlid kama Barzanji n.k., mambo ambayo yote hayo hayana umuhimu wowote.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share