Ufafanuzi Wa Maneno Katika Kitabu Cha Ibn Taymiyyah Kuhusu Bid'ah Ya Maulidi

 

SWALI:

 

Bismillaahi rahmaani rahiim Asslaamu alaikum warahmatu llahi wabarakatu Shukurani na sifa njema zote ni za Allah subhaanahu wataala na namtakia bwana wetu mjumbe wa mwenyezimngu Muhammad rehma na amani za mwenyenimgu ziwe juu yake.

 

Ndugu zangu waislamu wa alhidaaya kwa hisani yenu nifafanulieni nami maneno ya fuatao ya sheikhu-l-islam mwenyezimgu amrehemu ibnu taimiya. Kwa hakika maneno haya natutatanisha kulingana na yanavyo tafsiriwa na ahlusuna na ahlubidaa. Maneno haya yako katika kitabu kiitwacho iqtidhwaau swiratulmistaqiima, mjalada wapili, kilicho chapishwa na daarul-aaswima mwaka wa 1998m/1419h - Ahlusunnah Wanasema ibnu taymia radhi za mungu ziwe juu yake amesema katika ukurasa wa 123 wa kitabu hicho kuwa kusoma maulidi na kuyafanya kila mwaka wakati fulani hayafai kwa sababu wanazuoni walopita awakuyafanya.

 

Ahlubidaa Wanasema ibnu taymia radhi za mungu ziwe juu yake amesema katika ukurasa wa 126 wakitabu hich kuwa kusoma mawlid na kuyafanya wakati Fulani kila mwaka basi mwenyekufanya hivyo atapata thawabu nyingi sana Ninaomba munifafanulie hizi tafsiri mbili. ipi iko sawa na ipi iko makosa.

 

Munielezee usawa wake na makosa yake. Na pia ikiwa kuna masuala ya nahwu muniwekee wazi kwamfano ikiwa kuna maneno yalio tangulia au yalio akhirishwa Kwa hisani yenu ikiwa mutaweza kuni jibu kwahara itakuwa uzuri zaidi. Kwa sababu tuna hitajia maneno haya kwenye mjadala utarajiwao kufanyika mwezi ujao. Asanteni sana. Inshaallah mungu atawajazi kheri

 

SWALI LA PILI:

 

Assalaam alaikum warahamatu llahi wa barakatu. ndu zangu niliwatumia suali kuhusu sheikhu-l-islam ibnu taimiya kuwa kwenye kitabu chake cha iqtwidhwaau swiratu-l- mustaqiim, mjalada wapili, kilicho chapishwa na daarul-aaswima mwaka wa 1998m/1419h. Katika ukurasa wa 123 amesema mawlid hayafai kusherehekewa na kwenye ukurasa wa 126 hufaa kusherehekewa. Ni vipi masaala haya.

shukran

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu maneno ya Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaahu).

 

Katika kitabu hicho ulichokitaja ‘Iqtidhwaa’ asw-Swiraatw al-Mustaqiym’ kilichochapishwa na al-Maktabuth Thaqaafiy as-Su‘udiyy, Morocco cha 1419 H, uk. 294 – 296 ambacho kimehakikiwa na mwanachuoni mkubwa Shaykh Muhammad Haamid al-Fiqqiy.

 

Ibn Taymiyyah amepatia kichwa cha habari, “Bid’ah za Sherehe za Mazazi ya Mtume”. Amesema ndani: “Na hivyo hivyo yaliyozuliwa na baadhi ya watu ima kwa kuwafuata Manaswara kusherehekea mazazi ya ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) au kwa ajili ya kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuadhimisha. Huenda Allaah Aliyetukuka Akawapatia thawabu kwa mahaba haya na ijtihadi hii (1) sio kwa bid’ah. Pamoja na kuchukua mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni sherehe, pamoja na kutofautiana watu na mazazi yake. Kwa kuwa hili halikufanywa na watangu wema pamoja na kusimamia haja hiyo na kutokataza. Na lau kufanya hivyo ingekuwa ni kheri au yenye nguvu zaidi Watangu wema (Radhiya Allaahu ‘anhum) wangetutangulia kwayo kwani wao walikuwa na mahaba makubwa na kumtukuza zaidi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko sisi. Na wao katika kufanya kheri walikuwa msitari wa mbele. Na hakika ni kuwa mahaba kwake na kumtukuza ni kumfuata, kumtii, kufuata amri zake na kuhuisha Sunnah zake za wazi na za siri. Pia kueneza kwa aliyotumwa nayo na kutia juhudi katika hayo kwa moyo, mkono na ulimi. Hakika hii ndiyo iliyokuwa njia ya wale wa mwanzo miongoni mwa Muhajirina na Answari na wale waliowafuata kwa wema na ihsani. Na utawakuta wengi wa hawa wenye kutilia mkazo bid’ah kama hizi pamoja na yale waliyo nayo, kama malengo mazuri na ile ijtihadi inayotazamiwa kuwapatia wao thawabu, utawakuta ni wavivu sana katika kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nashati inayotakiwa. Hakika huyu yuko katika daraja sawa na mwenye Msahafu asiyeusoma au akasoma pasi na kufuata. Na yuko daraja sawa na mwenye kupamba Msikiti pasi na yeye kuswali ndani yake au kuswali kwa uchache. Na katika daraja ya yule anayechukua tasbihi na miswala iliyopambwa. Na mifano ya hayo mapambo ya dhahiri ambayo hayapo katika Shari’ah, yanayompeleka kwenye riyaa na kiburi na yenye kumshughulisha na sheria yenye kuharibu hali ya mwenye kuyafanya (2). Hii imekuja katika Hadiyth: “Haitoharibika ‘amali ya Ummah kabisa isipokuwa wanapamba Misikiti”.”

 

Haya ndio maneno ya Ibn Taymiyyah katika kitabu chake hicho.

Shaykh Muhammad Haamid ameandika yafuatayo chini yake:

 

(1) Vipi watapata thawabu kwa hilo? Na wao wamekwenda kinyume na uongofu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na uongofu wa Maswahaba zake? Panaposemwa: Kwa kuwa wao wamefanya juhudi, wakakosea; sisi twasema: Ni ijtihaad gani katika hili. Je, nuswuus (maandiko) zimeacha nafasi kwa ijtihaad katika mas-ala ya Ibaadah? Na jambo hilo lipo wazi kabisa. Na hilo ni kushindwa na ujahili na kuhukumu kwa matamanio, yaliyowachukua watu kukengeuka na uongofu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufuata Uyahudi, Unaswara na Upagani. Wanastahiki juu yao laana ya Allaah na ghadhabu Yake. Na je, mahaba na kumuadhimisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapatikana kwa kukengeuka na uongofu wake na kumchukia na kuchukia aliyokuja nayo ya kweli katika kuwatengeneza watu kutoka kwa Mola wake Mlezi na kuwaendea na kushidana na Upagani, Uyahudi na Unaswara? Na ni wapi hao waliohuisha sherehe hizo za Kipagani? Je, hao ni Maalik au ash-Shaafi‘iy au Ahmad au Abu Haniyfah au Sufyaan wawili au wengineo miongoni mwa Ma-Imaam waongofu (Radhiya Allaahu ‘anhum)? Mpaka awaombe msamaha na makosa yao.

Sivyo hivyo! Bali yaliyozuliwa katika sherehe hizi za shirki ni kutoka kwa ‘Ubayd (‘UbayduLlaah) ambao Ummah umejumuika juu ya uzindiki wao na kuwa wao ni makafiri zaidi hata kuliko Mayahudi na Manaswara na kwamba wao walikuwa maafa kwa Waislamu. Na kwa mikono yao pamoja na vitimbi vyao na waliyopiliza kwa Ummah katika sumu za Kisufi ziliwapoteza Waislamu na njia nyoofu. Mpaka wakawa pamoja na walioghadhibikiwa na waliopotea.

Na maneno ya Ibn Taymiyyah mwenyewe ni dalili juu ya kinyume kwa alichosema kupata thawabu kwao. Kwa kuwa kumpenda na kumtukuza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajibu wa kila Muislamu: Hakika hiyo ni kufuata kwa aliyokuja nayo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Hii ni kama Alivyosema Allaah Aliyetukuka:

Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Alaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu(Aal-‘Imraan 3: 31).

Na Amesema tena:

Huwaoni wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shaytwaan anataka kuwapotezelea mbali. Na wanapoambiwa: Njooni kwenye yale Aliyoyateremsha Allaah, na njooni kwa Mtume; utawaona wanafiki wanakukwepa kwa upinzani. Basi inakuwaje unapowasibu msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao? Hapo tena hukujia wakiapa kwa Allaah wakisema: Hatukutaka ila wema na mapatano. Hao ndio wale ambao Allaah Anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Basi waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika nafsi zao. Na hatukumtuma Mtume yeyote ila atiiwe kwa idhini ya Allaah. Na lau pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia, wakamwomba Allaah msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangelimkuta Allaah ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu. La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa(an-Nisaa’ 4: 60-65).

Na pia:

Na wanasema: Tumemuamini Allaah na Mtume, na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini. Na wanapoitwa kumuendea Allaah na Mtume Wake ili ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa. Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kutii. Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au wanaogopa ya kuwa Allaah na Mtume Wake watawadhulumu? Bali hao ndio madhalimu. Haiwi kauli ya Waumini wanapoitwa kwa Allaah na Mtume Wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumetii! Na hao ndio wenye kufanikiwa. Na wenye kumtii Allaah na Mtume Wake, na wakamwogopa Allaah na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu(an-Nuur 24: 47-52).

 

(2) Na vipi baada ya yote haya anatarajiwa kuwa atapata thawabu au kukubaliwa kwa mwito wa lengo jema? Na je, ‘amali za dhahiri ndio anuwani ya malengo na Niyah? Na ikiwa hawa watapata thawabu kwa bid’ah zao, basi itakuwa kwa Mayahudi na Manaswara na kila kafiri thawabu kwa wanaokuja nayo katika ukafiri na upagani kwa kuwa wao pia wanafanya juhudi kwa Imani yao na hawakusudii kwayo ila wema na tawfiki.

 

Yaliyotangulia juu ndio maneno ya Ibn Taymiyyah na maelezo na maelekezo yaliyofuatia ni uchambuzi wa Shaykh Muhammad Haamid.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share