Kupelekea Posa Kufuata Mila Za Kupeleka Barua Katika Kitambaa Cheupe

SWALI:

 

Assalaam Alaykum

Samahani mimi ni kijana wa kiislam amabye ninaishi kwa mujibu wa Qur-an na Sunnah ambaye nimefikia umri wa kuowa na Alhamdulillah nimeshampata mwenza wa kutengeneza nae familia kwa mujibu wa Qur-an na Sunnah na hivi punde nataka nitume wazee wangu kupeleka posa maana me nipo ughaibuni (Europe) na huyu mwenzi wangu nae pia yuko hukuhuku.

 

Sasa tatizo langu ni kwamba huyu mwenzangu ananiambia ya kwamba niwaambie wazazi wangu ya kwamba watakapo peleka posa kuwe na barua na hiyo barua iwe na kitambaa sijuwi na pia kuwe na pesa ndani ya barua hiyo, kwa upeo wangu mimi dini yetu ya kiislam ambayo ndiyo mila yetu haijaelekeza tupeleke posa kwa style hiyo ya barua kuwa na kitambaa na pesa ndani sasa me nimemwambia kwamba wazee wangu wakipeleka hiyo posa hawatoweza kufanya hivyo kwa sababu siyo mila yetu sisi waislam. Sasa tatizo langu hapa ni kwamba Je! KUPELEKA POSA KWA BARUA ILIYOKUWA NA KITAMBAA NA PESA NDANI NDIVYO ALLAH (S.W) NA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) WALIVYOTUELEKEZA AU WAMUTUELEKEZA TUPELEKEJE POSA? Tafadhali naomba msaada wenu ndugu zangu. Natanguliza shukrani zangu za dhati kwenu.

WABILLAH    TAWFIIQ

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu posa katika Uislamu.

Hakika ni kuwa posa ilivyofanyika katika Uislamu kuanzia wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inafahamika vilivyo. Posa inaweza kuja kutoka kwa mume na watu wake kwa jamaa za mke au mzazi wa mke kumtafutia binti yake mume.

 

Ikiwa wazazi watakwenda kwa wazazi wa mke, baada ya kupeleka maneno, na wazazi wa mke watataka kupatiwa muda wa kufikiria, kufanya shuuraa, kuulizia, kutafiti na baadaye kukubali au kukataa.

Ikiwa wamekubali baada ya kumshauri binti yao ni vyema mume mtarajiwa aende amuone atakaye kuwa mkewe ili apate kutulia na kuridhika kabla siku ya Nikaah.

Binti huyo au wazazi wake wataweka kiwango cha mahari ambacho mume anatakiwa kutoa.

 

Hii njia ya kuweka pesa kwenye kitambaa au bahasha haipo katika mafunzo ya Kiislam, na huenda ni njia ya kitamaduni fulani au itikadi fulani ya kishirikina ambayo inakwenda kinyume na Uislamu na hapo shari’ah haitokubaliana nalo ikiwa ni hivyo.

 

Hivyo, inatakiwa uulize maana ya pesa kutiwa hapo ndani ya kitauna kisiwe cha rangi nyengine yoyote? Na kwanini yasitumwe mahari tu bila kuwekwa kwenye kitambaa?

 

Hivyo, ukipata majibu yako, basi utayalinganisha na hayo tuliyokueleza na utakuwa na jibu tayari kuhusiana na jambo hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share