Unapotenda Dhambi Omba Tawbah

 

Naaswir Haamid

 

 

tawbah ni kuwacha madhambi yote na kujuta kwa kila dhambi Muislamu aliyoifanya, pamoja na kuwa na azma ya kutorudia tena kutenda dhambi hiyo. Wala Muislamu aliyeamini Siku ya Qiyaamah asitosheke na hayo tu, bali aelewe kwamba hana uhakika wa 100% kwamba tawbah yake imekubaliwa ama laa. Hivyo, ni wajibu wake kuendelea kuwa na matarajio tu na unyenyekevu wa hali ya juu.

 

Mola wetu Mwenye kusamehe madhambi makubwa makubwa na madogo Anatuambia:

 

{{Enyi Mlioamini! Tubuni kwa Allaah tawbah iliyo ya kweli, huwenda Mola wenu Akakufutieni maovu yenu na Akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito mbele yake. Siku ambayo Allaah Hatomdhalilisha Mtume wala wale walioamini pamoja naye; nuru yao itakuwa inakwenda mbele yao na pande zao za kulia (na kushoto); na huku wanasema: "Mola wetu! Tutimiziye nuru yetu, na utughufiriye, hakika wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu".}} [Suratut-Tahriym: 8]

 

Hakuna shaka yoyote kwamba nafsi ya mwanaadamu ni yenye kumshawishi mja kuingia kwenye upotofu kwa lengo la kumuasi Mola wake. Na iwapo mja anajitahidi kutenda mema, basi Ibilisi mkosefu wa Rahmah za Allaah humletea wasi wasi mbaya na kumharibia Ibada zake. Ndio sababu Muislamu anahitajika milele kuwa na hadhari dhidi ya adui yake Ibilisi Maluuni.

 

Kutubia kwa Mola ni katika sifa njema za Waislamu. Halikadhalika, kwa kuwa Rahmah Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zipo juu basi Anawakubalia tawbah za waja Wake madhali bado hawajafikia katika mauti:

 

{{Na tubieni nyote kwa Allaah, enyi Waislamu ili mpate kufaulu.}} [Suratun-Nuwr: 31]

 

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

((Kwa hakika Allaah Anakubali tawbah ya mja (Wake) madhali bado hajawa katika Sakaratul-Mawt.)) [Imesimuliwa na Ibn 'Umar na kupokelewa na Imaam At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Tuache ujinga na turudie kwa Mola. Na kwa sababu gani kiumbe dhaifu umuasi Mola Aliyekuumba, Alikunyima kitu gani Allaah? Huna shukurani kwa mola wako? Na kama wewe unajiona una nguvu za kumuasi Allaah basi usikae katika Ardhi wala usitembee katika Mbingu Yake, nenda katafute pahala ukae peke yako, au hata usile neema Zake, tafuta riziki yako mwenyewe ule. Hayo yote hutoyaweza, tena WaLlaahi utashindwa, ni muhali kuwa hivyo.

 

Enyi wenye kuchelewesha tawbah kwa kusubiri uzee, mumeweka ahadi gani kwa Mola wenu kwamba Atawafikisha umri huo? Nini mnachokipata katika kumuasi Mola?

 

Basi kama unamuhitajia Allaah na unahitajia Rahmah Zake, usimuasi na wala usikate tamaa. Atakaeteleza kisha akarudi kwa Mola wake kweli kweli na akatenda mema kwa kutaka kulipiza ule wakati alioupoteza katika mambo mabaya, basi huyo hupokelewa tawbah yake.

 

 

Share