Amembusu Mke Wa Mtu, Anajuta Na Ametubu, Je, Amjulishe Mume Wa Huyo Mwanamke? Na Mwanamke Bado Anamtaka

SWALI:

 

Assalam alaikum. Suala langu nikua nina rafiki yangu kaniuliza swali nikashindwa kumjibu. Anauliza: je kumbusu mke wa mtu na unajua kama ni vibaya lakini ibilisi kanizidi je nifanye nini tokea siku hio sina mawasiliano nae na wala sina khabari nae tena. Kwa kutambua nililofanya sio sahihi. Lakini sina raha hata kidogo juu ya jambo hili, huyo binti nilikua nimuoe hapo awali lakini haikua riski, yeye bado ananitaka na mimi nilikua bado namtaka japokua yeye keshaolewa ndio yakatokea haya ya kumbusu, lakini mimi sasa hivi najuta kwa hayo yote japokua yeye bado anata mawasiliano na mimi lakini mimi nimekata mawasiliano na yeye, je nifanye nini maana baadhi ya marafiki zangu wananiambia nikamwambie mumuwe kua nimefanya jambo hili, lakini mimi roho yangu nzito sababu naona kua wao bado wanaishi maisha mazuri na mumewe nikisema nikamwambie inaweza kua mimi ndio sababu ya huyo mwanamke kuachwa. Naomba jibu tafadhali. Shukran

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumbusu mke wa mtu.

Ni hakika kutokana na maelezo yako kuwa umefahamu alilofanya si sawa kishari’ah.

 

 

Allaah Aliyetukuka Anatuhimiza sana tusiikaribie zinaa (al-Israa’ [17]: 32). Na kumbusu mke wa mtu au msichana ambaye unaweza kumuoa ni makosa na ni katika kuikaribia zinaa.

 

Kwa maasiya yoyote kusamehewa inatakiwa afanye toba ya kweli kweli, bila ya hivyo atakuwa bado ana dhambi. Ama ikiwa dhambi aliyofanya inahusisha heshima au haki ya mtu ni lazima atimize masharti manne kabla ya kusamehewa. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo:

 

1.     Ni kuacha maasiya hayo.

2.     Kujuta kwa kufanya.

3.     Kuazimia kutorudia tena madhambi hayo.

4.     Kumuomba msamaha mwanaadamu aliyemfanyia makosa.

 

Kukosekana moja katika masharti haya, toba yake itakuwa haijakamika. Bila shaka upo msingi muhimu wa Fiqh ambao unasema: “Dhara dogo katika madhara mawili”. Huenda katika kwenda kumwambia mume kukatokea dhara kubwa la kuachwa mke au kupata madhara mengine kutoka kwa mume.

Katika hofu hiyo ataacha kumwambia mume kuhusu yaliyotendeka huku akimuomba sana Allaah Aliyetukuka Amsamehe kwa madhambi hayo pamoja na kufuata masharti mengine yaliyo hapo juu.

 

Ama akiwa ana habari kuwa mume huyo amepata habari kuhusu hayo yaliyotendeka itabidi awe jasiri wa kumkabili amwambie yaliyojiri pamoja na kumtaka msamaha.

 

Hata hivyo, inatakiwa tuwe na tahadhari sana kuhusu kufanya madhambi. Na katika hilo tusitazame ukubwa au udogo wa dhambi bali tutazame tunayemkosea. Ikiwa mwanaadamu tunayemkosea tunaogopa kumkabili seuze Allaah Aliyetukuka tutamkabili vipi siku ya Qiyaamah.

 

Kwa kuwa nduguyo amekwambia amejuta sana anatakiwa akate mahusiano kabisa wala asiwe ni mwenye kuzungumza na huyo mke wa mtu, kwani mazungumzo ndio chanzo cha uzinzi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share