Nakaribia Kuzini Na Shemeji, Je, Nifanyeje Kujiepusha Na Vipi Nitahukumiwa Na Allaah?

 

 
SWALI:
 
Asaalam alaykum.Mimi ni mke wa mtu nipo na mume wangu miaka kumi,na sijawahi kuzini nje ila ninak urubia zina na mdogo wake mume wangu.je mnaweza kunisaidia vipi? ili niweze kujitoa kwenye jambo hili?na kwa Mwenyezi Mungu nahukumiwa vipi?naombeni msaada wenu  
 


 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Tumepokea swali lako hili, na tumeamua kukujibu haraka mno ingawa kuna maswali mengi nyuma yako, lakini kutokana na hali hiyo uliyonayo ya hatari, tumeona ni muhimu na wajibu wetu kulipa swali lako kiupambele ili kukupa nasaha uweze kujiokoa na maasi hayo haraka iwezekanavyo.
 
Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutujaalia kutekeleza kazi hizi kwa ajili Yake khaswa kutuwezesha kuwajibu maswali yenu yenye mas-ala mbali mbali yanayohitaji nasaha na elimu. Vile vile tunakushukuru wewe ndugu yetu kwa ujasiri wako wa kuweza kutukabili katika mas-ala haya nyeti kabisa na yanayokaribia kukuingiza katika maasi makubwa. Hivyo utambue kabla ya lolote kwamba hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anakupenda kwani Amekuzindua mapema kabla ya kutumbukia katika maasi haya na Akakuhidi kutukabili kutafuta uongofu uokoke nayo. Hivyo inapasa kwanza umshukuru Mola Mtukufu, kwani wangapi wako katika hali kama yako lakini wanashindwa kuzindukana bali moja kwa moja wanatumbukia katika maasi kama hayo ambayo ni mepesi kabisa mtu kuingia kutokana na nafsi zetu zilivyo dhaifu khaswa katika jambo hili, na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuonya hata kuyakaribia Anaposema:
 
 
 ((وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً))
 ((Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya))  [Al-Israa: 32]
 
Jambo la pili upasalo kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni kuwa uko katika neema ya kuishi na mume kwa muda wa miaka kumi, bila shaka mume huyo ni mtu mwema kwani inavyoonyesha mna masikilizano mazuri hadi muweze kuishi pamoja kwa salama kama ulivyotaja kuwa hukupata kuingia katika maasi hayo kabla. Wanawake wangapi wanatamani kuolewa katika zama hizi na hawapati waume? Na wangapi walioolewa na hawana maisha mazuri na waume zao? Kisha fikiria kamamumeo ndiye angekuwa katika hiyo nafasi yako ya kutaka kufanya maasi hayo ambayo wewe ndiye unayafikiria kuyafanya, kisha ukaja kujua, ingekuwaje hali yako? Hivyo ndugu yetu inakupasa pia uzingatie jambo hili, utafakari na ufanye hima kuihifadhi neema hii uliyojaaliwa kwa kulinda ndoa yako usije kuiharibu kwa matamanio hayo ya nafsi ya muda mfupi yenye majuto ya milele.
 
 
Umetaja kuwa anayekushawishi kuingia katika maasi haya ni shemeji yako; je, unaishi naye nyumba moja? Kama unaishi naye nyumba moja, basi jambo la kwanza ni kumwambia mume wako amuondoshe bila ya kujua sababu ili isisababishe kuleta uhasama baina ya ndugu. Hivyo unaweza kumpa sababu kuwa umepata mafunzo yanayokataza kuishi na mtu asiye mahram wako, bali ni hatari zaidi kuishi na shemeji kama Hadiyth ifuatayo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inavyotufunza:
 
  ))إياكم والدخول على النساء، قالوا: يا رسول الله أرأيت الحمو؟ قال: الحمو الموت((متفق عليه
 
((Tahadharini kuwaingilia [kuingia majumbani mwao] wanawake)) Wakasema: Ewe Mjumbe wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: ((Shemeji ni mauti)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
 
 
Mtajie mume wako kuwa umeiona Hadiyth hiyo na hivyo hutaki tena huyo Shemeji aishi na nyinyi hapo, na pia kuna makala muhimu sana kuhusu hatari ya kuchanganyikana wanawake na wanaume wasio maharimu. Soma hapa
 
 
 
 
Kwa hiyo mjulishe kuwa unataka kuishi kwa kufuata sheria za Kiislamu na hivyo ni kheri kwenu nyote.
 
Na ikiwa huishi naye shemeji yako bali anakuja hapo nyumbani, basi hali kadhaalika unatakiwa uzingatie maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hayo na ujiepushe kabisa kukutana naye, na khaswa kuwa pekee naye.

 
 
Tambua kwamba shaytwaan yuko tayari amekuvaa kutaka kukutumbukiza katika maasi haya kwa hiyo inakupasa ufanye juhudi kubwa mno kujiepusha naye kabisa kwa kila njia, kwani hila zake ni za nguvu mno na hatokuacha ila utakapoamua kumuepuka kikweli kweli. Atakupambia kwa kila aina ya fikra na vitendo akujaze matamanio katika nafsi yako hadi ufikie wakati usiweze kutambua baina ya makosa uyatakayo kuyafanya, nafsi yako ikakuamrisha kuzidi kukaribia hatimaye ukajikuta tayari umeshatumbukia.

 
 
Tunakupa uhakika ndugu yetu kwamba madamu umetaka kujiokoa na maasi haya basi utaweza kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kutia nia ya dhati na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), Akuepushe nayo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
(( وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا))
((Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea))[At-Twalaaq: 2]
 
 
(( وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ
 لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا))
 
((Na Humruzuku kwa njia asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah Kajaalia kila kitu na kipimo chake)) [At-Twalaaq: 3]
 
 
(( وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا
((Na anayemcha Allaah, Humfanyia mambo yake kuwa mepesi)) [At-Twalaaq: 4]
 
 
 
Hivyo jambo la kufanya baada ya kutia nia na kumuomba sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), zidisha taqwa; zidisha vitendo vya Sunnah baada ya kutimiza fardhi zako; Swalah na Swawm, soma Qur-aan sana, soma adhkaar, omba maghfirah sana na muhimu zaidi sikiliza mawaidha mengi khaswa yanayohusu uovu wa maasi haya na adhabu zake n.k. Tunakuwekea mwisho wa hili jibu baadhi ya mawaidha na Inshaa Allaah yaweze kukuzidishia taqwa na khofu ya kumuasi Mola wako.

 
 
 
 
 
Na uhakika mwingine ni kuwa tambua maasi kama haya anapotenda mtu mwema kama wewe ambaye hakupata kufanya na mwenye kutaka uongofu, hujuta sana baada ya kutenda, na majuto yatabakia milele yakikuumiza utatamani urudishe wakati ujirekebishe lakini kama unavyojua kuwa maji yakimwagika hayazoleki, na kama inavyosemwa 'prevention is better than cure' (Kinga ni bora kuliko matibabu), kwa hiyo chukua tahadhari kubwa kujikinga kabla ya majuto.

 
 
 
 
 
Vile vile utambue kwamba kufanya maasi hayo na shemeji yako utasababisha uhasama baina ya ndugu hao wawili pamoja na ndugu na jamaa zake, kwani hakuna atakayekupendelea wewe kufanya kitendo hicho. Wewe ni mtu wa nje kwao na shemeji yako ni ndugu yao hivyo kama inavyosemwa: 'Damu nzito kuliko maji", jamaa zake wote watakuona wewe ndiye muovu, ama ndugu yao, kwa vyovyote iko siku wanaweza kupatana naye tuna hali wewe unaweza kuwa tayari ushapewa talaka.
 
 
 
Pia Uhasama baina ya ndugu na kukatana (kutengana) ni jambo Alilolikemea Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) sana katika Qur-aan pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi, na wewe ndiye utakayechukua jukumu la wote hao kwani wewe ndiye wa kwanza mwenye kupasa kujiepusha na maasi haya kwa vile umeolewa na unaishi vizuri na mumeo, na madamu mafunzo haya yameshakufikia utakuwa huna hoja mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) siku ya Qiyaamah.
 
Hakika ndugu yetu inakupasa uzingatie sana jambo hili na haraka mno umlaani shaytwaan akuepuke. Jitahidi kumuepusha shaytwaan kwa kujenga hisia za chuki kwa shemeji yako iwe unamchukia badala ya kuwa na hisia za mapenzi naye na kila unapomuona ujitenge mbali naye kabisa na Inshaa Allaah hila hii itakusaidia.  Fahamu kuwa huyo shemeji yako naye si mtu mzuri kabisa, hana huruma na ndugu yake wala hana heshima, achilia mbali staha kwa Mola wake Muumba.

 
Ama kuhusu adhabu zake, tunapata mafunzo kutoka katika Qur-aan na Sunnah; ni madhambi makubwa Aliyoyakemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuahidi adhabu kwa mwenye kutenda, na Amewapa sifa ya 'Ibaadur-Rahmaan' (Waja wa Ar-Rahmaan) wale ambao watajiepusha nayo:

 
 
 ((وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَايَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَايَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا))  
 
(( يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ))
 
 ((إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَيُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًارَّحِيمًا))
 
((Wale wasiomuomba mungu mwengine pamoja na Allaah wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakayefanya hayo atapata madhara))
 
 
 
 
((Azidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka))
 
 
 
 
 
((Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema.  Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema.  Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-Furqaan: 68-70]
 
 
 
Pia kuzini kwa mwanamume na mwanamke aliye huru (sio mtumwa), mwenye akili timamu, na amefanya zinaa wakati tayari yumo katika fungamano la ndoa, basi adhabu yake ni kupigwa mawe hadi mauti yawafike kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo:
 
 
 
فِي الصَّحِيحَيْنِ مِنْ رِوَايَة الزُّهْرِيّ عَنْ عُبَيْد اللَّه بْن عَبْد اللَّه بْن عُتْبَة بْن مَسْعُود عَنْ أَبِي هُرَيْرَة وَزَيْد بْن خَالِد الْجُهَنِيّ فِي الْأَعْرَابِيَّيْنِ اللَّذَيْنِ أَتَيَا رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ أَحَدهمَا : يَا رَسُول اللَّه إِنَّ اِبْنِي هَذَا كَانَ عَسِيفًا - يَعْنِي أَجِيرًا - عَلَى هَذَا فَزَنَى بِامْرَأَتِهِ فَافْتَدَيْت اِبْنِي مِنْهُ بِمِائَةِ شَاة وَوَلِيدَة فَسَأَلْت أَهْل الْعِلْم فَأَخْبَرُونِي أَنَّ عَلَى اِبْنِي جَلْد مِائَة وَتَغْرِيب عَام وَأَنَّ عَلَى اِمْرَأَة هَذَا : الرَّجْم فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَأَقْضِيَنَّ بَيْنكُمَا بِكِتَابِ اللَّه تَعَالَى الْوَلِيدَة وَالْغَنَم رَدّ عَلَيْك وَعَلَى اِبْنك مِائَة جَلْدَة وَتَغْرِيب عَام . وَاغْدُ يَا أُنَيْس  - لِرَجُلٍ مِنْ أَسْلَم - إِلَى اِمْرَأَة هَذَا فَإِنْ اِعْتَرَفَتْ فَارْجُمْهَا))  فَغَدَا عَلَيْهَا فَاعْتَرَفَتْ فَرَجَمَهَا      البخاري  و مسلم

 
 
 
  Katika Swahihayn kutoka kwa Abu Hurayrah na Zayd bin Khaalid Al-Juhani (Radhiya Allahu 'anhum) katika kisa cha Mabedui wawili waliokuja kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Mmoja alisema: "Ewe Mjume wa Allaah, mwanangu (wa kiume) aliajiriwa na bwana huyu kisha akafanya zinaa na mke wake. Nimemlipa fidia kwa ajili ya mwanangu kwa kumpa kondoo mia moja na mtumwa mwanamke. Lakini nilipowauliza watu wenye elimu, wamesema kwamba mwanangu apigwe mijeledi mia na ahamishwe mji kwa muda wa mwaka na mke wa huyu bwana apigwe mawe hadi afariki".  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, nitahukumu baina yenu wawili kutokana na kitabu cha Allaah. Rudisha mtumwa mwanamke na kondoo  na mwanao apigwe bakora mia kisha mwanao ahamishwe mbali kwa muda wa mwaka. Nenda Ewe Unays! )) Alimwambia mtu katika kabila la Aslam, ((Nenda kwa mke wa huyu bwana na akikiri makosa yake, basi mpige mawe hadi mauti [yamfike])) Unays akamuendea na akakiri makosa yake, kwa hiyo akampiga mawe hadi mauti. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 
 
 
 
Vile vile,

 
 
 
قال الإمام مالك أن عمر، رضي الله عنه، قام فحمد الله وأثنى عليه، ثم قال: أما بعد، أيها الناس، فإن الله بعث محمدًا بالحق، وأنـزل عليه الكتاب، فكان فيما أنـزل عليه آية الرجم، فقرأناها وَوَعَيْناها، وَرَجمَ رسول الله صلى الله عليه وسلم وَرَجمْنا بعده، فأخشى أن يطول بالناس زمان أن يقول قائل: لا نجد آية الرجم في كتاب الله، فيضلوا بترك فريضة قد أنـزلها الله، فالرجم في كتاب الله حق على من زنى، إذا أحصن، من الرجال والنساء، إذا قامت البينة، أو الحبل، أو الاعتراف. (  الموطأ و البخاري و مسلم  )

 
 
 
 
 
Imaam Maalik amerikodi kwamba 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alisimama na kumsifu na kumtukuza Allaah, kisha akasema: "Enyi watu! Allaah Amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa haki na Amemfunulia Kitabu Chake. Jambo moja alilofunuliwa ni Aayah ya kupigwa mawe hadi mauti ambayo tumeisoma na kuifahamu. Mjumbe wa Allaah ameitimiza adhabu hii ya kupigwa mawe na baada yake pia sisi tumeitimiza. Lakini nakhofu kuwa muda (miaka) utakapopita wengine watakuja kusema kuwa hawakuiona hii Aayah ya kupigwa mawe katika Kitabu cha Allaah, na watapotoka kwa sababu ya kuacha moja ya wajibu wa kisheria iliyofunuliwa katika Kitabu cha Allaah kwa mwanamume au mwanamke watakaofanya zinaa, ikiwa mmojawapo ameoa au ameolewa, na ushahidi ukipatikana au mimba ikidhihirika kutokana   na kitendo hicho, au akikiri mmojawao.[Al-Muwattwaa, Al-Bukhaariy na Muslim]
 
 
 
 
 
 
Hadiyth hizi pekee, ndugu yetu bila ya shaka zitakutosheleza kutambua jinsi gani maasi haya yalivyo maovu mbele ya Allaah hadi Ahukumu adhabu kama hii, na lau ingelikuwa hukumu hii inatekelezwa katika dola za Kiislamu au kwa kila Muislamu anayetenda kitendo hiki, basi hakika hakuna mtu yeyote angelithubutu kutenda kitendo hiki kiovu kabisa.
 
 
 
 
 
 
Tunatumai kwamba nasaha zetu pamoja na mafunzo hayo ya dini yetu yatakukinasiha ndugu yetu uzindukane zaidi na uzuie nafsi yako na kujieupusha haraka na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuhidi katika jambo hili na Akuzidishie taqwa ubakie katika radhi Zake. Aaamiyn.

 
 
 
 
 
 
Bonyeza hapa upate mawaidha yanayohusu maudhui:

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Na Allaah Anajua zaidi
Share