Maonyo Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kujiepusha Na Kughafilika Kwa Nafsi

Maonyo Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kujiepusha Na Kughafilika Kwa Nafsi

 

www.alhidaaya.com

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuonya tusije kufikia hali ya nafsi kujuta kwa kutokana na kushughulika na mambo ya dunia ambayo ndio sababu kubwa ya kujikuta mtu yuko kwenye 'ghaflah' (kughafilika na Aakhirah), kusahau kama mauti yako tayari kwa yule iliyomfikia ajali yake bila ya kujua lini au wapi ameandikiwa, kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

(( وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ))

((Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari)). [Luqmaan: 34].

 

Kwa hiyo inapomfikia mtu ajali yake na roho inapotoka hapo nafsi tena hutambua kuwa yale yaliyokuwa yakimshughulisha duniani hayana tena faida naye wala hayawezi kumsaidia wakati huu, ndipo hubaki kujuta na kutambua kuwa yupo katika hasara kubwa!     

Tunaona jinsi gani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) anavyotoa onyo au tanabahisho kwa mwanaadam kwa kughafilika na dhikr (ukumbusho) wa Allaah, na kuendekeza dunia na mapambo yake. 

 

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّهِ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ))

((Enyi walioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Allaah. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri)). [Al-Munaafiquwn: 9]

 

Bali mwana Aadam ni mwingi wa kusahau na kughafilika, pamoja na maonyo na tanbihi zote hizo za Mola wake lakini dunia imemzamisha na kuyanywa maji yake yaliyomlewesha na hadi kutojitambua, mwisho wake ni majuto yale yale ya  kutamani kurudishwa duniani afanye mema:

 

((وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَى أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ))  

((Na toeni katika tulichokupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema)). [Al-Munaafiquwn: 10].

 

Lakini wapi! 

 

((وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّهُ نَفْسًا إِذَا جَاء أَجَلُهَا وَاللَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ))  

((Wala Allaah Hatoiakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake; na Allaah Anazo khabari za mnayo yatenda)). [Al-Munaafiquwn: 11].

 

Na vilevile Kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tena katika Suratul-Muuminuwn:

 

((حَتَّى إِذَا جَاء أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ))  

((Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu! Nirudishe))

 

((لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَى يَوْمِ يُبْعَثُونَ))

((Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapofufuliwa)). [Al-Muuminuwn: 99-100].

 

 

Share