Mawlid: Kusoma Maulidi Kwenye Harusi Badala Kupiga Ngoma Inafaa?

SWALI:

 assalam laykum

napenda kuuliza juu ya hizi harusi zetu, nafaham kwamba harusi yenye ngoma haifai jee kama kumefanywa maulidi ya wanawake naweza kuhudhuria harusi hio naomba nifahamiswe kwani tuna mitihani juu ya ufanyaji wa harusi zetu

 


 

 

JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako muhimu. Mara zote tunapoacha Sunnah sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa tunaingia katika Bid‘ah. Jambo hili linatupunguzia sisi mema yetu katika mizani yetu ya mambo mema.

 

Haifai kwetu sisi kuondosha munkar (ovu) moja kwa kuleta ovu jengine. Inatakiwa sisi tuwe na msimamo, je Qur-aan imesema nini na Hadiyth sahihi zinatueleza nini? Hebu tumsikilize kipenzi chetu anatueleza nini kuhusu haya: “Mwenye kuzua katika hili jambo letu lisilokuwamo humo litakataliwa” (al-Bukhaariy na Muslim). Katika riwaya ya Muslim: “Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa”. Kila mmoja wetu ajiulize na awe mkweli katika jibu lake: Je, kusoma kwangu maulidi katika Nikaah huwa ninataka nini? Kila mwenye kusoma atakuambia kuwa hiyo ni ‘Ibaadah hivyo anatarajia thawabu.

 

Swali jengine ni, je amali hii ninayoifanya imewafikiana na sheria na Uislamu wangu ninaoufuata au vipi? Ikiwa unakwenda kinyume na sheria basi kila mwenye kufanya ataruka patupu. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Asizifanye amali zetu kuruka patupu! Tuitazame ayah ifuatayo: “Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Kukutimizieni neema Yangu na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu” (5: 3). Imaam Maalik aliielezea ayah hii kwa kusema: “Lolote ambalo halikuwa Dini wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haliwezi kuwa Dini sasa”. Hii ina maana Dini imekamilika hatuwezi kuikamilisha zaidi ya hapo wala sisi hatuna daraja ya kuja kumkosoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yeye alifanya khiyana hakufikisha mengine ambayo alikuwa afaa atufikishie hivyo sisi Waislamu wa sasa tumekuja tukakamilisha hayo.

 

Maulidi katika hali ya kawaida hayafai, seuze katika ‘Ibaadah ya ndoa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo kuwa katika Nikaah kusomwe khutbah ya kuwafunganisha wanandoa. Baada ya ndoa na nje ya Msikiti wanawake wakiwa katika sehemu zao za sitara bila ya kuwa wanaume wamo ndani wanaweza kupiga dufu (twari) kavu na kuimba nyimbo zenye maana mazuri kama alivyofundishwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Tutosheke na hayo na kufanya hivyo kutatupunguzia sisi mengi sana. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atutilie tawfiki katika ndoa zetu na Atuepushie mabid‘ah kwayo.

 

Soma jibu katika kiungo kifuatacho chenye maelezo ya sherehe za ndoa:

 

 Yanayopasa Na Yasiyopasa Katika Sherehe za Ndoa

 

Vile vile usiache kusoma vitabu vya ndoa vilivyoko kwenye ALHIDAAYA, tunakuwekea hapa baadhi yake, na vingine vipo njiani karibuni inshaAllaah

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share