Sababu Za Kuharibika Ndoa Nyingi Ulaya

 

 SWALI:

ASSALAM alykum wa -RAHMA tuh wa barakatuh.  MWENYEZI MUNGU akujaliyeni kila la kheri na afya njema. Nina shukuru kwa msaada wenu na kwakujitolea kutu elimisha.

Swaali langu nikuomba kuelimishwa mimi na wenzangu kuhusu maisha tunao kwa wakazi wa europa. Ni kwanini ndoa nyingi zinaharibika kwa mwaka hii??? 

Samahani kwa kiswahili changu. Kila lakheri  

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu sabab u za kuharibika ndoa Ulaya.

Sababu za kuharibika ndoa nyingi hasa Ulaya na sehemu nyingine kwa ujumla ni nyingi zikiwemo kama hizi:

 

Zifuatazo zinamhusu mwanamke:

1.     Kutokuwa au kutokuwepo mapenzi kwa mmoja wa wanandoa wawili mume au mke; au kwa wote wawili.

 

2.      Mwanamke kutokuwa na akhlaaq nzuri.

 

3.     Kwa mwanamke kutomtii au kutomsikiliza mumewe katika mambo mema; kama vile akimuamrisha kuswali akawa hataki kuswali, akimwambia avae hijabu akawa hataki kuvaa, akimwambia asende harusini/sherehe za birthdays akawa hataki, akimwambia shoga yako huyu simtaki katika nyumba yangu au sitaki awe shoga yako na akawa hataki.

 

4.     Mwanamke kutomjali mumewe na kutohisi kuwa ana haki, kama vile mke akawa anatoka bila ya idhini ya mumewe; mke kutomjali wala kutomshughulikia mumewe wakati anarudi nyumbani kwa kumpokea kumkaribisha kwa uzuri, kumtayarishia chakula, kumfulia nguo zake na kadhalika; mtamsikia mke akimwambia kuwa kama wewe unavyochoka basi na mimi vile vile nachoka basi jitengezee chakula mwenyewe na kadhalika.

 

5.     Mwanamke kunuka kuwa na harufu mbaya iwe kunuka mdomo au jasho au kupuu na kutojali bali mume akimwambia unanuka hujibu kwa kusema na yeye pia unanuka, ikawa ni mashindano na kujibizana maneno.

 

6.     Kutokuwa na furaha wala bashasha wakati wa kukutana iwe kindoa au hata kama mmoja aliondoka na kurudi; bali kuhisi kuwa keshakuja kunidhibiti na kuninyang’anya uhuru wangu. 

 

7.     Kipato cha mwanamke ni jambo linalomtia kiburi na kumtoa zaidi adabu mwanamke na kumpelekea kutomjali mumewe na kumuona kuwa hana maana yoyote wala hana haja yoyote kwa huyo mume kwani anachokitaka katika mahitaji yake ya manunuzi anapata.

 

8.     Mwanamke kumiliki nyumba na kuona kuwa ana uwezo wa kumtimua na kumtoa mumewe katika nyumba wakati apendao na wala hakuna yeyote mwenye uwezo wa kumrejesha kama hataki.

 

9.     Mwanamke kuhisi kuwa hana haja ya mume. Bali mume si lazima kwani ni mzigo na wako wengi katika wanawake wenzake na wengine ni shoga zake hawana waume wa kuwashughulisha wala kuwashughulikia. Na kwa kuwa hawana waume basi huwa na uhuru wa kufanya walitakalo na kwenda watakapo wakati wautakao, na mwanamke huona kuwa hilo ni katika haki yake atoke atakapo na afanye atakalo bila ya kuulizwa. Na ikitokea mume kumuuliza huthubutu kusema mbona wewe sikuulizi unakwenda wapi na umetoka wapi wala mbona huniombi ruhusa unapotaka kutoka.

 

10.             Mwanamke kutojipamba na kuonyesha uzuri wake kwa kumvutia mumewe.

 

11.            Mwanamke kufanya kazi hasa hasa wengine hufanya kazi usiku na huku kumuacha mumewe nyumbani akihesabu saa huku akisahau jukumu lake katika nyumba kwa kisingizio kuwa amechoka kwa kazi ngumu azifanyazo.

 

 

Na katika sababu zenye kumhusu mume ni kama hizi:

 

1.     Mwanamume kutokuwa na tabia nzuri.

 

2.     Mwanamume kumdhulumu mwanamke na kutomtendea haki kwa kutomtimizia anayotakiwa amtimizie wa visingizio kama vile unafanya kazi kama ninavyofanya hivyo akawa hampi fedha wala hamnunulii mahitaji yake na kadhalika.

 

3.     Mwanamume kushindwa kumtimizia mkewe haki yake kwa kujituma kupita kiasi na kila anapodaiwa haki akawa hawezi kwa uchovu au vyenginevyo.

 

4.     Kupatikana kwa uasi kwa mmoja wao au kwa wote wawili jambo ambalo hupelekea kuharibika uhusiano baina yao kwa uasi huo mpaka ikafikia kupelekea kuachana.

 

5.     Mwanamume kutokufan ya kazi na kutegemea kipato cha mwanamke anachosaidiwa na serikali kwa udanganyifu n.k.

 

6.     Mwanamume kuwa mvivu na kutegemea serikali kumsaidia yeye kwa kudanganya serikali na pia kuwa na tabia za udanganyifu kwa kupata kipato cha haramu.

 

7.     Mwanamume kupoteza masaa mengi kwenye internet au tv kutazama mipira na upuuzi mwengine na kutothamini kutumia wakati wake na mkewe.

 

8.     Mwanamume kuwa na mahusiano na wanawake wengine nje ya ndoa.

 

9.     Mwanamume kutumia masaa mengi kazini na kufanya overtime nyingi hata akirudi nyumbani yu hoi na hana nafasi na mkewe.

 

10.            Mwanamume alioa kwa lengo la kudandia nyumba ya mke anayolipiwa na serikali ili abane matumizi na fedha zake atume makontena Afrika na kuanzisha miradi.

 

11.            Tabiya chafu za wanaume kama kuvuta sigara, kula mirungi na mengine yenye kumkirihisha mke na kumkosesha subira za kukaa na mume.

 

12.            Mwanamume kuoa mke mwengine.

 

13.            Mwanamume kupenda maovu kama kutaama picha za ngono na sinema zisizo na maadili.

 

14.            Mwanamume kutokuswali au kutokufanya ‘Ibaadah nyinginezo au kutoshikamana na Diyn kwa ujumla.

 

Mengine ambayo yanawahusu wote wawili ni haya yafuatayo:

 

1.     Mahusiano mabaya baina ya mke na wazee wa mumewe au mahusiano ya mume na wazee wa mke.

 

2.     Wazazi kuingilia kati ya ndoa ya watoto wao.

 

3.     Kutokuwa na Imani na Taqwa inayohitajika.

 

4.     Kutoijua Dini inavyohitajiwa kwa kila Muislamu.

 

5.     Watu kuingia katika ndoa bila ya kujua haki na majukumu yake.

 

6.     Ukabila na utaifa.

 

7.     Watu kuwa na ada za siri (kujichua na kujisugua).

 

8.     Watu kuwa na marafiki kabla ya kuoa au nje ya ndoa.

 

Na Alllaah Anajua zaidi

 

 

Share