Makundi Ya Jamaa'atu Tabliygh Kufanya Mikutano Misikitini, Kulala Na Kula Humo

 

Makundi Ya Jamaa'atu Tabliygh Kufanya

Mikutano Misikitini, Kulala Na Kula Humo

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaamu Aleykum Warahmatul-laahi Wabarakaatuh.

 

Kwanza kabisa natoa shukrani kwa maustwadhi wetu wa alhidaaya, kwa kutujiba maswali yetu kwa majibu yasiyokuwa na shaka wala utatanishi wowowte ndani yake. Inshaallah kama mnavotufanyia wepesi dini yetu, Twamuomba Allaah (subhanahu wa ta'aalaa) awafanyie tahfiif katika killa mnalo likurubia AMIIN.

 

Sheikh nilikuwa nauliza, Tabliiq {kutemblea killa msikiti na kufanya ijtimaa kwa mda wa siku kadha ikiwa mnakula humo msikitini na kulala humo ndani} inafaa? naomba jibu lililo wazi kwa kuwa wengi wetu wanahamu ya kujuwa. "jazaakumu Llaahu kheyr"

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika hilo kundi haliitwi Tabliiq kama ulivyoandika kwani kwa jina hilo itakuwa inahusisha kikundi chenye kufuata Sunnah kinavyoitwa nchini Uganda. Na Tabliiq hiyo ya Uganda na Tabliygh labda ulivyotaka kuelewa ni tofauti kabisa.

 

Tabliygh ambayo unakusudia wewe maana yake ni kufikisha ujumbe kwa wengine.

 

Ama wanayofanya jamaa hao wa Tabliygh kutembelea Misikiti na kuwawaidhia maamuma wa sehemu hiyo hakuna tatizo katika Dini kwani hiyo ni kutekeleza amri ya kufikisha ujumbe kwa kila mmoja. Na wakati wake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituma watu nje ya mji wa Madiynah ili kufikisha ujumbe kwenye vijiji, miji na vitongoji. Tatizo lililo kubwa ni kuwa hawa wenye kufikisha wengi katika hilo kundi la Tabliygh si wenye uwezo huo na si wenye elimu; hivyo inakuwa mara nyingi hutegemea kitabu kilichoandikwa na kiongozi wao kiitwacho ‘Fadhaail al-A’amaal’ ambacho kimejaa Hadiyth dhaifu na za kutungwa na visa vya israiliyaat vingi. Kadhaalika kundi hilo lina mambo mengi linalofuata yanayokwenda kinyume na Sunnah. Na hao walinganiaji wa kundi hilo kwa sababu hawana elimu ya kutosha na uwezo wa kupambanua, na pia kwa kufuata kwao Taqliyd (ufuataji wa kibubusa bila elimu) wamekuwa wanakitegemea kitabu hicho katika ulinganizi wao kuliko hata wanavyotegemea Qur-aan na Sunnah sahihi.

 

Kwa mtindo huo, haipendezi kuwaalika au kuwakaribisha watu wasio na elimu kwenye Msikiti kuja kulingania, bali wao ndio wanapaswa walinganiwe na wafundishwe mafunzo sahihi ya Qur-aan na Sunnah na kuepukana na mambo ya uzushi na ya kufuata kibubusa yaliyoanzishwa na muasisi wao ambayo mengi yanapingana na Qur-aan na Sunnah.

 

Ama kula ndani ya Msikiti hakuna tatizo kabisa kwani Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wanakula katika Msikiti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kulala humo bila ya wasiwasi. Kulikuwa na Swahaba hao (Radhwiya Allaahu ‘anhum) takriban sabiini waliokuwa wakiishi ndani ya Msikiti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakitekeleza haja zao hizo na kupata mafundisho ya Uislamu. Bora tu katika kufanya hayo Msikiti usiwe ni wenye kuchafuliwa au kutumia kwa njia ambayo si nzuri.

 

Bonyeza kiungo kiufatacho upate maelezo zaidi

 

Kundi Tabliygh Liko Katika Sheria Ya Kiislam?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share