Wamefariki Kabla Ya Kupewa Mirathi

SWALI: 

Swali lenyewe ni kama lifwatalo.baba amekufa na ameacha mke na watoto wawili.na hawo watoto wake wawili wako na watoto.baada ya muda mke wa baba kafariki kabla hajapewa mirathi yake.je mtoto wake anaweza kupewa mirathi ya mama yake ambayo angepashwa kupewa kutoka kwa mme wake aliyo fariki? 

 Swali la pili.baba kafariki na ameacha watoto wawili. na wajukuu wawili.baada tuu na  watoto wake wawili hawo wakafariki kabla hawajapewa mirathi yao.je;wajukuu hawo  wawili wanayo haki ya kumrithi babu yao?nazani swali zangu zimefahamika.na  ntashukuru ntapo pata majibu yake.na mungu  awaafikishe. Amin.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka siku ya mwisho.

Japokuwa swali lenyewe lina utata kwani muulizaji hakubaini jinsia ya watoto wa aliyefariki. Ikiwa hao waliotajwa ndio warithi wa pekee wa aliyefariki basi wirathi wake utagawanya kama ifuatavyo:

1)       Hapa mke wa aliyefariki atapata thumuni (1/8).

2)      Ikiwa watoto wote ni wa kiume watagawa wirathi sawasawa baina yao.

3)     Ikiwa watoto wote ni wasichana basi watapata thuluthi mbili (2/3) na kila mmoja atapata kiwango sawa cha mirathi.

4)   Ikiwa mtoto mmoja ni wa kiume na mwengine ni wa kike, mali ya aliyefariki itapigwa mafungu matatu, mawili katika hayo atapewa mtoto wa kiume na msichana atapata fungu moja.

Ikiwa mke wa aliyefariki naye alifariki kabla ya kupata sehemu yake katika wirathi basi sehemu yake hiyo itachang’anywa na mali yake nyengine ikiwa alikuwa nayo na baada ya hapo itagawanywa kwa warithi wake. Na bila ya shaka yeyote watoto wake wana sehemu yao maalumu. Lakini mgao utategemea wale watu waliobakia na wanamrithi huyo bibi aliyefariki.

 

Jibu kwa Swali la Pili: Wajukuu kawaida hawamrithi babu yao iwapo watoto wa babu wako hai. Na iwapo watoto wa babu wamekufa baada ya baba yao kuaga dunia kabla ya kupata sehemu yao ya mirathi, hao watoto watarithishwa ingawa wamekufa. Baada ya kufanya hivyo, hawa wazazi (ambao ni mababa) watarithiwa ile mali yao na watoto wao ambao ni wajukuu wa babu.

Tanbihi: Ieleweke kuwa wirathi unatolewa tu baada ya:

a)      Kulipwa madeni ya aliyefariki.

b)    Kutoa fungu ambalo ameusia aliyefariki kabla ya kuaga dunia kwake na kisheria halifai kuzidi thuluthi (1/3).

c)    Kutoa masrufu ya mazishi kwa mfano sanda, kaburi na mengineyo.

  

Tanbihi kwa wenye kuuliza Maswali ya Mirathi:

 

Ili maswali yenu yajibike haraka inatakiwa kuwa wale watu wote ambao wana ukaribu wa kidamu wa aliyefariki wawe ni wenye kuandikwa ili iwe hapana utata wowote. Na katika hayo tungependa watu wafuatao watiliwe maanani sana:

1.                 Kijana mwanamume.

2.                 Kijana mwanaume wa kijana mwanaume (mjukuu).

3.                 Baba.

4.                 Babu wa kwa baba.

5.                 Ndugu mume wa kwa baba na mama (khalisa).

6.                 Ndugu wa kwa baba.

7.                 Ndugu mume wa kwa mama.

8.                 Kijana mwanaume wa ndugu mume khalisa.

9.                 Kijana mwanaume wa ndugu mume wa kwa baba.

10.             Ami wa kwa baba na mama.

11.             Ami wa kwa baba.

12.             Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba na mama.

13.             Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba.

14.             Mume.

15.             Binti.

16.             Binti wa kijana mwanaume.

17.             Mama.

18.             Dada khalisa.

19.             Dada wa kwa baba.

20.             Dada wa kwa mama.

21.             Bibi mzaa baba.

22.             Bibi mzaa mama.

23.             Mke.

Hii itatusaidia sana katika kujibu maswali yenu ya mirathi. Shukran.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share